Kenya Kwanza haituwezi, Uhuru aambia wafuasi
NA BENSON MATHEKA
RAIS Uhuru Kenyatta ame – hakikishia wafuasi wake kwamba muungano wa Azimio La Umoja uko na nguvu kuliko ule wa Kenya Kwanza (KKA) unaoongozwa na naibu wake William Ruto.
Alipuuza Dkt Ruto na washirika wake wanaodai kuwa chama cha Jubilee kimeisha makali akisema ana imani kikiungana na ODM cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga na vyama vingine, watashinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Akitaja KKA kama hatari kwa nchi, Rais Kenyatta alisema kwamba Wakenya wanapaswa kuungana na sio kutenganishwa kwa misingi ya kisiasa.
“Tuko na mgombeaji wetu katika Azimio, tuko na rasilmali na uwezo na tutaingia katika kampeni kuelezea Wakenya
tuliyofanya kama serikali ya Jubilee na kwamba tunataka nchi iliyoungana,” Rais Kenyatta aliambia vijana zaidi ya 3,000 katika ikulu ya Nairo – bi Ijumaa . Alitaja vinara kwa Kenya kwanza Alliance kama wasiopenda usawa wa uwakilishi nchini ambao ni muhimu kwa nchi kuafikia viwango vya juu vya maendeleo.
“Suala ambalo limeathiri nchi hii ni ukosefu wa usawa katika uwakilishi miongoni mwa watu wetu ambao tulijaribu kutatua kupitia Mpango wa Maridhiano. Hata hivyo, watu wachache walipotosha Wakenya,” alisema Rais Kenyatta.
Bw Odinga na washirika wa Rais Kenyatta katika Jubilee wamekuwa wakivumisha Azimio la Umoja linalotarajiwa kusajiliwa kuwa muungano mkubwa wa kisiasa baada ya Februari 26.
Muungano wa Kenya Kwanza unaleta pamoja vyama vya United Democratic Alliance (UDA) ambacho Dkt Ruto aliunda baada ya kutofautiana na Rais Kenyatta, Amani National Congress cha Musalia Mudavadi na Ford Kenya cha Moses Wetangula.
Rais Kenyatta aliwataja watatu hao kama watu wasiotakia nchi mema kwa kuhubiri siasa za mgawanyiko badala ya kuunganisha Wakenya.
“Ili kufanikisha ajenda hii, ( ya kuunganisha nchi na kuhakikisha usawa wa uwakilishi serikalini) ni lazima tuchague kwa uangalifu viongozi wetu wa kisiasa tunapochagua uongozi mpya wa nchi hii, uongozi ambao hautaogopa kuendeleza ajenda ya vijana,” alisema.
Alikariri kuwa chama cha Jubilee kingali imara na kwamba kitaungana na vyama na miungano mingine kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Ushindi wa Azimio la Umoja, alisema, utahakikisha miradi ambayo serikali yake inaendeleza itakamilishwa.
“Wanaposema Jubilee imekufa, mnaona kile ambacho chama kimekuwa kikifanya. Tumeafikia mengi lakini kuna miradi ambayo haijakamilika na kwa hivyo kama Jubilee tunatoka nje ya ofisi kufanya sia – sa kamili,” alisema.
Aliendelea: “Na kwa kuwa baadhi wamekuwa wakipiga siasa tulipokuwa tukifanya kazi, tumesema tunataka muungano wa vyama vilivyo na maono sawa na yetu na pamoja tunajiunga na Azimio. Tuko na mgombea urais, tuko na pesa na vijana wako nasi,” alisema Rais Kenyatta.
Next article
Benki Kuu yapanga kupunguza ada za kutuma pesa