Connect with us

General News

Magavana 3 waahidi Raila kura za ‘zizi’ la Kalonzo – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Magavana 3 waahidi Raila kura za ‘zizi’ la Kalonzo – Taifa Leo

Magavana 3 waahidi Raila kura za ‘zizi’ la Kalonzo

PIUS MAUNDU NA BENSON MATHEKA

MAGAVANA wa Ukambani wamesisitiza kuwa wana uwezo wa kumsaidia kinara wa ODM, Raila Odinga kupenya katika eneo hilo bila msaada wa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Magavana hao, Dkt Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Kivutha Kibwana (Makueni), mnamo Ijumaa walimwambia Bw Musyoka kwamba wana uwezo wa kuwashawishi zaidi ya wapiga kura milioni 1.6 katika eneo hilo, wamuunge mkono Bw Odinga.

Watatu hao walimtaka waziri huyo mkuu wa zamani kutoshirikiana na Bw Musyoka katika juhudi zake za kupenya eneo hilo.

“Hatutaki mtu mwingine kumfanyia kampeni Bw Odinga katika eneo la Ukambani. Tunaweza kumsaidia Bw Odinga kupata kura katika eneo la Ukambani. Mtu yeyote ndani ya jamii yetu ambaye anasubiri kubembelezwa anapoteza wakati wake.

Ikiwa ni pesa anazotaka, anafaa kurejea kwetu tunaweza kumchangia,” Gavana Ngilu alisema baada ya kuandaa mkutano na wataalamu, viongozi wa kidini na wafanyabiashara katika mkahawa mmoja mjini Machakos.

Kauli yake ilijiri kufuatia minong’ono kwamba tayari Bw Musyoka anafanya mazungumzo na Bw Raila kwa lengo la wao kufanya kazi pamoja kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Duru katika mazungumzo hayo zinasema kuwa Bw Musyoka anataka achukuliwe kuwa kigogo wa kisiasa wa Ukambani na hivyo anapaswa kutengewa cheo cha juu katika serikali itakayoundwa na Bw Odinga.

Lakini Dkt Mutua na Bi Ngilu walimshutumu Bw Musyoka kwa kujitakia makuu katika mazungumzo kati yake na wagombeaji urais walioko vifua mbele katika kinyang’anyiro cha urais.

“Inaudhi kwamba anafanya hivyo kwa manufaa yake binafsi wala si jamii nzima ya Wakamba,” akasema Dkt Mutua.

Magavana hao walisema japo Bw Musyoka yu huru kuwaagiza wafuasi wake wamuunge mkono Bw Odinga, kujivuta kwake ni “hatari”.

“Huku ikisalia miezi mitano pekee kabla ya Wakenya kuelekea debeni, itatugharimu pakubwa ikiwa tutaendelea kupoteza wakati pasi na kuamua mrengo tutakaounga mkono.

Tunaunga mkono wafanyabiashara, viongozi wa kidini na wataalamu ambao tayari wameamua kuunga mkono vuguvugu la Azimio la Umoja,” akasema Profesa Kibwana.

Dkt Mutua na Prof Kibwana walikariri kuwa wameweka kando ndoto zao za urais ili kumuunga mkono Bw Odinga. Magavana hao wamepanga mikutano kadhaa eneo la Ukambani kumpigia debe Bw Odinga.

Bi Ngilu ni mwanachama wa bodi ya kampeni ya Bw Odinga inayoongozwa na Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi.

Duru zinasema kwamba mazungumzo yamekamilika kwa Bw Musyoka kujiunga na Azimio la Umoja la Bw Odinga kupitia muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Vinara wa OKA wamepuuza uwezekano wao kuungana na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Wadai kuwa wana uwezo wa kuwashawishi wapigakura takriban milioni 1.6 wa Ukambani wamuunge waziri mkuu wa zamani huku wakimhimiza aache ‘kumbembeleza’ aliyekuwa makamu wa rais ili amuunge mkono.