Connect with us

General News

Wanjigi atisha kuzima ndoto ya Raila kuingia Ikulu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wanjigi atisha kuzima ndoto ya Raila kuingia Ikulu – Taifa Leo

Wanjigi atisha kuzima ndoto ya Raila kuingia Ikulu

Na CHARLES WASONGA

MIKIMBIO ya kisiasa ya mfanyabiashara Jimi Wanjigi sasa inaonekana kuwakosesha usingizi vigogo wa ODM kwani ametisha kuvuruga safari ya kiongozi wa chama hicho, Raila Odinga ya kuingia Ikulu.

Bw Wanjigi ametisha kuwasilisha kesi kortini kupinga kuandaliwa kwa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) la chama hicho ikiwa uteuzi wa mgombea urais hautaorodheshwa kama mojawapo ya ajenda ya mkutano huo.

Anadai notisi iliyochapishwa magazetini wiki jana kuhusu mkutano ni haramu kwani  haikuorodhesha suala hilo kama ajenda kuu, kuambatana na hitaji la Katiba ya ODM.  Mkutano huo umeratibiwa kufanyika katika uwanja wa michezi wa Nyayo, jijini Nairobi Februari 25 na 26.

Mnamo Jumatano, kundi la wajumbe wa ODM kutoka maeneo ya Mlima Kenya na Mashariki mwa nchi na wanaomuunga mkono Bw Wanjigi walitoa makataa ya wiki moja kwa chama hicho kujumuisha uteuzi wa mgombea urais katika notisi hiyo la sivyo waelekee kortini kuzima NDC hiyo.

“Ikiwa matakwa yetu hayatatimizwa ndani ya siku saba zijazo, tutawasilisha kesi kortini kusitisha kongamano hilo. Tayari tumeandika barua kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa nan a Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya ODM (NEB) kuhusu suala hili muhimu,” Bw John Njenga ambaye ni mjumbe wa ODM kutoka Nyandarua alisema kwenye kikao na wanahabari katika mkahawa wa Panafric, Nairobi.

Awali, Bw Wanjigi alikuwa amemwandikia barua Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna akitaka notisi kuhusu NDC hiyo ifutiliwe na nyingine itolewe yenye ajenda kuhusu uteuzi wa mgombeaji urais.

“Kama mwanachama wa ODM wa maisha ambaye anasaka tiketi ya chama ili niwanie urais nahisi kwamba haki zangu zimekiuka kwa kutojumuishwa kwa suala la uteuzi wa mgombeaji urais katika ajenda ya NDC. Kulingana na Katiba yetu kongamano hili hufanyika mara moja baada ya miaka mitano ambapo mgombeaji wa urais wa huteuliwa,” akaeleza.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi amemjibu Bw Wanjigi kwa kudai kuwa mfanyabiashara huyo hana usemi kuhusu ajenda ya mkutano wa asasi hiyo yenye mamlaka makuu zaidi katika chama hicho cha Chungwa.

“Mbona anataka kuvuruga shughuli za chama?. Awasilishe ajenga anayotaka kwa Baraza Kuu la ODM (NEC). Na asiposikizwa anaweza kuwasilishwa malalamishi yake kwa Jopo la Kutatua Mizozo ndani ya Vyama vya Kisiasa (PPDRT),” Bw Mbadi akaambia safu hii kwa njia ya simu.

“Yu huru kwenda mahakamani lakini afahamu kwamba majaji watamshauri awasilishe malalamishi yake katika asasi husika za chama kwanza. Wanjigi ni mwanachama wa ODM na ana haki ya kusikizwa. Aachane na mbio nyingi zisizo na manufaa kwake na kwa chama,” anaongeza mbunge huyo wa Suba Kusini.

Wadadisi wanasema endapo Bw Wanjigi atafaulu kuzima kongamano hilo la NDC, atakuwa amevurugwa mipango ya ODM ya kumwidhinishwa Bw Odinga kama mgombeaji wake wa urais ili kutoa nafasi chama hicho kuungana na vyama vingine chini ya mwavuli wa muungano wa Azimio la Umoja.

“ODM inafaa kuchukulia malalamishi ya Bw Wanjigi kwa uzito kwani anaweza kuvuruga hesabu zake za katika kubuni muungano utakaomwezesha Bw Odinga kuingia Ikulu kwa tiketi ya Azimio la Umoja,” anasema Bw Martin Andati ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

NDC ya ODM itafanyika siku moja na ile ya chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Duru zinasema kuwa wajumbe wa vyama hivyo viwili wanatarajiwa kumwidhinisha Bw Odinga kuwa mgombea urais wa muungano wa vyama hivyo chini ya mwavuli wa Azimio la Umoja.

Vyama vingine 12 pia vimetangaza kutia saini mkataba wa kuwa vyama tanzu chini ya muungano huo na kumuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.