Hofu mabwanyenye wameteka chama cha ODM Pwani
MAUREEN ONGALA NA VALENTINE OBARA
WASIWASI umeibuka miongoni mwa baadhi ya wanachama wa ODM wanaolenga kutafuta tikiti za kuwania nyadhifa tofauti katika uchaguzi ujao maeneo ya Pwani, wakilalama kuwa huenda wanachama matajiri wakapendelewa.
Wanachama hao, wengi wao wakiwa ni vijana, wameelezea hofu kuwa huenda wakakosa kutendewa haki wakati wa mchujo chamani.
Hofu hii imeibuka baada ya baadhi yao kupewa fursa ya kufadhili shughuli za chama ambazo ni pamoja na mikutano ya kisiasa.
Duru ziliambia Taifa Leo kuwa, waandalizi wa mikutano hutumia nafasi hiyo kuwaziba midomo wapinzani wao wanaotaka kushindania tikiti moja nao huku wakijionyesha kuwa waaminifu zaidi kwa wakuu wa chama.
Haya yanajiri wakati chama hicho kinatarajiwa kuongoza mikutano ya hadhara Pwani kuanzia wikendi kuvumisha Muungano wa Azimio La Umoja kwa maandalizi ya uchaguzi ujao.
Kulingana na ratiba iliyotolewa kwa umma, mikutano hiyo imepangwa kufanyika Kaunti za Kilifi, Mombasa, Kwale na Taita Taveta kuanzia Jumamosi hadi Jumanne.
Mwanachama aliyeomba jina lake libanwe kwa kuhofia kuadhibiwa kwa kuzungumzia masuala hayo hadharani, alitoa mfano wa vurugu zilizoshuhudiwa katika mkutano wa chama Kilifi wikendi iliyopita.
Mwanachama huyo alisema, mkutano huo ulipaswa kuwa wa wajumbe na wagombeaji watarajiwa pekee lakini waandalizi ambao ndio wafadhili, wakaamua kuingiza makundi ya vijana waliotatiza wapinzani wao.
“Haieleweki ilikuwaje hadi maafisa wakaruhusu pia wafuasi ambao si wajumbe wala wanaotaka tikiti za ugombeaji kuingia mkutanoni,” akaeleza. Mwenyekiti wa ODM katika Kaunti ya Kilifi, Bw Teddy Mwambire, alithibitisha kuwa mkutano huo ulikuwa umefadhiliwa na mmoja wa wanasiasa wanaotaka tikiti ya chama kuwania ugavana katika uchaguzi ujao.
Hata hivyo, aliondolea wanachama hofu ya mapendeleo kwa msingi huo akisema kutakuwa na hafla nyingi ambazo chama kitaandaa katika maeneo tofauti na kila anayetaka tikiti ya chama, atapata nafasi kutoa mchango wake wa kifedha.
“Tunashirikiana kama chama. Siku nyingine mtu mwingine ndiye atafadhili. Kuna mikutano mingi inayopangiwa kufanyika ikiwemo ya wanawake, vijana, na walemavu kwa hivyo tutashirikiana kwa upendo na umoja,” akasema.
Kiongozi wa vijana, Bw Fikirini Jacobs, alieleza wasiwasi kuwa mpango wa chama kutaka wagombeaji washauriane ili kuepusha kura za mchujo, huenda ukapendelea baadhi ya wawaniaji.
ODM ilikuwa imetangaza kuwa itazingatia mbinu mbalimbali kuchagua wagombeaji ikiwemo kura za maoni kutambua walio maarufu zaidi, mashauriano kati ya wagombeaji kuunga mkono mmoja wao, uchaguzi utakaofanywa na wajumbe, mbali na kura ya mchujo itakayohusisha wanachama ambayo ni mbinu ya mwisho kabisa itakayozingatiwa.
Next article
Jenerali Badi ajikuta katika kashfa ya ardhi