Wakenya milioni 5 bado hawajaamua ni Ruto au Raila
MERCY SIMIYU na JOSEPH WANGUI
KARIBU wapigakura milioni 5 hawajaamua iwapo watampigia kura Naibu Rais Dkt William Ruto au Kinara wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Kwa mujibu wa utafiti wa Kampuni ya Trends & Insights for Africa (Tifa), asilimia 20 ya wapigakura hawajafanya uamuzi wa nani watakayemchagua, hiyo ikiwa ni sawa na watu milioni 5. Hii inatokea wakati ambapo zimesalia siku 172 kabla ya uchaguzi mkuu kuandaliwa.
Utafiti huo kwa mara nyingine ulimweka Dkt Ruto kifua mbele kwa asilimia 38 huku Bw Odinga akimfuata kwa asilimia 27. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa hakuna mwaniaji wa Urais ambaye ana uwezo wa kufikisha zaidi ya asilimia 50 jinsi inavyohitajika kikatiba na kushinda duru ya kwanza ya uchaguzi.
Ili kupata ushindi katika raundi ya kwanza, lazima apate zaidi ya asilimia 25 katika zaidi ya kaunti 24 kati ya kaunti zote 47.
Kwenye utafiti huo ambao ulifanyika kati ya Februari 3-9, Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka alishikilia nafasi ya tatu kwa asilimia mbili pekee. Wapigakura 1,541 kutoka iliyokuwa mikoa minane waliohojiwa na utafiti huo ulikuwa na tofauti ya kiwastani ya asilimia 2.49.
Aidha, asilimia 27 ya wapigakura wanamtaka Naibu Rais ametue Kinara wa ANC Musalia Mudavadi kama mgombeaji mwenza wake. Wengine waliotajwa ni Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru (asilimia 15) mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua (asilimia 11) na Bw Musyoka (asilimia nane).
Kwa upande wa Bw Odinga, asilimia 41 wanamtaka amteue aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth kama mwaniaji mwenza.
Utafiti huo pia ulionyesha kuwa UDA anayoiongoza Dkt Ruto ndiyo maarufu zaidi kwa asilimia 35 ikifuatwa na ODM kwa asilimia 24. Hata hivyo, asilimia 26 ya wapigakura bado hawafahamu ni chama kipi ambacho wanafaa kukiunga mkono.
UDA ni maarufu sana katikati mwa Bonde la Ufa kwa asilimia 60 huku ODM ikitawala Nyanza kwa asilimia 55.
Wakati huo huo, Dkt Ruto amejumuishwa kwenye kesi ya mwanaharakati Okiya Omtata ambayo inalenga kumzuia kuwania kiti cha Urais.
Bw Omtata kwenye kesi yake, anataka mahakama imwaamrishe Dkt Ruto na wanasiasa wengine wanaoshikilia vyeo wajiuzulu kabla ya vyama kufanya uteuzi na kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Kando na Naibu Rais, wengine ambao Bw Omtata anataka wajiuzulu ni Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na Gavana wa Murang’a Mwangi Wa Iria.
Bw Omtata anadai kuwa sheria inabagua kwa kuwataka watumishi wa umma wajiuzulu na wakati huo huo kuwaruhusu wengine waliochaguliwa kuendelea kuhudumu katika nyadhifa zao.
Aidha mwanaharakati huyo wa haki za kibinadamu anataka mahakama itoe uamuzi kuwa Rais, Naibu Rais, Gavana na Naibu Gavana hawafai kuchaguliwa katika nyadhifa nyingine ila tu hizo walizoshikilia.
Next article
Hofu mabwanyenye wameteka chama cha ODM Pwani