CHARLES WASONGA: Serikali isiache vyuo vikuu viangamizwe na madeni
NA CHARLES WASONGA
SHUJAA wa ukombozi wa Afrika Kusini hayati Nelson Mandela aliwahi kusema kauli hii kuhusu elimu: “Elimu ni silaha yenye nguvu zaidi ambayo unaweza kutumia kubadilisha ulimwengu.”
Mandela, ambaye ni rais wa kwanza mweusi nchini humo, alimaanisha kuwa elimu husaidia watu kupata ufahamu, fikra pevu, uwezo na ujuzi hitajika kufanya ulimwengu kuwa mahala pema
Hii ina maana kuwa elimu ndiyo huzalisha nguvu-kazi inayohitajika kuendesha gurudumu la maendeleo humu nchini na kote ulimwenguni.
Kwa sababu hii, Wizara ya Elimu hutengewa kiasi kikubwa zaidi cha pesa za bajeti ya kitaifa kila mwaka nchini kufadhili mipango mbalimbali.
Lakini inasikitisha kuwa Serikali Kuu haijachukua hatua zozote kushughulikia changamoto za kifedha zinazozonga vyuo vikuu vya umma wakati huu.
Kwa mfano, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Moi, Humphrey Njuguna juzi aliungama kwamba taasisi hiyo imelemewa na mzigo wa madeni ya kima cha Sh5 bilioni.
Mbali na usimamizi mbaya wa kifedha katika chuo hicho, inasemekana kuwa hali hiyo imechangiwa na hali ya serikali kuu kupunguza ufadhili kwa vyuo vikuu vya umma, kupungua kwa mapato baada ya kufungwa kwa mabewa kadha, idadi kubwa ya wafanyakazi na kupungua kwa idadi ya wanafunzi kutoka 50,000 hadi 30,000.
Hali ni hiyo hiyo katika Chuo Kikuu cha Egerton ambacho kilifungwa Novemba 26, 2021 kufuatia mgomo wa wahadhiri.
Naibu Chansela wa chuo hicho Prof Isaac Kibwage anasema kuwa taasisi hiyo inahitaji Sh6 bilioni kuiwezesha kujinasua kutoka kwenye minyonyoro ya madeni.
Chuo Kikuu cha Nairobi na kile cha Kenyatta vilevile vinakabiliwa na tatizo lilo hilo la madeni na shinikizo za wahadhiri wanaotaka waongezewe mishahara na marupurupu mengineyo.
Kwa mfano, kutokana na mzigo wa madeni na kupungua kwa mapato, usimamizi wa Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka jana uliamua kuongeza karo kwa wanafunzi wapya kutoka Sh26,500 to Sh59,000.
Hatua hii iliibua manung’uniko makubwa kutoka kwa wanafunzi, ambao wengi wao wanatoka jamii masikini.
Bodi ya Kutoa Mikopo kwa Elimu Juu (HELB) pia inakabiliwa na uhaba wa pesa kiasi kwamba imeshindwa kutoa mikopo kwa wengi wa wanafunzi waliotuma maombi kwa sababu hupokea pesa kidogo kutoka kwa hazina ya kitaifa.
Katika hali hii, vyuo hivi vikuu vinakabiliwa na hatari ya kufungwa kabisa ikiwa serikali kuu haitachukua hatua za haraka kuvinusuru. Serikali kuu inafaa kubuni mikakati mbadala ya kuongeza ufadhili kwa vyuo hivi ambavyo ni baadhi ya vile vikongwe zaidi nchini. Kwa mfano, serikali ifutilie mbali au iunganishe baadhi ya mashirika yake ambayo hayaleti faida yoyote.
Pili, sheria za vyuo vikuu ifanyiwe mabadiliko ili kutoa nafasi kwa wanafunzi wa zamani wa vyuo hivyo wahusishwe katika usimamizi wazo na mipango ya uzalishaji mapato zaidi.
Sh8.5 bilioni ambazo Hazina ya Kitaifa ilitengea kwa ajili ya kusaidia vyuo vikuu vya umma nchini ni sawa na tone ya maji baharini.
Inakadiriwa kuwa vyuo taasisi hizo zinahitaji zaidi ya Sh50 bilioni ili kuziokoa kutoka kwa lindi la madeni.