Chelsea kukosa tegemeo Mount, Hudson-Odoi na Chilwell dhidi ya Lille kwenye UEFA
Na MASHIRIKA
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Chelsea, watakosa maarifa ya fowadi Mason Mount watakapoalika Lille kwa hatua ya 16-bora leo Jumanne usiku, ugani Stamford Bridge.
Ingawa Mount amerejelea mazoezi baada ya kupona jeraha alilopata wakati wa kampeni za Kombe la Dunia mwanzoni mwa mwezi huu, kocha Thomas Tuchel amefichua kwamba itakuwa mapema sana kuanza kumwajibisha katika michuano ya haiba kubwa.
Callum Hudson-Odoi, Reece James na Ben Chilwell ni masogora wengine ambao Tuchel amebainisha kwamba hawatakuwa sehemu ya kikosi chake dhidi ya Lille ambao ni wafalme wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1). Hata hivyo, nafuu zaidi ni kupona kwa beki Cesar Azpilicueta.
Huku Lille wakitegemea zaidi maarifa ya fowadi raia wa Uturuki, Burak Yilmaz na mvamizi wa timu ya taifa ya Canada, Jonathan David, Chelsea wataweka matumaini makubwa kwa Romelu Lukaku na Hakim Ziyech.
Chelsea walikamilisha kampeni za Kundi H katika nafasi ya pili kwa alama 13 baada ya kushinda mechi nne, kuambulia sare mara moja na kupoteza mchuano mmoja.
Matokeo hayo yaliwaweka nyuma ya miamba wa Italia, Juventus. Chelsea waliokomoa Palmeiras ya Brazil 2-1 mnamo Februari 12 na kutawazwa mabingwa wa dunia, sasa hawajapoteza mechi yoyote kati ya tano zilizopita katika mashindano yote.
Watajibwaga ugani wakipania kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 1-0 dhidi ya Crystal Palace katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Februari 19 ugani Selhurst Park. Kwa sasa wanakamata nafasi ya tatu ligini kwa alama 50 kutokana na mechi 25.
Hadi walipotawazwa wafalme wa UEFA mnamo 2020-21, walikuwa wamedenguliwa katika hatua ya 16-bora ya kipute hicho mara nne mfululizo. Ingawa rekodi hiyo, inafanya Chelsea kutokuwa miongoni mwa vikosi vinavyopigiwa upatu wa kutwaa taji la UEFA muhula huu, miamba hao wanajivunia uthabiti mkubwa chini ya Tuchel.
Mbali na kushinda mechi nne zilizopita za UEFA ugani Stamford Bridge bila kufungwa bao, Chelsea hawajapoteza mchuano wowote katika uwanja wao wa nyumbani tangu Septemba 2021.
Lille watashuka dimbani wakilenga kujinyanyua baada ya Metz kuwalazimishia sare tasa katika mechi iliyopita ya Ligue 1. Kikosi hicho kinachoshikilia nafasi ya 11 kwa alama 36 ligini kimeshinda mechi mbili pekee kutokana na saba zilizopita katika mashindano yote.
Nafuu zaidi kwa Chelsea ni rekodi duni ya Lille ambao hawajawahi kukamilisha mechi ya UEFA ugenini bila kufungwa tangu 2014.
Lille wamewahi kutinga hatua ya 16-bora ya UEFA mara moja pekee mnamo 2006-07 ambapo walibanduliwa na Manchester United kwa jumla ya mabao 3-0. Chelsea iliwatinda 2-1 katika mikondo miwili ya makundi ya UEFA mnamo 2019-20.
Chelsea watavaana na Liverpool kwenye fainali ya Carabao Cup mnamo Februari 27, 2022 ugani Wembley.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
Next article
STEVE ITELA: Wahifadhi mazingira wakataa marekebisho ya…