Uhuru atafanikiwa kutikisa Mlima Kenya?
NA MWANGI MUIRURI
RAIS Uhuru Kenyatta anaenda Ikulu ya Sagana, Kaunti ya Nyeri leo Jumatano akiwa amejihami vikali kujaribu kubomoa ufuasi mkubwa anaofurahia naibu wake William Ruto eneo la Mlima Kenya.
Kulingana na wanasiasa wakereketwa wa chama cha Jubilee, lengo la mkutano wa leo Jumatano ni kuweka mikakati ya ‘kummaliza’ Dkt Ruto kisiasa katika eneo hilo lenye kura nyingi.
Walieleza Taifa Leo kuwa mkutano wa leo utakuwa pia msingi wa kongamano la kitaifa (NDC) la Jubilee litakaloandaliwa Ijumaa hasa kuhusu ushirikiano baina yake na ODM chake Raila Odinga.
Kongamano la ODM pia limepangwa kufanyika siku hiyo hiyo, hatua ambayo wachanganuzi wanasema imepangwa kutumika kwa vyama hivyo kupitisha azimio la kushirikiana na kumuidhinisha Bw Odinga kuwa mgombea wao wa urais Agosti 9.
Suala lingine kuu ambalo limo kwenye ajenda ya leo Jumatano ni kujadili kuhusu madaraka ambayo wafuasi wa rais watapewa katika muungano wa Azimio la Umoja iwapo utashinda urais.
Rais pia anatarajiwa kuongoza mjadala kuhusu uwezekano wa washirika katika Azimio kufanya uteuzi wa pamoja wa wagombeaji. Baadhi ya wajumbe hali kadhalika wanashinikiza kuteuliwa ama kuchaguliwa kwa maafisa wapya wa Jubilee.
Wandani wa Rais Kenyatta walieleza Taifa Leo kuwa wamepatia Idara ya Ujasusi (NIS) na maafisa wa utawala wa mikoa wakiwemo machifu jukumu la kutambua wajumbe watakaohudhuria kikao cha Sagana ili kuzuia wandani wa Dkt Ruto kupenya.
Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe anasema mkutano huo utahudhuriwa tu na watu ambao uaminifu wao kwa Rais Kenyatta hautiliwi shaka.
“Huu ni mkutano wa kusafisha nyumba ya Jubilee na utahudhuriwa na wale tu ambao hawajawahi ‘kumdharau rais’ na chama ama kukosa uaminifu kwake,” akasema Bw Murathe.
Kulingana na Mwenyekiti wa Jubilee katika Kaunti ya Kirinyaga, Muriithi Kang’ara, wajumbe watatumia mkutano wa leo kushinikiza kuadhibiwa kwa wanasiasa ambao “wamekosa uaminifu kwa rais.”
“Hatutaki yeyote ambaye amejihusisha na chama kingine kukubaliwa kuingia Sagana ama NDC. Pia tutamuomba rais aidhinishe watu hao wapokonywe walinzi na magari ya serikali,” akasema Bw Kang’ara.
Kumaliza Ruto Kisiasa
Anapoelekea mlimani katika jitihada za kushawishi wenyeji kumuunga mkono Bw Odinga awe rais wa tano wa Kenya, Rais Kenyatta anafahamu kuhusu umaarufu wa Dkt Ruto mashinani.
Dkt Ruto amekuwa akijipigia debe eneo hilo kwa zaidi ya miaka minane sasa, hali ambayo imemweka guu moja mbele ya wapinzani wake wa urais katika Mlima Kenya.
Wachanganuzi wa siasa wanasema Rais Kenyatta ana kibarua kigumu kumuuza Bw Odinga eneo hilo kutokana na kile wanasema ni hisia za wengi kwamba amepuuza maslahi yao ya kiuchumi.
Ni katika kutambua malalamiko kuhusu kiuchumi ambapo serikali sasa inapanga kujaribu mbinu za kutuliza hasira zao.
Waziri wa Kilimo, Peter Munya aliambia Taifa Leo kuwa wenyeji wa Mlima Kenya wataanza kushuhudia maendeleo ya haraka na pia watapata nafasi ya kutangamana na rais ana kwa ana. Tangu 2018 imekuwa nadra kwa Rais Kenyatta kuzuru maeneo hayo.
“Tutapunguza bei ya pembejeo za kilimo, miradi inayoendelea itakamilishwa na wafanyabiashara watasaidiwa. Tuko na imani kwamba tutafanikiwa kushawishi wapiga kura watuunge mkono,” akasema Bw Munya.
Hata hivyo, Seneta wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata, ambaye ni wa mrengo wa Dkt Ruto anasema: “Shida ni kwamba wamechelewa kwa kuwa wangefanya hayo kitambo. Hawangengoja mpaka kiburi cha washauri wa rais kimtenganishe na wenyeji.”
Kiongozi wa wengi bungeni, Amos Kimunya anasema rais amejipanga kuhakikisha mwelekeo wa Mlima Kenya kisiasa ni ndani ya Azimio la Umoja.
Kwa upande wake aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth anasema kunahitajika tu mikutano mikubwa kadhaa ambapo rais atajitetea kwa wenyeji wa Mlima Kenya.
“Rais wetu ana ujanja wa kipekee wa kisiasa. Ni mweledi wa hotuba na anajua kushawishi wakazi,” asema Bw Kenneth.