Connect with us

General News

Ruto afukuzwa kutoka Jubilee – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Ruto afukuzwa kutoka Jubilee – Taifa Leo

Ruto afukuzwa kutoka Jubilee

BENSON MATHEKA Na CHARLES WASONGA

NI rasmi sasa kwamba, Naibu Rais William Ruto sio Naibu Kiongozi wa chama cha Jubilee baada ya kuvuliwa wadhifa huo katika kongamano la kitaifa la wajumbe (NDC) lililofanyika Jumamosi.

Uamuzi huo ulitolewa Jumamosi katika kongamano la kitaifa la wajumbe (NDC) wa chama hicho tawala katika uwanja wa jumba la mikutano ya kimataifa la KICC, Nairobi.

Wadhifa huo sasa umegawanywa kwa vitengo vinne, ambavyo vilipewa Mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini Jimmy Angwenyi, Mbunge wa Taveta Naomi Shabaan, aliyekuwa Seneta wa Kajiado Peter Mositet na aliyekuwa Mbunge wa Buuri Kinoti Gatobu; kila mmoja akishughulikia masuala tofauti ya chama.

Wajumbe wa Jubilee vile vile waliamua kwa kauli moja kuondoa jina la Dkt Ruto na wanasiasa wandani wake ambao waliasi chama hicho kwa kujihusisha na chama cha United Democratic Alliance (UDA).

“Wanachama wote wa chama cha Jubilee ambao wamekuwa wakiendeleza sera na itikadi za vyama vingine watachukuliwa kama watu ambao wamekoma kuwa wanachama wa Jubilee na hivyo majina yao yameondolewa kutoka orodha ya chama,” wajumbe wa chama hicho waliamua.

Lakini mapema mwaka 2021, Dkt Ruto alipinga vikali njama ya kufurushwa kwake kutoka chama hicho, akishikilia kuwa ndiye mwasisi wake.

“Hamuwezi kuniondoa ODM na kisha mnifuate tena kuniondoa kutoka Jubilee, nyumba ambayo nilishiriki katika ujenzi wake,” akasema akilaumu handisheki ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Dkt Ruto alidai handisheki ilikuwa ya kuvunja Jubilee na kumtimua serikalini.

Hata hivyo, licha ya kuondolewa kwa jina la Dkt Ruto kutoka orodha ya wanachama wa Jubilee, mwanasiasa huyo ataendelea kushikilia wadhifa wake wa Naibu Rais.

Hii ni kwa sababu hatua hiyo sio mojawapo ya sababu za kuondolewa afisini kwa mshikilizi wa kiti hicho kwa mujibu wa kipengele cha 150 cha Katiba ya sasa.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta aliidhinishwa kwa kauli moja kuendelea kuhudumu kama kiongozi wa chama hicho.

Hatua hiyo itamfanya kusalia katika ulingo wa siasa za kitaifa hata baada ya kustaafu Agosti 9, mwaka huu.

Naye Bw Nelson Nzuya ataendelea kushikilia wadhifa wa mwenyekiti wa kitaifa wa Jubilee huku naibu wake akiendelea kuwa Bw David Murathe.

Kwa upande wake, Bw Raphael Tuju alijizulu wadhifa wa Katibu Mkuu na cheo hicho kikapewa Mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni.

Mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny ataendelea kushikilia wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu, cheo alichotunukiwa mwaka 2021 baada ya kutimuliwa kwa Mbunge wa Soy, Caleb Kositany.

Mbunge wa Kieni Kanini Kega naye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Jubilee huku mwenzake wa Eldas Aden Keynan akisalia kuwa Katibu wa Kundi la Wabunge wa Jubilee

Rais Kenyatta jana alisema kwamba, atampigia debe Bw Odinga kupitia muungano mkubwa wa Azimio la Umoja hadi amrithi ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Alimsifu Bw Odinga kwa kukubali handisheki iliyoleta utulivu nchini baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 huku akifichua kuwa, waziri mkuu huyo wa zamani pia alimsaidia kutuliza mgogoro uliokuwa umekumba chama tawala cha Jubilee.

Ili kuondoa shaka kwamba ameamua chaguo la mrithi wake ni Bw Odinga, Rais Kenyatta alihudhuria kongamano la kitaifa la wajumbe wa chama cha ODM katika uwanja wa michezo wa Kasarani, muda mfupi baada ya Bw Odinga kuhudhuria kongamano sawa la Jubilee katika Kenyatta International Conference Center, Nairobi.

“Mimi ni Jubilee lakini mnaona nimevaa kofia ya Azimio. Kuanzia leo kwa fikira zangu, kwa damu na roho, tunasema ni Azimio. Twende kazi tuhubiri amani na umoja,” Rais Kenyatta alisema.

Alimtaja Bw Odinga kama kiongozi muungwana aliyemsaidia katika masuala mengi ya utawala bila kuwa na tamaa ya kuingia serikalini.

“Nyumba yako ikiwa inachomeka na ndugu yako awe anaketi kitako akitazama uteketee kisha jirani aje na maji kukusaidia kuuzima, ni nani anayekufaa? Hawa wazee (Bw Odinga na viongozi wengine wa vyama vya kisiasa vilivyounga handisheki) ndio walinisaidia kuzima moto na tukaweza kutekeleza mengi katika muhula wa pili wa utawala wangu,” alisema Rais Kenyatta.

Alimtaja Bw Odinga kama kiongozi asiye na tamaa anayependa na kujali nchi yake.

“Wengine wanasema eti handisheki ilikuwa ya kuingiza Odinga serikalini. Mimi nataka anayejua mmoja anayejua kitu Raila aliitisha kwangu anionyeshe. Raila hakuwa na masharti ila kutaka amani nchi isonge mbele,” alisema.

Alifichua kuwa yeye na Bw Odinga wamekuwa wakishauriana kuhusu yanayostahili kupeleka nchi mbele.

“Wengi hawaelewi maana ya amani. Wanafiriki amani inachimbwa kwa shamba au kununuliwa sokoni. Lakini amani ni kitu kigumu. Kinahitaji mtu shujaa, anayeweza kusimama na kutetea amani hata kama wale walio karibu na wewe wanakuhimiza usimame kidete watu wakiuana. Handisheki yangu na baba haikuwa rahisi,” Rais Kenyatta alisema.

“Raila alikuwa na ujasiri, alikuwa na upendo mkubwa kwa nchi. Yale ambayo tumefanya nikiwa na huyu mzee wangu hii miaka minne imezidi ile tulikuwa tumefanya hapo mbele,” alisema.

Alisema Raila alimsaidia kufanikisha mengi ikiwemo kuagiza wabunge wa chama chake kumsaidia kupitisha miswada muhimu bungeni huku washirika wake waliokataa handisheki wakipinga

Alimtetea Bw Odinga dhidi ya madai kwamba, anapenda kuzua ghasia wakati wa uchaguzi akisema kama angekuwa mtu wa vita, hangeungana na Rais Mwai Kibaki baada ya ghasia za uchaguzi mkuu za 2008.