IEBC motoni kwa dai inaendesha ‘usajili haramu’
NA PHILIP MUYANGA
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), imeshtakiwa kwa madai ya kuendeleza usajili na uhamishaji wa wapigakura nje ya afisi zao.
Mlalamishi, Bw George Mutuku, ameambia mahakama kwamba IEBC ilikuwa imetangaza kukamilisha usajili uliolenga wapigakura wengi Februari 6, na ikaongeza kwamba usajili ambao umesalia utakuwa ukiendeshwa tu katika afisi zake na vituo vya Huduma Centre.
Kulingana naye, tume hiyo inayosimamiwa na Bw Wafula Chebukati, imeenda kinyume kwa kufanya uhamisho wa wapigakura katika kijiji cha Lang’ata kilicho Kaunti ya Taita Taveta, kinachopakana na Kaunti ya Kajiado.
Kesi hiyo imewasilishwa wakati ambapo maswali yameibuka miongoni mwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu kwa nini usajili bado unaonekana ukiendelezwa nje ikiwemo katika afisi za wanasiasa na maeneo ya kijamii.
Kwenye kesi aliyowasilisha katika Mahakama Kuu ya Mombasa, Bw Mutuku amesema usajili unaoendelezwa ni haramu.Jaji John Mativo ameamua kuwa kesi hiyo ni ya dharura na akaagiza itajwe Machi 10, ili mwelekeo utolewe.
Mlalamishi huyo amedai kuwa, maafisa wa IEBC wanafanya usajili katika boma la afisa ambaye ni mfanyakazi wa afisi ya mbunge wa Taveta, wakisimamiwa na polisi na chifu wa eneo hilo.
Mbali na IEBC, Bw Mutuku ameshtaki pia mratibu wa uchaguzi katika eneobunge la Taveta, mkuu wa polisi wa Taveta, na Naibu Kamishna wa Kaunti anayesimamia eneo la Taveta.
Amezidi kudai kuwa, mratibu wa IEBC anayesimamia eneobunge hilo kwa ushirikiano na maafisa wa Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF), polisi na machifu wamehamisha kisiri mitambo ya kusajili wapigakura hadi mahali hapo ambapo, kulingana naye, wapigakura wanahamishwa.
Kulingana naye, maafisa wanaosimamia shughuli hiyo wamefunga mlango wa afisi za eneobunge ili kuendeleza usajili kwa njia haramu.
Ameambia mahakama kuwa wananchi wanaotaka kujisajili katika afisi za IEBC zilizo eneobunge hilo wamekosa namna kwa vile mitambo ya usajili haiko afisini.
“Shughuli nzima ya usajili katika eneo ambalo halitambuliki rasmi kisheria, ni ukiukaji wa sheria kwa vile watu wa asili moja wanaotambuliwa na maafisa wa NG-CDF pekee ndio wanaokubaliwa kujisajili,” hati aliyowasilisha mahakamani inaeleza.
Bw Mutuku amedai kuwa, watu wanaokubaliwa kuhamisha vituo vyao vya kupiga kura katika kijiji cha Lang’ata waliambiwa wawasilishe majina yao na vitambulisho kwa mtu fulani, ndipo wakaambiwa mahali ambapo wangeenda kusajiliwa.
“Mlalamishi anafahamu kuwa baada ya usajili huo, wapigakura wanaohamishwa hulipwa Sh500 kila mmoja. Kuna pia chakula ambacho huwa wanapewa wakati wa usajili na chakula hicho kimefadhiliwa na afisi ya mbunge,” hati ya kesi ikadai.
Bw Mutuku anataka mahakama iagize mratibu wa uchaguzi katika eneobunge hilo awasilishe barua ya kuonyesha kuwa IEBC iliidhinisha usajili nje ya sehemu zilizotangazwa rasmi.
Next article
Mahangaiko ya Wakenya walio nchini Ukraine