Kingi sasa ajitolea kuzima Ruto Pwani
MAUREEN ONGALA NA VALENTINE OBARA
GAVANA wa Kaunti ya Kilifi, Bw Amason Kingi, ameanzisha kampeni kali za kuzima majaribio ya Naibu Rais, Dkt William Ruto, kujizolea umaarufu Pwani kuelekea uchaguzi ujao.
Kupitia kwa chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA), gavana huyo anampigia debe Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kwa urais chini ya Muungano wa Azimio la Umoja.
Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa PAA mashinani uliofanywa Kaunti Ndogo ya Rabai, Bw Kingi, alisema uamuzi wa Dkt Ruto kupinga katiba iliyoleta mfumo wa ugatuzi mwaka wa 2010, ni mojawapo ya sababu kuu ambazo zinamfanya asiwe kiongozi anayefaa kuungwa mkono na Wapwani.
“Wakati Raila alikuwa anatoa wito wa marekebisho ya katiba, naibu rais alizunguka kote nchini akisema kuwa hatuhitaji katiba mpya bali tuendelee kutumia ile ya zamani,” akasema.
Mfumo wa ugatuzi ulikumbatiwa na idadi kubwa ya viongozi na wenyeji wa Pwani kwa vile ulikaribiana na mfumo wa ‘majimbo’ ambao ulikuwa ukipiganiwa eneo hilo kwa miaka mingi tangu zamani.
Hii ni kutokana na kuwa, mfumo huo uliaminika ungetatua changamoto kuhusu jinsi ukanda huo ulivyokuwa miongoni mwa maeneo ambayo yalitengwa kimaendeleo kwa muda mrefu.Wiki iliyopita, PAA iliweka makubaliano na Chama cha Jubilee kujiunga na Azimio la Umoja.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya majaribio ya kuungana na ODM kugonga mwamba. Viongozi wa ODM walihofia Bw Kingi angetumia umaarufu wa Bw Odinga kuvumisha PAA na hivyo basi kuhatarisha uwezo wa ODM kuzoa viti vingine vya kisiasa uchaguzini.
Jana, ilibainika kuwa maafisa wakuu wa ODM walifahamu kuhusu juhudi za kuvuruga majaribio yoyote ya Bw Kingi kuungana na chama hicho kupitia kwa PAA.
Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna, alisema hakuna vile wangekubalia chama ambacho kiliundwa na waasi wake kirudi kutaka kuungana nao kwa hivyo ni vyema kama chama hicho kilipata njia nyingine ya kuingia Azimio la Umoja kupitia kwa Jubilee.
“Hicho ni chama kilichoanzishwa na gavana ambaye alishinda vipindi viwili vya uongozi kupitia kwa ODM. Ingelikuwa mzaha kwetu kutia sahihi ya kushirikiana na kikundi kilichotuasi,” akasema katika mahojiano kwa runinga.
Licha ya hayo, msimamo wa PAA unatarajiwa kupiga jeki kampeni za Bw Odinga Pwani dhidi ya Dkt Ruto ambaye ni mshindani wake wa karibu.
Wakati alipotangaza uamuzi wa kushirikiana na Jubilee, Bw Kingi alisisitiza amefanya hivyo kwa sharti kuwa Bw Odinga ndiye atapeperusha bendera ya Azimio la Umoja katika uchaguzi ujao wa urais.
Katika mkutano wake na viongozi wa mashinani, alisema walikutana ili kutoa mwelekeo kuhusu kampeni zao kuelekea kwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.
“Tunataka kujiongeza nguvu kwa kuchagua madiwani wengi, wabunge na seneta ili tupate uwezo na nguvu za kuzungumza ndani ya serikali ya Raila. Kumpigia debe ili awe rais si mtihani, bali suala ni kuhusu jinsi tutakayvonufaika kutokana na serikali yake,” akasema.
Alisisitiza kuwa uamuzi wa kuunda PAA ni kwa manufaa ya Wapwani, huku akikosoa wanasiasa ambao wamekatalia vyama vilivyo na mizizi yao nje ya Pwani.
Kulingana naye, ukanda huo utaendelea kupewa ahadi hewa na matatizo hayatatatuliwa ikiwa hakutakuwa na chombo cha kuwapa sauti katika meza ya siasa za kitaifa.