Hatua ya Raila kusaliti washirika yahujumu juhudi zake za kuingia Ikulu
NA BENSON MATHEKA
Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, amejipata katika hali ngumu kutafuta washirika wa kuungana naye kwenye uchaguzi mkuu ujao kufuatia malalamishi kwamba, amekuwa akitupa kapuni makubaliano ya miungano ya kisiasa.
Kinachomfanya kuogopwa na vigogo wa kisiasa nchini uchaguzi mkuu wa Agosti 9 unapokaribia, ni malalamishi ya vinara wenza katika uliokuwa muungano wa NASA, aliotumia kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017.
Mnamo 2020, waliokuwa vinara wenza katika NASA, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC) na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya walijitenga naye wakimlaumu kwa kukiuka mkataba wa muungano huo.
Malalamishi yao ni kuwa, Bw Odinga hangegombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kwamba, chama chake cha ODM kilikataa kugawia vyama tanzu vya NASA pesa kutoka kwa Hazina ya Vyama vya Kisiasa.
Watatu hao waliungana na mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi kubuni muungano wa One Kenya Alliance (OKA) na mwezi Januari
23, Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula walijitenga na OKA na kuungana na Naibu Rais William Ruto, mpinzani mkuu wa Bw Odinga, wakimlaumu Rais Kenyatta kwa kuwasukuma wamuunge kiongozi huyo wa ODM.
Kulingana na Bw Mudavadi, Bw Odinga hawezi kuaminika kwa kuwa alikiuka mkataba wa NASA na kuwaacha nje kwenye handisheki yake na Rais Kenyatta.
“Hatuwezi kushirikiana na viongozi wasioweza kuaminika, wale unaojiweka kwenye hatari ukiamua kuwaamini. Kwa kuondoa shaka, Azimio la Umoja sio chaguo letu,” Bw Mudavadi aliambia mkutano wa wajumbe wa chama chake Januari 23.
Jana, Bw Musyoka aliweka wazi mkataba ambao Bw Odinga aliahidi kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Kulingana na mkataba huo, Bw Odinga angeunga azima ya urais ya Bw Musyoka hata kama hawangeshinda uchaguzi mkuu wa 2017.
“Bw Odinga anaweza kuchagua kutimiza makubaliano haya au kukaidi kabisa,” alisema Bw Musyoka Kulingana na Bw Musyoka, mkataba huo ni tofauti na ule wa NASA ambao Odinga amelaumiwa kukiuka.
Malalamishi haya yamemwandama Bw Odinga wakati huu anaposuka muungano wa Azimio la Umoja huku Bw Musyoka akisema waziri mkuu huyo wa zamani alisaliti mkataba wao.
Katika muungano huo mpya, Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wamekuwa wakijaribu kuleta pamoja vyama vya kisiasa lakini hakuna kinachokubali kushirikiana na ODM.
Vyama zaidi ya 13 vilivyokubali kuwa chini ya Azimio la Umoja vinafanya hivyo kupitia Jubilee, kinachoongozwa na Rais Kenyatta. Baadhi ya vyama hivyo ni Democratic Alliance Party (DAP-K), Party of National Unity(PNU), Narc, Upia, Pan African Alliance ( PAA), Maendeleo Chap Chap, Kenya Union Party (KUP).
Gavana wa Kilifi Amason Kingi anayeon – goza PAA, amekuwa mshirika wa karibu wa Bw Odinga lakini hata yeye alitumia Jubilee cha Rais Kenyatta kuingia Azimio la Umoja.
Bw Musyoka anasema yuko tayari kujiunga na Azimio la Umoja kupitia mazungumzo ya uwazi chini ya unahodha wa Rais Uhuru Kenyatta ili kuepuka kurukwa na Bw Odinga.
“Tuko tayari kuungana na Azimio ili kuunganisha nchi. Ninataka kuweka wazi kwamba, tunazungumza na Rais Kenyatta,” alisema Februari 24 mwaka huu siku moja kabla ya kuhudhuria kongamano la kitaifa la wajumbe wa chama cha Jubilee na kususia lile la chama cha ODM lililofanyika siku hiyo.
Next article
Linturi aishtaki Serikali kufuatia kukamatwa kwake