Tutaingia Azimio iwapo Raila atakubali Kalonzo apeperushe bendera ya urais, Mutula Jr asema
Na CHARLES WASONGA
SENETA wa Makueni Mutula Kilonzo Junior amesema kuwa kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka atakubali tu kujiunga na Azimio la Umoja ikiwa Raila Odinga atakubali kuunga mkono azma yake ya urais.
Akiongea katika kipindi cha Day Break saa za asubuhi Bw Kilonzo Junior ambaye ni kiranja wa wachache katika Seneti alisisitiza kuwa msimamo huo hauwezi kubadilisha kwani ndio wawili hao walikubaliana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017.
“Raila Odinga alikubali kumuunga Kalonzo Musyoka mkono kwa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2022. Hatutakubali makubaliano hayo yakiukwe. Msimamo wetu ni kwamba tutaungana na Azimio la Umoja ikiwa Raila atakubali kumuunga mkono Kalonzo katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9,” Kilonzo Junior akasema.
“Ikiwa hawatakubali, basi kila mtu aende kivyake,” akaongeza.
Bw Mutula Junior alimsuta Bw Odinga kwa kuweka kando makubaliano kati yake na Kalonzo na sasa anataka kiongozi huyo wa Wiper amuunge mkono kwa urais, bila kuelezea sababu alikiuka makubaliano kati kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017.
“Tumesisitiza kuwa hatuwezi kuweka kando mambo ambayo hayajatimizwa kati ya Wiper na ODM. Kwa sababu masuala hayo hayajasuluhishwa, hatuoni sababu ya kumuunga mkono Raila Amolo Odinga kwa mara ya tatu,” Seneta huyo wa Makueni akakariri.
Mutula Junior vile vile, alimkashifu Bw Odinga kwa kujaribu kusaka kura za Wakenya “kupitia mlango wa nyuma” kwa kuwavutia upande wake magavana Charity Ngilu (Kitui), Kivutha Kibwana (Makueni) na Dkt Alfred Mutua wa Machakos.
“Hatuwezi kumuunga mkono Raila kwa mara nyingi hata kama ameamua kutumia njia za mkato kuingia Ukambani magavana wetu watatu. Ningependa kumhakikishia kwamba hilo halitafanyika,” Kilonzo Junior akasema.
Akijibu madai hayo ya Seneta wa Makueni, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alishauri Wiper kufanyakazi na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga bila kuweka masharti mengi ikiwa kweli chama hicho kinakubaliana na maono ya Azimio la Umoja.
“Ninyi mumetoa taswira kwamba sisi (ODM) tunatamani sana uungwaji mkono kutoka kwenu (Wiper). Hiyo sio kweli. Ushirikiano wa kisiasa utategemea hiari yenu na uhuru wa kutangamana.
“Hakuna mtu anaweza kukulazimisha kujiunga na muungano fulani kinyume na matakwa yako. Ikiwa mnakubaliana na maoni ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, mko huru kujiunga bila masharti ili tufanye mazungumzo,” Bw Sifuna, ambaye pia alihudhuria kipindi hicho cha mjadala kuhusu masuala ya siasa, akasema.
Kulingana na takwimu kutoka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), eneo la Ukambani (kaunti za Makueni, Machakos, na Kitui) ambako Bw Musyoka ana ufuasi mkubwa, lina jumla ya kura 1.7 milioni.
Katika uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Kalonzo alimwezesha Bw Odinga kupata karibu kura milioni moja.
Next article
Narc Kenya yaomba muda zaidi kabla ya kutia saini…