Connect with us

General News

Maafisa walioghushi zabuni ya IEBC wapigwa faini ya Sh12 milioni – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Maafisa walioghushi zabuni ya IEBC wapigwa faini ya Sh12 milioni – Taifa Leo

Maafisa walioghushi zabuni ya IEBC wapigwa faini ya Sh12 milioni

Na RICHARD MUNGUTI 

“TUMEPIGANA vita tangu 2013 lakini tumefikia ukingoni na sasa haki itatwaa usukani,” wakili Paul Kamau aliyewatetea washtakiwa walioghushi zabuni ya ununuzi wa taa za kutumika wakati wa uchaguzi mkuu wa 2013.

Licha ya kupigana kufa na kupona  washtakiwa waliopatikana na hatia ya kughushi zabuni ya taa za kumulika wakati wa uchaguzi wa 2013 juhudi zao za kuachiliwa huru ziligonga mwamba na sasa watawasha hizo taa jela wakishindwa kulipa faini ya Sh11.8milioni ama watumikie kifungo cha miaka 16 gerezani.

Ilibidi Bw Kamau anukuu kifungu cha II Timotheo 4:7 kumshawishi  hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Lawrence Mugambi awaonee huruma walaghai hao.

Hata hivyo Bw Mugambi alisema makosa waliyofanya washtakiwa Benson Gethi Wangui, Joyce Makena,Gabriel  Ngonyo Mutunga, Willie Gachanga Kamanga na Kennedy Ochae ni mabaya kwa vile tume huru ya uchaguzi na mipaka ingelipoteza Sh105milioni.

“IEBC ingepoteza Sh105 milioni kama zabuni hiyo haingelisimamishwa na Serikali,” alisema Bw Mugambi.

Hakimu huyo alisema sakata hiyo ilibuniwa na Gethi na Makena ambao ni wakurugenzi wa kampuni ya Solarmak Technologies Limited 2013.

Solarmak iliwasilisha ombi kwa IEBC ipewe tenda ya kununua taa za kutumia nishati ya jua kuangaza wakati wa kuhesabu kura wakati wa uchaguzi mkuu wa 2013.

Solarmak ilieleza IEBC itanunua taa hizo kwa bei ya Sh147milioni.

Lakini kampuni nyingine Konexion Limited iliyoomba zabuni hiyo ilikuwa imeeleza IEBC itanunua taa hizo kwa bei ya Sh107milioni.

Baada ya kupashwa habari  Konexion ilikuwa imetaja bei ya chini , Solarmak iliwatumia maafisa wa IEBC kubadilisha hati zake kuonyesha itazinunua taa hizo kwa bei ya Sh105 milioni.

“Solarmak ndiyo ingelinufaika na ufisadi huo wa kubadilishiwa nakala za hati zake,” alisema Mugambi.

Hakimu huyo alisema ukora huo ulitekelezwa na Gabriel Ngonyo Mutunga na Kennedy Ochae ambao walikuwa maafisa waq IEBC.

Mahakama ilisema Mutunga alifungua maombi ya Solarmak na kumpa Ochae kubadilisha herufi za ununuzi wa taa hizo kusomeka Sh105milioni badala ya Sh147milioni.

“Mutunga ndiye kinara wa ufisadi huo.Alimshirikisha Ochae ambaye alikuwa na siku 21 tangu aajiriwe kama karani na IEBC idara ya ununuzi wa bidhaa,” alisema Mugambi.

Kuhusu Mutunga , Mugambi alisema mshtakiwa huyo atapata adhabu ya juu kuliko wenzake. Alimtoza faini ya Sh2.8milioni ama atumikie kifungo cha miaka mitano.

Kamanga aliye na umri wa miaka 70 na aliyestaafu kutoka utumishi wa umma alitozwa faini ya Sh800,000 ama atumikie kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Kamanga alikuwa na cheo cha Meneja wa Mauzo IEBC uhalifu huo ulipotekelezwa.

Mugambi alimpata Kamanga na hatia ya kutojali na kushindwa kutunza hati za IEBC ikapelekea zabuni zibadilishwe.

Hakimu alitupilia mbali ushahidi wa Makena kwamba hakujua kwamba ni mmoja wa wakurugenzi wa Solarmak. Alidai baba yake ndiye alikuwa akiendesha kampuni hiyo.

“Makena na Gethi walibuni uwongo kwamba hawakujua ni wakurugenzi wa Solarmak.Uwongo wao haufui dafu,”alisema Mugambi.

Lakini Makena alijitetea kwamba “yuko na mtotot mwenye umri wa miaka mitatu na kwamba ataumia endapo atahukumiwa kifungo cha jela.”

Akipitisha hukumu hakimu alisema sheria imesema wanawake wanaonyonyesha wasihukumiwe vifungo vya jela ili kuwatunza watoto wao.

Hakimu alisema kwa vile washtakiwa walikuwa wakosaji wa mara ya kwanza korti itawatoza faini pamoja na kupitisha kifungo cha jela wakishindwa kulipa faini hiyo.

Mahabusu hao watano hawakulipa faini walizotozwa mara moja. Walipelekwa rumande hadi Jumatano kuwezesha watu wa familia zao kulipa faini hizo.