Connect with us

General News

Kwale yalegea kujenga madarasa – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kwale yalegea kujenga madarasa – Taifa Leo

CBC: Kwale yalegea kujenga madarasa

SIAGO CECE NA WINNIE ATIENO

KAUNTI ya Kwale ni miongoni mwa zile ambazo bado ziko nyuma kukamilisha ujenzi wa madarasa mapya ya kufanikisha mfumo wa elimu wa CBC, kwa mujibu wa Wizara ya Elimu.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, amemtaka mkurugenzi wa elimu kutafuta wanakandarasi mbadala ikiwa waliopewa kazi wameshindwa kukamilisha.

Kulingana naye, ni asilimia 65 pekee ya madarasa imekamilika katika kaunti hiyo.

“Mpango wetu ni kuwa baada ya mitihani kukamilika, tutaanza awamu ya pili ya ujenzi wa madarasa. Mkandarasi atakayekosa kumaliza awamu ya kwanza hatakubaliwa kufanya ujenzi katika awamu hii nyingine,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika Kaunti ya Kwale alipokuwa akifungua darasa jipya katika shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Prof Magoha alisema kuwa kitaifa, ujenzi wa madarasa ya kufanikisha CBC umekamilika kwa asilimia 80.

“Tulikuwa na lengo ambalo lilitolewa na Rais Uhuru Kenyatta la madarasa 10,000 ambayo yalipaswa kukamilishwa kufikia mwisho wa mwaka huu. Tuligawanya hayo kuwa

awamu mbili kuanzia na 6,740 na hivi tunavyozungumza zaidi ya madarasa 3,000 yamekamilika,” alisema.

Aliongeza kuwa mengine 2,000 bado yanawekewa paa na yatakamilika ndani ya wiki moja.

Serikali haikufanikiwa kutekeleza mpango wake wa kukamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya madarasa hayo kabla ya mitihani ya Kitaifa ya KCPE na KCSE.

Kulingana na Prof Magoha, kaunti nne pekee kati ya 47 zimekamilisha ujenzi wa madarasa hayo. Kaunti hizo ni Meru, Garissa, Wajir na Madera.

Katika eneo la Nyanza, madarasa yamekamilika kwa asilimia 90, huku maeneo yaliyosalia yakitarajiwa kukamilika wiki ijayo.

“Kaunti zote za Nyanza ziko katika asilimia 90 na ndani ya wiki moja zote zitakuwa zimekamilika. Hii inamaanisha kuwa eneo la Nyanza linafanya vyema sana. Pia Kaunti ya Kitui ambayo ilikuwa na lengo la kujenga madarasa 300 iko karibu kukamilisha,” alisema.

Wakati huo huo, waziri huyo amewataka watahiniwa wanaoanza mitihani yao ya kitaifa wasishawishike kufanya udanganyifu, kwani mitihani iliyowekwa ni ‘rahisi’.

Alisema mitihani hiyo ilizingatia kuwa shule zilifungwa kwa muda mrefu kwa sababu ya janga la corona.

“Tumezingatia changamoto zote walizopitia ambazo zilikuwa za nje na ngumu. Hakuna aliyeleta Covid-19. Watupe tu walichonacho vichwani mwao na hiyo inatutosha,” Prof Magoha alisema.

Ili kukabiliana na wizi wa mitihani, Prof Magoha alisema wizara yake itapunguza masaa ya kufungua kontena ya mitihani kutoka saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili unusu asubuhi.

Prof Magoha aliwaonya wasimamizi wa mitihani kutothubutu kuiba mitihani mwaka huu.

“Kuna wakora wanapanga kuiba mitihani wakati wa ufunguzi wa kontena za mitihani. Tunataka watu wanaosimamia mitihani kutosongamana

kando na pia kupunguza masaa ya kufungua kontena asbuhi. Majangili washaanza kuuza mitihani mtandao wa telegram, lakini ni ghushi, msipoteze pesa zenu wazazi jamani,” alisema Prof Magoha.

Alisema inasikitisha kwamba kuna watu wanajizatiti kudanganya watahiniwa kwamba wana mitihani ya kitaifa, akaonya wazazi na wanafunzi wasipumbazwe na matapeli wanaouza karatasi feki za mitihani.

Wiki ijayo, wadau wakuu wa sekta hiyo watakutana ili kujadili masuala ya maandalizi ya KCPE.

Prof Magoha alisema vyombo vya usalama vitakabiliana vikali na mtu yeyote ambaye atapatikana akijaribu kuleta udanganyifu katika mitihani.