Serikali yatangaza mlipuko wa homa ya manjano, watu 15 wafariki
NA WANGU KANURI
SERIKALI imetangaza mlipuko wa ugonjwa wa homa ya manjano nchini huku ikisema tayari watu 15 wamefariki kutokana na maradhi hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu, Patrick Amoth jana alisema vifo vimerekodiwa katika Kaunti za Wajir, Garissa, Marsabit, Meru, Samburu, Baringo, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi, Tana River, Mandera na Turkana.
“Homa ya manjano husambazwa na mbu aina ya Aedes na Haemogogus. Mbu hao huzaana nyumbani, kichakani au kwenye mazingira yote mawili,” akasema Dkt Amoth.
Mwathiriwa hufahamu anaugua homa hiyo akiwa na dalili za joto jingi mwilini, kuumwa na mishipa, mgongo, kichwa, kukosa hamu ya kula na anatapika au kuhisi kichefuchefu. Hata hivyo, dalili hizi hutoweka baada ya siku tatu au nne.
Chini ya saa 24 baada ya kupona, asilimia ndogo ya wagonjwa hulemewa tena na homa hiyo huku ini na fi – go zikidhurika. Takwimu za wizara zinaonyesha nusu ya watu ambao huonyesha dalili sugu za homa ya manjano hufariki kati ya siku 7 na 10.
Licha ya kutokuwa na dawa ya kupambana na virusi vya homa hiyo, wizara hiyo inaeleza kuwa kupokea matibabu ya mapema kunasaidia kuongeza muda wa kuishi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiria kuwa ifikapo 2026, watu bil – ioni 1 watakuwa wamelindwa kutokana na homa ya manjano kupitia chanjo. Dkt Amoth alishauri kuwa pindi tu mtu akipata virusi hivyo anafaa kupumzika, kunywa maji kwa wingi na kumeza dawa za kupunguza maumivu pamoja na joto mwilini.
Kulingana na Dkt Amoth, watu watatu walifariki huku wengine zaidi ya 20 wakipata virusi vya homa hiyo katika maeneo bunge ya Imerti na Garbatulla, Isiolo mwezi jana.
Waziri wa Afya Kaunti ya Isiolo, Wario Galma jana alisema chanjo zilizo katika kaunti hazitoshi.
“Kenya imekuwa ikichanja tu wanaosafiri ndiposa hakuna chanjo za ku – tosha lakini sababu ya mlipuko unaoshuhudiwa, chanjo nyingi zitanunuliwa,” akaeleza.
Hata hivyo Bw Wario alisema kuwa ni mtu mmoja pekee aliyefariki kutokana na homa hiyo.