Connect with us

General News

Ni KCPE kwa hofu vijiji vikichomwa kaunti ya Baringo – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Ni KCPE kwa hofu vijiji vikichomwa kaunti ya Baringo – Taifa Leo

Ni KCPE kwa hofu vijiji vikichomwa kaunti ya Baringo

NA WANDISHI WETU

WATAHINIWA katika baadhi ya shule Kaunti ya Baringo, Jumatatu walifanya mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) kwa hofu kutokana na uvamizi ambao umekuwa ukitekelezwa na majangili katika eneo hilo.

Hali ya taharuki ilitanda katika shule ya msingi ya Karne, Kaunti ya Baringo, baada ya majangili kuvamia kijiji cha Kapkosom, Jumatatu asubuhi na kuteketeza nyumba.

Kijiji cha Kapkosom kiko tu umbali wa kilomita mbili kutoka shule ya Karne.

Watahiniwa kutoka shule za msingi za Kapkechir na Koitilil wanafanyia mtihani wao katika shule ya Karne baada ya kuhamishwa maeneo yao kutokana na kudorora kwa usalama.

Jana Jumatatu, baadhi ya wakazi wa Kapkosom walitoroka makazi yao na kutafuta hifadhi katika maeneo mengine.

Watahiniwa wa shule ya msingi ya Sinoni, Kaunti ya Baringo, wanafanyia mtihani wa KCPE katika shule ya Mochongoi baada ya kuhamishiwa hapo kutokana na uvamizi uliotekelezwa Machi 7, 2022.

Katika Kaunti ya Kwale, Kamanda wa Polisi Bw Ambrose-Steve Oloo, ametishia kuwaadhibu maafisa wa usalama wanaosimamia mtihani watakaopatikana wakilewa.

Bw Oloo alikuwa akizungumza wakati wa kufungua kontena ya mtihani katika Kaunti ya Kwale. Mkuu huyo wa polisi pia alionya maafisa hao kutowapa wanafunzi bunduki kupiga picha nazo.

Takriban watahiniwa 23,375 watafanya mtihani huo katika vituo 464 katika Kaunti ya Kwale.

Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Kwale Martin Cheruyiot alisema kuwa mitihani hiyo inatarajiwa kukamilika Jumatano, na matokeo yatatangazwa katika muda wa wiki tatu zijazo.

Katika Kaunti ya Lamu, usalama umeimarishwa katika mpaka wa Kenya na Somali wakati huu ambapo watahiniwa wanafanya mtihani wa KCPE.

Jumla ya wanafunzi 3,661, wavulana 1,845 na wasichana 1,816 wanafanya mtihani huo katika vituo 62 katika Kaunti ya Lamu.

Kamishna wa Lamu Irungu Macharia aliwahakikishia watahiniwa, wazazi, walimu na wasimamizi wa mitihani kuwa kuna usalama wa kutosha.

Bw Macharia alisema kila kituo cha mtihani wa KCPE kimepewa angalau polisi wawili ilhali doria zimeimarishwa vilivyo kipindi chote cha mtihani.

Januari mwaka huu, vijiji vya Widho, Juhudi, Salama, Mashogoni, Ukumbi, Kibokoni, Milihoi na Bobo-Sunkia vilishuhudia mashambulio ya Al-Shabaab yaliyoangamiza watu 15, nyumba kuchomwa na wakazi kutorokea usalama wao kwenye kambi za wakimbizi.

Kamishna wa Kaunti ya Kilifi Kutswa Olaka naye alisema kuwa maafisa wa usalama wa Gereza la Shimo la Tewa na Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) wamehusishwa katika ulinzi wa mtihani.

Jumla ya watahiniwa 39,079 wanafanya KCPE katika vituo 503.

Katika Kaunti ya Kisii, mwanafunzi mmoja alifanyia mtihani wake katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii baada ya kujifungua mtoto wa kiume, kwa mujibu wa Katibu wa Wizara ya Elimu, Dkt Julius Jwan.

Habari zimekusanywa na Florah Koech, Siago Cece, Kalume Kazungu na Maureen Ongala

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending