Hatua ya Urusi yaibua kilio kote bei zikipanda
NA MASHIRIKA
MOSCOW, URUSI
ATHARI za vita nchini Ukraine zinaendelea kushuhudiwa kote duniani huku bei ya petroli na bidhaa nyinginezo ikipanda.
Bei ya mafuta ilipanda kwa kiasi kikubwa nchini Amerika mara baada ya Rais Joe Biden kupiga marufuku mafuta na gesi kutoka Urusi.
Bei ya mafuta nchini humo iliongezeka kwa asilimia 3.6 – ambayo ndiyo bei ya juu zaidi tangu 2008.
Rais Biden alipiga marufuku mafuta, gesi na makaa ya mawe kutoka Urusi kuingizwa nchini humo. Alisema hatua hiyo ilichukuliwa kuadhibu Urusi ambayo imevamia Ukraine.
Umoja wa Ulaya (EU), hata hivyo, ulikwepa kupiga marufuku mafuta kutoka Urusi kutokana na hofu ya kuathiri uchumi wake. Badala yake EU ilisema kuwa itaanza kupunguza mafuta kutoka Urusi kuanzia Disemba, mwaka huu.
Urusi husafirisha kiasi kikubwa cha mafuta kote duniani.
Bei ya vyuma pia imepanda duniani kufuatia mapigano nchini Ukraine. Urusi na Ukraine huchangia zaidi ya asilimia 20 ya vyuma vinavyouzwa duniani.
Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) , linasema kuwa bei ya vyakula kote duniani imepanda kwa asilimia 3.9.
Bei ya dhahabu katika soko la Uturuki imeongezeka maradufu kufuatia mzozo wa kivita nchini Ukraine.
Gramu moja ya dhahabu sasa inauzwa kwa Sh6,400 – bei ambayo ni ya juu zaidi tangu 2020.
Bei ya mafuta ya kupikia pia imepanda kote duniani. Urusi na Ukraine zinachangia kwa asilimia 50 uzalishaji wa mafuta ya alizeti (sunflower) kote duniani.
Nchini Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka raia wa nchi hiyo kujiandaa kwa bei ya juu ya bidhaa.
“Vita nchini Ukraine vimesababisha kupanda kwa bei za mafuta. Bidhaa zote zitapanda bei, nauli zote zitapanda, kila kitu kitapanda bei,” akasema Rais Samia.
Alisema kuwa viongozi hawana uwezo wa kudhibiti kupanda kwa bei hizo za bidhaa na hivyo Watanzania hawafai kulaumu serikali.
Hayo yanajiri huku Idara ya Ujasusi nchini Amerika (CIA), ikisema kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin anapanga kuteka mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, ndani ya siku mbili zijazo.
Mkuu wa CIA William Burns aliambia kamati ya bunge la Amerika kuwa majeshi ya Urusi yanajiandaa kwa mapigano makali kwa lengo la kuteka nyara Kyiv.
Kiongozi wa China, Xi Jinping, jana aliitaka Urusi kusitisha vita na badala yake ifanye mazungumzo na Ukraine.
Xi alisema hayo kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na kiongozi wa Ujerumani Olaf Scholz.
Makao makuu ya jeshi la Amerika, Pentagon, yanakadiria kuwa karibu watu 4,000 wameuawa katika mapigano hayo nchini Ukraine.
Next article
Marjan ateuliwa kuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC