MAKALA MAALUM: Wanawake wana fursa ya kutoa michango yao katika jamii
NA JURGEN NAMBEKA
JUMATATU wiki hii ulimwengu ulipoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake duniani, kura ya maoni ya TIFA ilionyesha kuwa asilimia 41 ya Wakenya wanamtaka Naibu wa Rais William Ruto, amteue mwanamke kuwa naibu wake.
Hii ni ishara kuwa, Wakenya ambao kwa muda mrefu hawakuwaamini viongozi wa kike miaka ya awali, sasa wameanza kubadili mtazamo wao.
Mada ya maadhimisho ya mwaka huu ni ‘Usawa wa jinsia leo, kwa kesho endelevu’. Mada hii inaashiria kuwa kila jinsia ikipewa nafasi sawa katika uongozi, nafasi za kazi na fursa nyinginezo, kutakuwa na mazingira mazuri ya maendeleo yasiyo na kikomo.
Siku ya wanawake duniani hutengwa kusheherekea mafanikio ya akina dada na michango katika sekta mbalimbali nchini. Siku hii spesheli pia, hutumika kueneza maudhui ya uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia.
Wiki iliyopita, Shirika la Maendeleo ya Wanawake (MYWO), liliadhimisha miaka 70, tangu kuzinduliwa hapa nchini. Shirika hilo lilianzishwa mnamo 1952, ili liwalee na kuwawezesha wanawake kwa kuanzisha mikakati ya kupigania haki zao na kuwapa nafasi za kung’aa katika jamii.
Kama ishara ya kuwatuza wanawake waliofuzu kwenye sekta tofauti tofauti, Wizara ya Jinsia na Utumishi wa Umma, ilitoa tuzo za waliobobea kuwasheherekea wanawake hao.
Akiwatuza wanawake kwenye tuzo hizo wiki mbili zilizopita, Waziri wa Jinsia, Dkt Margaret Kobia, aliwataja Phoebe Asiyo, Zipporah Kittony, Grace Onyango, na Joan Mjomba, kama wanawake shupavu.
Wanawake hao waliopewa tuzo hiyo, walikuwa wa kwanza hapa nchini kuingia kwenye siasa.
Viongozi hao shupavu, walionyesha mtindo mwafaka kwa akina dada ambao mara nyingi hufa moyo, kwa kutopewa nafasi sawa katika sekta mbali mbali.
Mabi Asiyo, Kittony, Onyango, na Mjomba walifahamu kuwa, siasa za humu nchini zilitawaliwa na wanaume. Kwa wakati huo wanadada wengi waliogopa kujihusisha na siasa. Licha ya hayo, walijitosa ulingoni na kuvunja dhana potovu za kuwa wanawake hawawezi kuongoza.
Kwenye karne ya 21, wanawake kote duniani wametia bidii kuhakikisha kuwa hawajawachwa nyuma kwenye nafasi mbalimbali.
Kina dada kwenye karne hii, wanajituma zaidi, na kuonyesha ubabe wao licha ya mazingira kutoashiria usawa wa asilimia 100.
Muungano wa Wanawake kwenye Vyombo vya Habari (AMWIK), uliandaa mkutano wa siku ya wanawake, na kuwahusisha wanawake katika jamii, pamoja na wale walio kwenye siasa.
Lengo kuu la mkutano huo likiwa, kuzungumzia masuala yanayowahusu akina dada, ambayo ni pamoja na mikakati itakayowawezesha wanawake wengi kuingia uongozini.
Mwaniaji wa kiti cha mwakilishi wa kike kaunti ya Marsabit, Bi Gedhia Mamo, alipinga vikali vikwazo vilivyowekwa na tamaduni za kiafrika kuwazuia wanawake kutwaa nafasi za uongozi.
“Utamaduni wetu umetuzuia sisi kama wanawake kuwa viongozi. Kinachoshangaza ni kuwa, sisi wanawake ndio tuko katikati ya changamoto zinazozikumba jamii zetu, mbona tusipewe nafasi sawa za kuwakilisha watu wetu,” alisema Bi Mamo.
Siku ya wanawake ikiadhimishwa, kuna wasiwasi kwanini miaka 12 baadaye, bado sheria ya kuhakikisha jinsia moja haizidi theluthi mbili katika bunge haijatimia. Mojawapo ya sababu ya idadi ya wanawake kuwa ndogo bungeni ni kwasababu wengi hawajajitolea kuwania viti vya uongozi.
Hadi wa sasa, wanawake wanaojitosa kwenye siasa hupatwa na changamoto nyingi zinazotokana na dhana mbovu ya kuwa hawawezi kuongoza. Licha ya dhana hii kuwepo kichinichini, wanawake kama Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga, Bi Anne Waiguru na Jaji Mkuu Martha Koome, wameonyesha kuwa kila mja ana uwezo wa kung’aa licha ya jinsia yake.
Kulingana na Mwakilishi wa Kike wa Uasin Gishu, Bi Gladys Boss Shollei, wanawake wanapaswa kuvumilia wanapotafuta nafasi za uongozi, kwani bado dhana hii haijafutiliwa mbali kikamilifu.
Anaeleza kuwa wagombeaji wa kike hushambuliwa pindi tu wanapotangaza azma yao ya kuwania viti mbalimbali.
“Kuwa kiongozi haswa ukiwa mwanamke siyo rahisi. Lakini nawashauri leo kuwa, tuwaige wanawake waliotutangulia. Tuwe na msingi mzuri wa kutusaidia kutwaa nafasi hizi na kuendelea na vita hivi,” alisema Bi Shollei, aliyehudhuria hafla hiyo.
Kando na uongozi, dunia inapoadhimisha siku hii kuu, ni muhimu kuangazia suala la unyanyasaji wa kijinsia ambalo limekithiri.
Wanawake wengi wamejipata kwenye mikono hatari ya watumiaji wa mitandao ya kijamii, ambao huwatupia maneno makali kwa kuzungumzia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia ama usawa. Wanadada wengi hutishiwa na cheche za matusi za watu mitandaoni na kutozungumzia changamoto wanazozipitia.
Kwa hivyo, wanawake wanapaswa kutumia vyombo vya habari kuhakikisha unyanyasaji huo dhidi yao, unazungumziwa na wanaopatikana na hatia za unyanyasaji kuachukuliwa hatua.
Ndio wanawake wawe na nafasi ya kunawiri katika sekta mbalimbali humu nchini, ni vyema serikali kuanzisha mipango ya kushughulikia changamoto zinazowahusu akina dada. Pia ni vyema iwapo sera zitaundwa ili zihakikishe changamoto zinazowakumba wanawake zimeshughulikiwa na kuwapa kina dada wakati rahisi, kukwea nyadhfa mbalimbali kazini.
Siku kuu inapoadhimishwa ni muhimu kutambua kuwa kuwawezesha wanawake kuafikia malengo yao, mi mwanzo wa kuikuza jamii kwa ujumla.
Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa AMWIK, Judie Kaberia, hadithi za wanawake waliong’aa kwenye sekta mbalimbali ni tunu muhimu kwa akina dada wanaokua.
“Iwapo tuna mpango wa kushughulikia changamoto zinazowakumba akina dada katika karne hii, ni muhimu kuwashika mkono akina dada wadogo na kuwaonyesha njia. Hii ndio njia pekee ya kuhakikisha tunapata nafasi sawa kwenye sekta mbalimbali,” anaeleza Bi Kaberia.
Nchi inapoadhimisha siku ya wanawake duniani, suala kuu ni iwapo usawa wa kijinsia katika sekta mbalimbali utapatikana. Iwapo sekta zote zitawajumuisha wanawake kwa usawa, kuna uwezekano wa utendakazi kuimarika na manufaa mengi kupatikana.
Next article
Hatua ya Urusi yaibua kilio kote bei zikipanda