NDUNG’U WAINAINA: Uchaguzi Mkuu uandaliwe katika mazingira ya uwazi
NA NDUNG’U WAINAINA
KENYA itaandaa uchaguzi wake wa tatu chini ya Katiba ya 2010 mnamo Agosti 9, 2022.
Uchaguzi wa Agosti 2022 hasa una ushindani mkali ambapo Rais anayestaafu anajitahidi kufanikisha urithishaji wake huku akiungwa mkono na kiongozi wa upinzani anayemezea mate urais.
Aidha, chaguzi hizo zitakuwa na nafasi muhimu ya kuunda mustakabali na mkondo wa taifa katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Rais anayeondoka pamoja na kiongozi wa upinzani wanaonekana kupendelea kuhifadhi hali iliyopo na kuiendeleza bila kuitatiza sana huku Naibu Rais akishinikiza mabadiliko makuu kwenye mifumo iliyopo.
Tayari kuna matumizi ya lugha kali na ya kutisha hadharani kwenye midahalo ya kisiasa katika vyombo vya habari na tasnia za kisiasa ikiwemo kuongezeka kwa migawanyiko inayosababishwa na jinsi vyombo vya habari vinavyoripoti habari.
Kanuni kuu inayosimamia chaguzi zinazofanyika kwa uadilifu ni kwamba, ni sharti zionyeshe uhuru wa watu.
Chaguzi ni sharti ziwe za wazi na jumuishi, zinazozingatia uwajibikaji na ni sharti kuwepo nafasi sawa za kushindana kwenye chaguzi.
Kushiriki kwa wapiga kura kwenye chaguzi ni kipimo muhimu cha mchakato wa uchaguzi.
Idadi ndogo ya usajili wa wapiga kura ikiwemo viwango vya chini vya wapiga kura wanaojitokeza katika siku ya uchaguzi huenda ikaibua maswali miongoni mwa baadhi ya vyama na wagombeaji kuhusu uadilifu wa chaguzi pamoja na njia iliyotumika kupata washindi.
Chaguzi zinazofanyika kwa njia sawa ni sharti zitimize masharti matatu muhimu ambayo ni pamoja na ujumuishaji, uwazi na uwajibikaji. Hii ndiyo njia pekee ya kuvutia imani ya washindani na umma.
Inatambulika duniani kote kwamba, chaguzi zinazofanyika kwa uadilifu ni sharti zishinde changamoto kadhaa.
Kwanza kabisa, ni sharti chaguzi ziwe zenye uwazi na zinazoungwa mkono na idadi kubwa ya umma kisheria. Ni sharti zifanyike katika mazingira yanayokubalika kisheria yanayolinda haki za wapiga kura na wagombea husika.
Pia, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni sharti izingatie kanuni za kitaaluma, ijiepushe na ubaguzi na kuzingatia uadilifu.
Isitoshe, taasisi na michakato ya uchaguzi ni sharti ziruhusu ushindani mwafaka wa vyama mbalimbali na kuthibitisha nguvu ya demokrasia kisiasa.
Ununuzi wa kura, kutoa hongo kwa wagombea ikiwemo matumizi ya magenge ya wahalifu ni sharti uzuiwe na kuadhibiwa vikali.
Mwandishi ni Mkurugenzi, Kituo cha Kimataifa kuhusu Sera na Migogoro