Connect with us

General News

Afisa wa serikali aliye kielelezo bora kwa raia – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Afisa wa serikali aliye kielelezo bora kwa raia – Taifa Leo

James Nandi: Afisa wa serikali aliye kielelezo bora kwa raia

NA MWANGI MUIRURI

HUKU tabia za baadhi ya maafisa wa serikali wakiwemo makamishna na polisi zikiwa ni za kukera kupitia udhalimu na kudai hongo kiholela, Bw James Nandi, 31 ni afisa ambaye ni kinyume cha nembo hiyo.

Bw Nandi ni afisa ambaye amejishindia upendo si haba wa raia kupitia juhudi zake za kuhudumia wananchi akiwa Kamishna Msaidizi wa Kaunti (ACC) na ambapo kwa sasa anahudumia eneo la Ijara, Kaunti ya Garissa.

Tangu ahamishiwe eneo hilo la Ijara miezi minane iliyopita, Bw Nandi anasema kuwa anahamasisha wenyeji kuhusu umuhimu wa kutekeleza usawa wa kijinsia, kutunza mazingira na kuzingatia ushirikiano na vitengo vya kiusalama ili kuimarisha usalama.

Kufuatia huduma zake kwa raia, aliteuliwa mwaka 2021 na gazeti la Business Daily ambalo ni la kampuni ya Nation Media Group kuwa mmoja wa Wakenya 40 walio chini ya umri wa miaka 40 ambao wametambulika kutokana na jitihada zao.

Kamishna Msaidizi Katika Tarafa ya Ijara Bw James Nandi. PICHA | MWANGI MUIRURI

Alipohudumu kama Kamishna msaidizi wa tarafa ya Kahuro, alipambana na watengenezaji wa pombe haramu na ulevi kiholela kiasi kwamba kuna mwanamume mmoja aliyekombolewa kutoka uraibu wa pombe na juhudi za afisa huyu, na hata akaamua kumpa mtoto wake jina ‘Nandi’.

“Niliamua kumpa mtoto wangu wa pili jina la afisa huyu kwa kuwa alinipa sababu ya kuendelea kuishi. Alipoletwa katika tarafa yetu ya Kahuro iliyoko katika Kaunti ya Murang’a, mimi nilikuwa ninatengeneza pombe haramu. Lakini afisa huyu aliniita afisini mwake na akanipa Sh20,000 kama mtaji wa kuzindua aina mbadala ya riziki,” asema Joseph Kamau, 45.

Anasema kwamba alitumia pesa hizo kujinunulia ng’ombe wa maziwa na ambapo alijijenga upya kupitia mauzo ya maziwa na pato akalitumia kuwekeza katika sekta ya ufugaji wa kuku na nguruwe kiasi kwamba ukwasi halali ulianza kumumiminikia.

“Mnano Juni 23, 2021, mke wangu alijifungua mtoto wa kiume na bila kusita, nikampa jina la afisa huyu. Zamani mke wangu alikuwa amenihepa kwa kukwera na biashara yangu haramu na ulevi kiholela lakini baada yangu kushauriwa na kusaidiwa na afisa huyu kujirekebisha kitabia, alirejea nyumbani,” asema.

Safari ya afisa huyu ya kuingia katika huduma kwa raia katika ajira ya serikali ilianza kama mwanga mdogo ambao kwa sasa umekuwa mkubwa na wa kutambulika na wengi.

Wakati wa kuandaa makala haya, Taifa Leo ilimfahamisha Kamishna wa eneo la Kati Bw Wilfred Nyagwanga ili atoe idhini ya kumhoji afisa huyu na akikubali, alisema “huyo ni mmoja wa maafisa wetu ambaye ni mwadilifu na ambaye mienendo yake inatupa nembo njema katika raia kwa kuwa anaingiana vyema nao.”

Akiwa na umri wa miaka 21 akisomea katika Chuo Kikuu cha Moi, Bw Nandi ambaye ni mpenda kusoma majarida tofauti alikumbana na habari ambazo zilimchochea kuhudumia umma kwa njia ya kipekee.

Kwa wakati huo, hakuwa na ufahamu kuwa safari yake ya kuingia katika ajira ya serikali ilikuwa imeanza kujipa mashiko.

“Nilikuwa katika maktaba ya chuo nikichambua majarida mbalimbali na ndipo nilikumbana na kichwa cha habari katika gazeti moja la hapa nchini kikielezea kumhusu mwanadada ambaye alikuwa amejitoa shuleni – ya upili – huko Baringo kufuatia ujauzito. Alikuwa amekaa nje ya elimu kwa miaka minne baada ya kujifungua na alikuwa sasa akielezea kuhusu nia yake ya kurejelea masomo yake,” asema Bw Nandi.

Bw Nandi anaelezea kuwa aliingiwa na huruma si haba kuhusu mahangaiko ya mwanafunzi huyo mzazi na akaamua kushawishi wanafunzi wenzake wazindue mpango wa kumchangia ili ndoto yake ya kurejelea masomo yake itimie.

“Tuliungana pamoja tukiwa wanafunzi kadha na tukafanikiwa kukusanya pesa zilizomwezesha mwanadada huyo kurudi shuleni na pia tukahakikisha kuwa tulimzidishia hela za kugharimia mahitaji ya mtoto wake mchanga,” asema.

Bw Nandi akiwa ni mtoto wa afisa wa polisi mstaafu Bw Elphas na mama mcha Mungu Kasisi Jani Nandi kutoka kijiji cha Bikeke katika Kaunti ya Trans Zoia, alihakikisha kuwa Bi Kosgey alikamilisha masomo yake ya sekondari, akaingia chuo kikuu na akahitimu.

Aliyekuwa Kamishna wa eneo la Rift Valley Bw George Natembeya ambaye ni mwandani wa familia ya Bw Nandi anasema kuwa “huyu ni afisa ambaye anaipa serikali ile nembo ya utu kupitia huduma kwa wanyonge na kuzingatia kuinua maisha ya anaowahudumia.”

Mbali na kisa cha mwanadada yule, Bw Nandi amekuwa akijihusisha na miradi mingine ya kuyatunza mazingira, afya na usalama hata kabla ya kujiunga na serikali, na alipoingia serikalini, akaimarisha juhudi zake.

Mwaka wa 2013, aliwaleta pamoja baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi kuunda vuguvugu la amani nchini na ambapo alilipanua kujumuisha wanafunzi wa vyuo vingine nchini.

Anasema kuwa alizingatia amani baada ya kushuhudia mahangaiko kwa watoto, walemavu, kina mama na wazee wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

“Vita huua amani ambayo huweka binadamu pamoja wakishiriki harakati za ujenzi wa maisha yao na taifa lao. Nilijituma kuhakikisha kuwa bidii zangu zingechangia amani hata ingekuwa ni kwa boma moja tu…” asema.

Anakumbuka kwamba kwa wakati mmoja akiwa na washirika katika vuguvugu lake la amani walitembea kwa umbali wa kilomita 170 wakipitia Eldoret, Kapsabet, Chavakali hadi Kakamega wakirai wananchi kupitia vipaza sauti wazingatie amani katika uchaguzi mkuu wa 2013.

Mwaka wa 2014 ukiingia, anasema kuwa alikuwa amesajili wafuasi katika vuguvugu hilo kutoka taasisi 30 za elimu ya juu hapa nchini.

Bw Nandi ambaye ni wa tatu katika familia yao anasema kuwa juhudi hizo zilimwezesha kupata ajira ya serikali mwaka wa 2015.

“Nilipewa kazi ya kuwa Kamishna Msaidizi katika Kaunti ya Nyeri eneo la Kieni Mashariki na ambapo nilihudumu kwa miaka mitano. Wakati wa kuhamishwa ulipoingia, niliacha nikiwa nimewarejeshea utaratibu wa kupenda kuyatunza mazingira na upanzi wa miti,” asema.

Alizingatia sanasana kuimarisha maisha ya vijana na ambapo aliwahamasisha kuhusu kuungana pamoja ili kufuatilia mipango ya serikali.

“Nilichangia sana katika shughuli za upanzi wa miti katika msitu wa Tanyai ambao ulikuwa umeharibiwa kabisa na wavunaji haramu wa miti. Leo hii, ukienda katika eneo hilo utaonyeshwa msitu huo ukiwa na miti 5,000 ambayo kwa ushirikiano na raia tulipanda,” akasema.

Anasema kuwa vijana wa eneo hilo walizindua mtandao wao wa kijamii kwa jina Kieni Youth Forum na ambapo aliwasaidia kunufaika na mipango ya kiserikali ya kuwafathili ili wajitosheleshe kimaisha.

Ndipo alihamishiwa hadi kaunti ya Murang’a na akakumbana na kero la pombe haramu, kudidimia kwa matumaini ya watoto wa kiume na wanaume wengi wakiwa wameishiwa na ujasiri wa kuwa viongozi wa boma kufuatia ulevi uliokuwa umewakosesha heshima.

Bw Nandi ambaye ni baba wa watoto wawili wa kike wa miaka sita na 10 anasema akiwa Murang’a alikumbana na hali ya watoto kukosa wengi wa kuiga maishani.

Anasema kuwa eneo hilo la Kahuro lilikuwa likijijenga upya baada ya kuwa katika uthibiti wa genge haramu la Mungiki kwa zaidi ya miaka 20.

“Badala ya kuzindua vita na raia kupitia misako na kesi mahakamani, niliwaendea polepole walevi na wagema na kupitia mazungumzo, wengi walibadili mienendo,” asema.

Afisa huyu anakiri kwamba humtazama mamake kama ngome yake thabiti katika huduma kwa taifa hili.

“Ndio, siaibiki nikisema kuwa mimi ni mtoto wa mama… Huwa ananipa motisha kupitia upendo na maombi yake. Babangu namshukuru kwa kuhakikisha ninakuwa na nidhamu bora,” asema.

Anasema kuwa nia yake kuu ni kuendelea kuhudumia Wakenya katika ajira yake na azidishe juhudi hizo hadi kiwango cha kimataifa katika siku za usoni.

“Watoto hasa ndio lengo langu kuu. Tukiwekeza rasilimali zetu kwa watoto na tuhakikishe kuwa wamepata elimu na uhamasisho wa maadili, siku za usoni za taifa letu zitakuwa salama,” asema.