CHARLES WASONGA: Wakenya watumie mdahalo wa urais kuchuja wagombeaji wa urais
Na CHARLES WASONGA
UAMUZI wa asasi kuu katika sekta ya uanahabari wa kuandaa mdahalo wa urais mwezi ujao ni wa busara zaidi.
Juzi Baraza la Vyombo vya Habari Nchini (MCK), Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MAO) na Chama cha Wahariri Nchini (KEG) kwa pamoja zilitangaza kuwa zitaendesha mdahalo huo kuanzia Julai 26, siku chache kabla ya Wakenya kuelekea debeni kuwachagua viongozi wapya mnamo Agosti 9.
Mdahalo huo utawafaa Wakenya zaidi ikizingatiwa kuwa uchaguzi wa urais wa mwaka huu ni wa mpito na hivyo unatarajiwa kushuhudia ushindani mkubwa.
Kwanza, mdahalo huo utatoa jukwaa mwafaka kwa wagombeaji urais kuwafafanulia Wakenya kuhusu ahadi nyingi ambazo wamekuwa wakitoa katika mikutano ya kampeni.
Wakenya nao watapata fursa ya kuelewa ahadi hizo, sera na itikadi za kila mgombeaji katika mazingira matulivu na chini ya mratibu mwenye ufahamu na utaalamu mpana.
Vile vile, jukwaa hilo litawapa wapiga kura nafasi ya kupima uwezo wa wagombea urais wa kujieleza na kuchanganua yaliyomo katika manifesto zao.
Kinyume na ‘kelele’ wanazotoa kwenye majukwaa ya kampeni hapa wagombea watatarajiwa kuelezea wananchi kwa utulivu na umakinifu mkubwa jinsi watakavyotekeleza ahadi ambazo wamekuwa wakitoa kila mara.
Kwa mfano, ni matarajio yetu na Wakenya kwa ujumla kwamba Naibu Rais William Ruto ambaye anatarajiwa kuidhinishwa kuwa mgombeaji urais wa muungano wa Kenya Kwanza atafafanua ni wapi atapata Sh100 bilioni kila mwaka za kutoa mikopo kwa wanafanya biashara wadogo.
Naye kiongozi wa ODM Raila Odinga anatarajiwa kutumia jukwaa hilo, kuelezea Wakenya jinsi atatekeleza ahadi yake ya kutoa ruzuku ya Sh6,000 kila mwezi kwa familia masikini.
Muhimu zaidi ni kwamba wapiga kura wanatarajia kuwa wagombea hao wa urais, pamoja na wagombea wenza wao wataelezea kwa kina jinsi watakabiliana na matatizo makuu yanayozonga taifa hili wakati huu.
Miongoni mwa changamoto hizo ni; zimwi la ufisadi, kupanda kwa gharama ya maisha, baa la njaa, mzigo wa deni la kitaifa ambalo limefikia 8. 2 trilioni miongoni mwa zingine.
Naamini kuwa baada ya mdahalo huo, wapiga kura ambao kufikia sasa hawajaamua mgombeaji urais watakayempigia kura wataweza kuamua ni nani bora.