Connect with us

General News

Majangili wavamia kituo na kuua afisa, waiba bunduki 4 na risasi 197 – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Majangili wavamia kituo na kuua afisa, waiba bunduki 4 na risasi 197 – Taifa Leo

Majangili wavamia kituo na kuua afisa, waiba bunduki 4 na risasi 197

NA GEOFFREY ONDIEKI

GENGE la majangili wenye bunduki lilivamia kituo kidogo cha polisi cha Lodokejek katika Kaunti ya Samburu na kuua afisa mmoja, kabla ya kuiba bunduki kadha na risasi.

Wavamizi hao ambao idadi yao haikujulikana, walitekeleza shambulio hilo Jumanne usiku, watawala walisema jana.

Maafisa wawili wa polisi walijeruhiwa katika tukio hilo na wanapokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Samburu mjini Maralal.

Afisa aliyeuawa alitambuliwa kama Joel Muchai, wa cheo cha konstebo, ambaye alipigwa risasi kadha alipokuwa akilinda doria nje ya kituo hicho.

Baadaye wafuasi wa genge hilo waliingia kituoni na kutwaa bunduki nne aina ya G3 na jumla ya risasi 197 kisha wakatoweka.

Kamishna wa Kaunti ya Samburu, Bw Henry Wafula, ambaye alithibitisha kisa hicho, alisema polisi wanawasaka majangili hao.

“Afisa wetu aliuawa katika kituo hicho na wengine wawili wamelazwa hospitalini wakitibiwa majeraha ya risasi. Tunalaani vikali kisa hiki. Tumeanzisha msako wa wahalifu hao ambao walitoweka baada ya kisa hicho,” Bw Wafula akaambia Taifa Leo jana.

Aliongeza kuwa maafisa wa usalama zaidi wamepelekwa eneo hilo akiongeza kuwa maafisa wa polisi waliokuwa kituoni wamethibitisha kuwa walivamiwa na majangili waliokuwa wakitumia pikipiki.

Mashambulio sawa na hiyo yameshuhudiwa katika maeneo kadha ya Kaunti ya Samburu ambako kuna idadi kubwa ya majangili.

Kituo kidogo cha polisi cha Lodokejek ni cha nne kuvamiwa na majangili katika kaunti hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Mnamo Januari 3, walishambulia kituo kidogo cha polisi cha Lerata katika eneo bunge la Samburu Mashariki na wakaua afisa mmoja wa polisi

wa cheo cha konstebo. Kituo hicho cha polisi kiko karibu na barabara ya Wamba-Achers Post.

Mnamo Novemba mwaka jana, majangili walivamia kituo kidogo cha polisi cha Kirimon na kuiba bunduki mbili aina ya G3.

Mnamo Januari mwaka huu, wavamizi wenye bunduki walivamia kituo cha polisi cha Achers post na kuwajeruhi maafisa kadha.

Vituo kadha vya polisi vilibuniwa katika kaunti ya Samburu wakati ambapo David Kimaiyo na Joseph Boinnet walihudumu kama inspekta wakuu wa polisi ili kupambana na wezi wa mifugo na wahalifu wengine.