Njaa kuumiza Wakenya zaidi
NA MARY WANGARI
HALI ya ukame inayoshuhudiwa katika maeneo mengi nchini inatarajiwa kuendelea huku Wakenya zaidi ya milioni mbili wakihitaji msaada wa dharura kutokana na uhaba wa chakula nchini.
Kulingana na taarifa iliyotolewa jana na Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga, maeneo kadhaa ikiwemo Pwani na Kaskazini Mashariki mwa Kenya yanatarajiwa kupokea mvua ya kiwango cha chini msimu wa masika ukianza mwezi huu.
Wakazi katika Kaunti za Pwani ikiwemo Lamu, Mombasa, Kwale, Kilifi na baadhi ya sehemu za Tana River watalazimika kuendelea kukabiliana na nyakati ngumu zijazo kutokana na uhaba wa maji na chakula huku mvua chache ikitarajiwa mwishoni mwa mwezi huu.
Aidha Kaunti za Samburu, Turkana, Wajir, Isiolo, Garissa, Marsabit na Mandera katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya zinatarajiwa kushuhudia makali ya ukame huku zikitarajia tu rasharasha mwishoni mwa mwezi huu hadi wiki ya kwanza ya Aprili.
“Msimu huu unatarajiwa kuanza kwa namna ya kawaida huku mvua ikinyesha kote nchini; isipokuwa katika maeneo kame ya Kaskazini Magharibi, Kaskazini Mashariki na Pwani ambayo yatashuhudia mvua chache,” ilieleza taarifa hiyo ya hali ya anga.
“Maeneo ya Kaskazini Mashariki, Kaskazini Magharibi na Pwani ambayo yamekuwa yakishuhudia vipindi vya jua na kiangazi katika nusu ya kwanza ya Machi huenda yakapata rasharasha za mvua katika wiki ya mwisho ya Machi hadi wiki ya kwanza Aprili zitakazoashiria mwanzo wa vua za masika eneo hilo.”
Taarifa hiyo inayoangazia kipindi kinachoanzia Machi 15-21, inaashiria kuwa maeneo mengineyo yanayokaribia Ziwa Victoria, sehemu za milimani Magharibi mwa Bonde la Ufa, Kusini mwa Bonde la Ufa, baadhi ya sehemu za milimani Mashariki mwa Bonde la Ufa na maeneo tambarare Kusini Mashariki (Kajiado na Taita Taveta) yatapokea rasharasha.
Hata hivyo, vua hizo za masika zilizoanza mwezi uliopita zinatarajiwa kuendelea kunyesha katika Kaunti zinazokaribia Ziwa Victoria ikiwemo Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, pamoja na maeneo ya Kusini mwa Bonde la Ufa kama vile Narok, Bomet, Kericho na Kajiado.
Kaunti za milimani Magharibi mwa Bonde la Ufa ikiwemo Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi, Nandi, Kakamega, Vihiga, Bungoma na Busia zinatarajiwa kuanza kupokea mvua mwishoni mwa Machi katika wiki ya tatu.
Vua hizo zinatarajiwa kuanza kunyesha mwishoni mwa Machi katika wiki ya nne kwenye sehemu za milimani Mashariki mwa Bonde la Ufa ikiwemo kaunti za Nairobi, Kirinyaga, Murang’a, Embu, Meru, Kiambu na Nyandarua.
Maeneo ya Katikati mwa Bonde la ufa linalojumuisha Kaunti za Nakuru na Laikipia pamoja na sehemu tambarare Kusini Mashariki zinazojumuisha Kaunti za Kajiado, Kitui, Makueni, Machakos, Taita Taveta na baadhi ya maeneo ya Tana River yatalazimika vilevile kusubiri vua hizo hadi mwishoni mwa Machi ambapo zinatarajiwa kuanza.