Connect with us

General News

Nassir ana nafasi nzuri kumrithi Joho, utafiti waonyesha – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Nassir ana nafasi nzuri kumrithi Joho, utafiti waonyesha – Taifa Leo

Nassir ana nafasi nzuri kumrithi Joho, utafiti waonyesha

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, ana nafasi bora kurithi kiti cha Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, katika uchaguzi ujao kulingana na kura ya maoni.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na shirika la Infotrak inaonyesha kuwa uchaguzi ungefanywa leo, Bw Nassir angezoa asilimia 48 ya kura za ugavana, akifuatwa na mfanyabiashara Suleiman Shahbal (asilimia 18).

Wawili hao wanashindania tikiti ya Chama cha ODM kwa sasa, na hivyo basi matokeo ya utafiti huo yanaashiria ushindani mkali unaotarajiwa endapo chama kitafanya kura ya mchujo.

Duru zilisema ODM inaendeleza utafiti huru kubainisha mwanasiasa aliye na umaarufu zaidi kati yao.

Aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, ambaye ni mwanachama wa United Democratic Alliance (UDA), angeibuka wa tatu kwa mbali akiwa na asilimia 5 ya kura, huku Mbunge wa Kisauni, Bw Ali Mbogo, ambaye ni mwanachama wa Wiper, angefuata kwa asilimia 4.

Bw Nassir angepata kura nyingi eneobunge lake la Mvita (asilimia 62), Likoni (asilimia 53) na Jomvu (asilimia 49).

Matokeo hayo yameibua hisia mseto kati ya Bw Nassir na Bw Shahbal ambao ni wapinzani wa karibu kufikia sasa.

Bw Nassir alisema utafiti huo unadhihirisha namna uchaguzi mkuu utakavyokuwa.

“Wakati ninauza sera zangu, wapinzani wangu wanaendelea kuniuza kwa kunifanya ajenda kwenye mikutano yao ya siasa. Wanadhania wananiharibia kumbe wananiongezea umaarufu. Sera zangu ni za kutatua changamoto za wananchi,” akasema Bw Nassir.

Hata hivyo, wandani wa Bw Shahbal walipuuzilia mbali utafiti huo, wakisema utafiti unaofanywa na ODM ndio utatumiwa kufanya maamuzi.

Licha ya mrengo wa Bw Shahbal kutilia shaka utafiti huo, shirika la Haki Africa lililoufadhili lilisema halipendelei upande wowote kisiasa.

Mkurugenzi Mkuu wa Haki Africa, Bw Hussein Khalid, alisema nia yao kuu ilikuwa ni kutambua maeneo yanayoweza kuwa na ghasia za uchaguzi ili mikakati iwekwe mapema.

“ODM, UDA na Jubilee vimeibuka kama vyama ambavyo vurugu zinaweza kushuhudiwa kwenye kampeni zao,” akasema.

Kando na ugavana, utafiti huo pia ulibainisha kuwa, Seneta Mohamed Faki, angeshinda tena kwa asilimia 21, akifuatwa na Bw Hamisi Mwaguya kwa asilimia tano.

Bw Mohamed Amir, ambaye ni kakake Bw Joho, angelipata asilimia moja pekee ya kura za useneta. Bw Amir na Bw Mwaguya wanashindania tikiti ya UDA kuwania useneta.

Katika kinyang’anyiro cha Mbunge Mwakilishi wa Kike, Bi Asha Hussein angeshinda tena kwa asilimia 17, akifuatwa na Bi Zamzam Mohamed, kwa asilimia kumi.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending