[ad_1]
WANTO WARUI: Tume ya elimu ya juu iadhibu vyuo vikuu vinavyotoa digrii feki
Na WANTO WARUI
MARA kwa mara, sekta ya elimu humulikwa kwa kile kinachoaminika kuwa ukosefu wa uwajibikaji katika utendakazi na tamaa ya pesa.
Vyuo zaidi ya kumi kote nchini vimeorodheshwa kwa kuanzisha na kutoa mafunzo ya digrii ambazo hazijaidhinishwa na Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu nchini (CUE).
Hii ina maana kuwa, wanafunzi wanaosomea digrii hizo wanapoteza pesa na muda wao bure.
Miongoni mwa vyuo vilivyoorodheshwa kwa kutoa mafunzo hayo yasiyokubalika ni Chuo kikuu cha Tom Mboya, Kisumu ambacho kina kozi 25 zilizofutiliwa mbali.
Hii inamaanisha kuwa, kuna wanafunzi waliokuwa washaanza kusomea digrii hizo hata wengine kumaliza masomo yao. Ikiwa digrii hizo ni feki ama hazina maana nchini, hii itakuwa gharama kubwa kwa wazazi na wanafunzi waliosomea kozi hizo.
Jambo kama hili kutokea katika sekta ya elimu linaashiria kuzorota kwa usimamizi wa elimu nchini, hasa katika usajili wa vyuo vikuu na usimamizi wake.
Wasimamizi wa vyuo vikuu ambao wanaongozwa na tamaa ya pesa hawafai kuachiliwa waendelee na mbinu hizo potovu bali wanafaa kufikishwa mahakamani.
Aidha, wanafunzi ambao wamepoteza muda wao na pesa katika digrii hizo zisizo na maana wanafaa kufidiwa mara moja ili waweze kuendelea na maisha yao. Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) inafaa kukagua vyuo vyote nchini ili kubaini vile ambavyo havifuati taratibu zilizowekwa kuhusu elimu ya juu.
Vyuo vikuu ambavyo havijakamilisha taratibu zote vinafaa kunyang’anywa leseni au kufungwa ili kuhakikisha kanuni zifaazo za masomo ya vyuo vikuu zinafuatwa.
Next article
WANDERI KAMAU: Ni wakati mwafaka wa kudhibiti kinywa…
[ad_2]
Source link