[ad_1]
Khalwale ampisha Malala kwa ugavana Kakamega
NA CHARLES WASONGA
ALIYEKUWA Seneta wa Kakamega Dkt Boni Khalwale amejiondoa kutoka kinyang’anyiro cha ugavana katika kaunti hiyo.
Dkt Khalwale ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto sasa amempisha mwenzake, Seneta wa Kakamega Cleophas Malala awanie kiti hicho. Badala yake Mbunge huyo wa zamani wa Ikolomani sasa atawania kiti cha Useneta wa Kakamega kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Muafaka kati ya Khalwale na Malala ulifikiwa katika mkutano ambao ulioongozwa na Dkt Ruto katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mkurugenzi wa mawasiliano katika sekritariati ya kuongoza kampeni za urais wa Dkt Ruto, Mohamed Hussein.
Dkt Khalwale na Bw Malala wamekuwa wakivutana kuhusu ni nani atafaa kupeperusha bendera ya muungano wa Kenya Kwanza katika uchaguzi wa ugavana wa Kakamega.
Kujiondoa kwa Dkt Khalwale sasa kunamaanisha kuwa Bw Malala atapambana na Fernandez Barasa wa ODM ambaye anapigiwa upatu kupewa tiketi ya Azimio la Umoja.
[ad_2]
Source link