DOUGLAS MUTUA: Familia za kisiasa duniani zajua wakati wa uhasama, kuungana
NA DOUGLAS MUTUA
FAMILIA tatu mashuhuri za kisiasa nchini Kenya kuungana ili kujaribu kushinda Uchaguzi wa urais ifikapo Agosti 9, 2022 si jambo geni duniani.
Labda ni geni tu kwa limbukeni wa siasa kwa kuwa, nyakati fulani familia za Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Oginga Odinga zimewahi kuwa na misimamo tofauti.
Kutokana na umaarufu wa majina ya familia husika katika nchi mbalimbali, miungano ya kisiasa isiyotarajiwa imeshuhudiwa na kuishia kuwa na matokeo ya ajabu.
Kwa taarifa yako, wakati huu ambapo Rais Uhuru Kenyatta anamuunga mkono aliyekuwa adui wake wa kisiasa, Raila Odinga, tukio jingine linafanyika nchini Ufilipino.
Rais anayeondoka, Rodrigo Duterte, amemuunga mkono shingo upande tu Ferdinand ‘Bongbong’ Marcos Junior, mwana wa aliyekuwa dikteta wa taifa hilo, Ferdinand Marcos.
Ingawa Marcos Junior anawania urais kwa chama tofauti na cha Rais Duterte, inaaminika kiongozi huyo wa nchi amelazimika kumuunga mkono kwa kugundua kuwa huenda akashinda uchaguzi utakaofanyika mapema mwezi Mei mwaka huu wa 2022.
Si hayo tu! Rais Duterte, anatamani kumwona binti yake mwenyewe, Bi Sara Duterte, akifanya kazi kama naibu rais wa Marcos Junior.
Binti ya Rais Duterte ndiye anayepigiwa upatu kushinda uchaguzi wa naibu rais, hivyo baba mtu anamuunganisha na atakayekuwa mkubwa wake – Marcos Junior.
Mamlaka yana utamu wake, kwa hivyo si ajabu kuwaona waliotangulia kila mtu kuingia ikulu au kasri wakitaka kurejea huko tena, hata ikibidi wasahau uadui wao kwa muda.
Tangu mwanzo, Rais Dutarte hakutaka Marcos Junior amrithi, hata amewahi kumwita dhaifu, lakini umaarufu wake na nia ya kutaka awe na ubia na binti yake umemlazimisha.
Ushirikiano wa aina hiyo ulishuhudiwa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pale waliokuwa maadui wa kisiasa walipoungana kuitawala nchi.
Joseph Kabila alipoondoka mamlakani yapata miaka mitatu iliyopita hakupoteza muda hata kidogo, bali alimuunga mkono Felix Tshisekedi na kumwezesha kuunda serikali.
Ukitaka kuamini kwamba, hakuna maadui wa kudumu katika siasa, hasa miongoni mwa familia maarufu, chunguza hali imekuwa vipi nchini Uganda.
Rais Yoweri Museveni amekuwa akishirikiana na wana wa marehemu dikteta Idd Amin; baadhi ya wajukuu wa Amin ni wanasiasa maarufu wa chama cha Museveni, National Resistance Movement (NRM).
[email protected]