Uzalishaji kawi kupitia samadi ya mifugo, kupunguza gharama ya umeme
Na SAMMY WAWERU
GHARAMA ya maisha inazidi kupanda kila uchao, licha ya taifa na ulimwengu kuendelea kupambana na janga la Covid-19.
Machi 2020, Kenya ilithibitisha kuwa mwenyeji wa virusi vya corona, ambavyo vimesambaratisha uchumi wa mataifa mengi. Mamia, maelfu na mamilioni ya wananchi Kenya waliathirika kwa njia moja ama nyingine, ikiwemo kupoteza ajira, biashara kufungwa na baadhi ya kampuni na hoteli kusitisha huduma.
Msambao wa virusi vya corona umechochea gharama ya maisha kukwea mara dufu. Si bei ya mafuta ya petroli, bidhaa za kula, fatalaiza, kati ya mahitaji mengine muhimu ya kimsingi, vyote vinaendelea kuwa ghali. Siku chache zilizopita, bei ya gesi ya mapishi ilipandishwa mara dufu.
Mfumko huo umejiri kipindi ambacho mafuta ya petroli, yakiwemo yale ya taa yanayotumika katika stovu bei haikamatiki. Gharama ya nguvu za umeme nayo ni ghali. Licha ya maisha kuendelea kuwa magumu, kiwango cha mapato kikisalia kilipokuwa, Fredrick Njunguna hahisi makali ya nguvu za kawi.
Eneo la Kamahuha, Kaunti ya Murang’a, Njuguna amezindua matumizi ya bayogesi kuzalisha nguvu za umeme zinazotumika kuwasha mataa na katika mapishi nyumbani kwake. Akiwa mkulima hodari wa matunda kama vile matomoko, maparachichi maarufu kama avokado na maembe, Njuguna pia ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa.
Fredrick Njuguna, akiongeza kinyesi cha mifugo eneo analozalisha nguvu za umeme na gesi kupitia bayogesi…Picha/ SAMMY WAWERU
Hutumia kinyesi cha ng’omge kuzalisha kawi, kupitia bayogesi. “Bayogesi haihitaji mwalimu. Mkulima yeyote yule mwenye mifugo anaweza kuizalisha” asema. Mita chache kutoka majengo ya boma lake, Njuguna ametenga eneo maalum kwa minajili ya shughuli hiyo.
Kando na kutumia kinyesi cha mifugo wake katika kukuza mseto wa matunda na mimea, anakitumia kuzalisha gesi na nguvu za umeme. “Ng’ombe wanapoenda haja, hukusanya kinyesi chao eneo moja na kukigeuza kuwa nguvu za umeme na gesi,” aelezea.
Aidha, kinyesi kinaporundikwa na kufunikwa huunda gesi na nguvu za umeme, taratibu za kuikusanya na kuielekeza kwenye jiko na nyaya za umeme zikifuatwa. Samuel Mwaniki, mkulima eneo la Joska, Malaa, Kaunti ya Machakos, pia huzalisha bayogesi.
“Kinyesi kinachotumika kikimaliza kutekeleza shughuli hiyo vilevile ni mbolea,” Mwaniki asema. Mkulima huyu pia ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa. Mwaniki hukuza aina tofauti ya vitunguu, pilipili mboga, nyanya na mseto wa mboga.
Kwa kauli moja, wanakiri bayogesi inapunguza kwa kiasi kikubwa gharama kulipia nguvu za umeme na kujaza gesi za mapishi. Kwa mfano, mtungi wa kilo 6 wa gesi baada ya idara ya kawi kutathmini bei majuzi unachezea Sh1, 500, juu kutoka Sh600 – 700 kabla Corona kuingia nchini.
“Bayogesi inatekeleza majukumu ya mapishi na haina gharama yoyote,” wanasema. Ni ubunifu ambao ukikumbatiwa na wafugaji, utawaletea afueni na zaidi ya yote kusaidia kupunguza gharama ya maisha. U“Kwangu, hutumia kawi ya bayogesi kuwasha mataa stima zinaposumbua na mapishi. Unachohitaji ni kinyesi cha mifugo pekee,” Njuguna aelezea, akihimiza wafugaji wenza kufumbua macho.
Akishangaa ni kwa namna gani wanaendelea kuwa mateka wa gharama ya juu ya gesi na nguvu za umeme, anasisitiza maliasili waliyonayo itawawezesha kujikwamua.
Samuel Mwaniki akionyesha eneo analotumia kuzalisha gesi ya mapishi na nguvu za umeme kupitia bayogesi…Picha/ SAMMY WAWERU