[ad_1]
Wahudumu wa matatu, bodaboda wapandisha nauli
Na KENYA NEWS AGENCY
WAHUDUMU wa matatu na bodaboda katika kaunti za Kericho na Uasin Gishu wameanza kupandisha nauli huku wakulima wakichelewa kulima mashamba yao kutokana na uhaba wa mafuta.
Katika kaunti za Kericho na Uasin Gishu, mamia ya wasafiri jana walianza kuhisi athari ya uhaba huo wa mafuta huku wakitatizika kufanikisha safari zao na kutozwa nauli ya juu. Uhaba huo wa mafuta ulianza kushuhudiwa mnamo Jumapili.
“Tunatumai kuwa serikali itasaka suluhu kwa sababu shughuli zetu za kibiashara haziwezi kuendelea bila mafuta. Kwa sasa tunanunua lita moja ya petroli kwa Sh135 na hatuna jingine ila kuvumilia bei hiyo ya juu,” akasema mfanyabiashara Ezekiel Kimutai.
“Wahudumu wa matatu na bodaboda tayari wamepandisha nauli na hilo linatuumiza mno. Nina wingu la matumaini hali itarejea kama kawaida,” akasema msafiri Nancy Chebet akiwa Kericho.
Kando na wasafiri, wakulima wanaotumia tingatinga kuyalima mashamba yao nao pia wanakabiliwa na shida kutokana na uhaba huo huku msimu wa upanzi nao ukibisha.
Mjini Kericho, ni kituo cha petroli cha Total kilichokuwa na mafuta pekee. Kulishuhudiwa msongamano wa magari na pikipiki huku vituo vingine vikisalia mahame kwa kukosa petroli.
Kupitia taarifa, Mamlaka ya Kudhibiti Kawi Nchini (EPRA) iliwaondolea wananchi wasiwasi ikisema kuwa kuna mafuta yanayotosheleza matumizi ya kila raia hapa nchini.
EPRA ilisema kuwa Wizara ya Kawi, kampuni za kuuza mafuta pamoja na washikadau katika sekta ya kawi, wanaendelea kusuluhisha matatizo yanayoathiri uwasilishaji wa bidhaa hiyo muhimu.
Next article
Mhubiri ashtakiwa kwa madai ya kuchafua mtoto
[ad_2]
Source link