Ukraine yasema imetwaa jiji kuu
NA AFP
KYIV, UKRAINE
UKRAINE imesema kuwa “imechukua udhibiti” wa mji mkuu, Kyiv, baada ya vikosi vya Urusi kuanza kujiondoa katika baadhi ya maeneo muhimu ya nchi hiyo iliyokuwa ikiyakalia.
Jumamosi, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Ganna Maliar, alitaja hilo kama “mwanzo kwa taifa hilo kukomboa himaya yake.”
“Tayari, tumefanikiwa kuyakomboa maeneo ya Irpin, Bucha na Gostomel kutoka kwa wavamizi wetu,” akasema Maliar, kwenye ujumbe alioweka kwenye mtandao wa Facebook.
Miji hiyo ambayo iko kaskazini magharibi mwa Kyiv, ni miongoni mwa maeneo yaliyoharibiwa vibaya kufuatia uvamizi wa Urusi mnamo Februari 24.
Miji ya Irpin na Bucha ilitwaliwa tena na majeshi ya Ukraine wikendi.
Waandishi wa shirika la AFP walisema kuwa walihesabu miili karibu 20 katika barabara moja pekee katika mji wa Bucha, Jumamosi. Mmoja wa waathiriwa hao alikuwa amefungwa mikononi mwake kwa kamba.
Meya wa mji huo alisema jumla ya watu 280 walizikwa katika kaburi la pamoja mjini Bucha. Alisema kuwa mamia ya miili ya watu imetapakaa kwenye barabara za mji huo.
Maafisa wa serikali wanasema kuwa karibu watu 200 wameuawa katika mji wa Irpin, tangu Urusi ilipoanza uvamizi huo.
Wanajeshi wanaoukarabati upya walisema wamefanikiwa kuzima makombora 643 tangu kuchukua udhibiti wake.
Hata hivyo, mapigano makali yalishuhudiwa katika eneo la Gostomel, karibu na Kyiv, ambapo vikosi vya Urusi vilikuwa vikijaribu kuchukua udhibiti wa uwanja mmoja wa ndege.
Ukraine imesema Urusi pia inajiondoa katika maeneo ya kaskazini, huku ikionekana kuangazia maeneo ya mashariki na kusini.
Wakati huo huo, Latvia imesema kuwa mataifa ya eneo la Baltic yameacha kuagiza gesi kutoka Urusi kufuatia hatua yake kuivamia Ukraine.
Nchi hiyo ilisema mataifa hayo yalichukua hatua hiyo baada ya “kupoteza imani kutoka kwa Urusi.”
“Mwelekeo wa matukio ya sasa unaonyesha hatuwezi kuiamini Urusi. Hatuamini ikiwa gesi tutakayoagiza itafika katika mataifa yetu ikiwa salama,” akasema Uldis Bariss, ambaye ndiye Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Conexus Baltic Grid kutoka Latvia.
“Tangu Ijumaa, mataifa ya Latvia, Estonia na Lithuania hayajakuwa yakipokea gesi kutoka Urusi,” akasema Jumamosi, kwenye mahojiano na Kituo cha Radio cha Latvia. Alisema kuwa mataifa hayo yameanza kutafuta gesi mbadala kutoka maeneo mengine.
Hilo linajiri licha ya Rais Vladimir Putin kuweka juhudi kuifanya Urusi kuwa taifa linaloongoza kwenye uzalishaji wa gesi asilia duniani.
Huku uchumi wa Urusi ukiendelea kuathirika kutokana na msururu wa vikwazo ambavyo imewekewa na mataifa ya Magharibi, Rais Putin ameonya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) kuwa lazima waheshimu mikataba iliyopo kwa kulipia gesi hiyo.
Alisema Urusi itakatiza mikataba hiyo yote ikiwa hayatailipa kwa gesi ambayo tayari yashatumia.
Nchi za Ulaya huwa zinanunua karibu nusu ya gesi asilia inayozalishwa nchini Urusi.
Rais Gitanas Nauseda wa Lithuania aliyarai mataifa ya Ulaya kufuata mfano wa taifa lake.
“Kuanzia mwezi huu kuendelea, hatutanunua gesi yoyote kutoka Urusi,” akasema, kwenye ujumbe alioweka kwenye mtandao wa Twitter.
Licha ya Ukraine kudai kutwaa baadhi ya maeneo muhimu, milipuko kadhaa iliripotiwa kusikika katika mji wa bandarini wa Odessa.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilithibitisha kutekeleza mashambulio hayo.
Next article
Simu za Sudi, Kositany zatwaliwa na DCI baada ya kuhojiwa…