Connect with us

General News

Kiini cha hospitali kuu kupewa jina la mfalme – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kiini cha hospitali kuu kupewa jina la mfalme – Taifa Leo

MAKALA MAALUM: Kiini cha hospitali kuu kupewa jina la mfalme

NA KALUME KAZUNGU

KWA wakazi wengi wa Kaunti ya Lamu, Hospitali ya Rufaa ya King Fahd iliyo katika kisiwa cha Lamu huwa ni kimbilio chao kwa matibabu kwa vile ndiyo taasisi kubwa zaidi ya afya eneo hilo.

Hospitali hiyo ilizinduliwa miaka ya themanini na kufikia sasa imepiga hatua katika utoaji wa huduma za afya kiasi cha kufikia kiwango cha hospitali ya Daraja la Tano.

Mbali na kutekeleza majukumu ya kutoa huduma za afya kwa wakazi, taasisi hiyo pia ina umuhimu wake katika historia ya kisiwa cha Lamu ambao wengi hawafahamu.

Hii ni kutokana na kuwa, Hospitali ya King Fahd ni mojawapo ya majengo ambayo yamechangia pakubwa katika kuufanya mji wa kale wa Lamu kuorodheshwa na Umoja wa Mataifa kuwa miongoni mwa maeneo yanayotambulika zaidi ulimwenguni kwa kuhifadhi ukale wake.

Zamani hospitali hiyo ilikuwa ikijulikana kuwa hospitali kuu ya tarafa ya Lamu.

Uchunguzi umebainisha kuwa, King Fahd ni jina lililozuka baada ya Mfalme wa Saudi Arabia, Fahd Ibn Abdulaziz Al Saud kutoa kima cha zaidi ya Sh100 milioni ili kufadhili kujengwa upya kwa taasisi hiyo mnamo mwaka 1984 kwa manufaa ya jamii ya Lamu na Kenya kwa jumla.

Chini ya uongozi wa Rais Mstaafu, marehemu Daniel arap Moi, mradi huo kwanza ulianza kutekelezwa eneo la Mokowe lakini baada ya wananchi wa kisiwa cha Lamu kulalamikia umbali wa kufikia kituo hicho, mradi ukasitishwa na ujenzi mpya kuanza kutekelezwa mjini Lamu.

Mradi huo ulikamilika 1989 ambapo jamii ya Lamu, katika harakati za kudhihirisha shukrani na kumuenzi mfalme wa Saudi Arabia wakaamua kuipa hospitali hiyo jina la King Fahd ambalo limedumu hadi wa leo.

Licha ya mfalme Fahd kufariki mwaka 2005, kumbukumbu zake bado zipo Lamu, hasa uwepo wa hospitali hiyo ya King Fahd.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Naibu Mkurugenzi wa idara ya turathi za kitaifa anayesimamia ukanda wa Pwani, Bw Athman Hussein alisema ramani iliyopitishwa na kujengewa hospitali ya King Fahd ni ya aina yake kwani haikwenda kinyume na ramani za nyumba za kale za Lamu zinazoshabihiana na misikiti.

Bw Hussein anasema wakati mikakati ya kujengwa kwa hospitali ya King Fahd ilipoanza mwaka 1982, mazungumzo tayari yalikuwa yanaendelea kuhusiana na pendekezo la Lamu kuorodheshwa na Unesco kuwa sehemu ya ukale na historia.

“Ilibidi serikali ya Kenya na ile ya Saudi Arabia kupitisha ramani ya hospitali hiyo ambayo haikukinzana na majumba ya kale ya Lamu. Ndiyo maana ukiitazama hospitali ya King Fahd utapata ni kama msikiti. Miaka 12 baada ya hospitali kukamilika, Lamu ikafanikiwa kujumuishwa katika sehemu za ukale wa kipekee ulimwenguni mnamo 2001. Naweza kusema ramani ya hospitali ya King Fahd pia ilichangia ufanisi wa historia ya mji wa Kale wa Lamu,” akasema Bw Hussein.

Naye Mkurugenzi wa Matibabu wa Kaunti ya Lamu, Abubakar Baasba aliushukuru utawala wa Saudi Arabia kwa ufadhili wake wa ujenzi wa hospitali ya King Fahad ambayo miongo miwili unusu baadaye imekua na kupanuka pakubwa na kuwa taasisi kuu inayotegemewa na wote Lamu.

Dkt Baasba alisema hospitali hiyo kwa sasa inatoa huduma kwa wananchi kwa masaa 24.

“Pia tuko na wataalamu wa afya wanaoshughulikia matibabu maalum kama vile usafishaji wa figo, upasuaji, matibabu ya macho, masikio na pua (ENT), miongoni mwa huduma zingine. Isingekuwa ufadhili wa mfalme Fahd wa Saudi Arabia, sidhani hospitali yetu kuu ya King Fahd ingefikia kiwango ilipo leo,” akasema Dkt Baasba.

Hata hivyo, sawa na hospitali nyingine zinazohudumia idadi kubwa ya umma, hospitali hiyo pia hukumbwa na changamoto zake mara kwa mara.

Hivi majuzi, Serikali ya Kaunti ya Lamu ililazimika kufunga kitengo cha matibabu ya figo katika hospitali hiyo kwa muda usiojulikana.

Hii ni kutokana na uhaba wa maji ambao kwa muda mrefu umekumba kitengo hicho baada ya mtambo wa kusafisha maji kwa matumizi ya mashine za kusafishia figo kwenye hospitali hiyo kuharibika.

Taifa Leo ilibaini kuwa wagonjwa wote wa figo 15 ambao wamekuwa wakitegemea hospitali hiyo kufuatilia matibabu yao tayari walikuwa wamepewa rufaa kutafuta huduma hiyo ya kusafisha figo kwenye hospitali mbalimbali mjini Mombasa.

Lamu kwa sasa ina jumla ya idadi ya watu 143,920 kulingana na ripoti ya sensa ya mwaka 2019 ambao wote hutegemea hospitali hiyo punde wanapopewa rufaa ya kimatibabu kwa hospitali kuu kutoka zahanati zilizoko karibu nao.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending