Connect with us

General News

Mwalimu mwenye kipaji cha uandishi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mwalimu mwenye kipaji cha uandishi – Taifa Leo

MWALIMU WA WIKI: Mwalimu mwenye kipaji cha uandishi

NA CHRIS ADUNGO

KWA kuwa uwezo wa wanafunzi wa kumudu masomo hutofautiana, mwalimu ana ulazima wa kuelewa kiwango cha kila mwanafunzi na kubuni mbinu za ufundishaji zitakazomwezesha kila mmoja wao kufikia malengo yake.

Mwanafunzi aliye na uwezo wa chini kimasomo huvunjika moyo upesi iwapo mwalimu ataanza kumlinganisha na wenzake wanaoelewa mambo haraka.

Mbinu rahisi zaidi ya kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa masomo miongoni mwa wanafunzi ni kuwaaminisha kwamba hakuna lisilowekezana.

Haya ni kwa mujibu wa mwalimu Otieno Mjomba ambaye sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika shule ya St Jude Doonholm (awali ikiitwa Doonholm Catholic) jijini Nairobi.

“Nashirikisha ubunifu wa kiteknolojia katika ufundishaji wangu”

Pamoja na kutumia vifaa vya kidijitali ambavyo husisimua sana wanafunzi, matumizi ya video na picha ni namna nyingine ya kufanya masomo kuvutia.”

“Kuwahusisha wanafunzi moja kwa moja huwapa fursa ya kufanya mambo kwa kujiamini. Mawanda ya fikira zao hupanuka zaidi na huanza kuona vitu wanavyofundishwa vikiwa vya kawaida mno,” anaeleza.

Otieno Mjomba alizaliwa yapata miongo mitatu iliyopita katika kijiji cha Kanyaudo, Kaunti ya Siaya. Alisomea katika shule za msingi za Kanyaudo na Nyalenya kabla ya kujiunga na shule ya upili ya St Paul’s Ndenga (Siaya) kisha chuo cha mafunzo ya ualimu cha International Teaching & Training Centre (ITTC), Dagoretti (2006-2008).

Yeye kwa sasa ni mwanafuzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Moi anakosomea taaluma ya masuala ya mawasiliano na mahusiano ya umma.

Baada ya kuhitimu ualimu mnamo 2008, alianza kufundisha katika shule ya Summit Vine Academy, Kaunti ya Kiambu kabla ya kuhamia Acacia Green Academy (Kiambu) kisha Junel Academy, Kaunti ya Nairobi.

Mjomba aliwahi pia kufundisha katika shule za Jubilant Junior (Ruai) na Rockfields Junior (Nairobi) kabla ya kujiunga na St Jude Donholm mnamo 2020 na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili.

Zaidi ya kufundisha, Mjomba ni mwandishi wa vitabu na mshauri nasaha chini ya mwavuli wa kampuni ya Niken Marketing and Communications Ltd aliyoianzisha kwa pamoja na Bw Zadock Amakoye na Bw Egidio Ndung’u mnamo 2020.

Kampuni hiyo inayotoa ushauri nasaha kwa wanafunzi na walimu, pia hushughulikia uundaji wa mipango mikakati ya mashirika mbalimbali pamoja na kuandaa sherehe na tafrija za kila sampuli katika kiwango cha mtu binafsi, kundi la watu au shirika.

Baadhi ya vitabu vyake ni ‘Fumbuo la Insha’, ‘Fumbuo la Msamiati’ na novela ya Kiingereza ‘Sour Grape’ inayopatikana kwenye Amazon.com. Ana miswada mingi ya riwaya ambayo sasa ipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika kampuni na mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu.

Mjomba pia ni mtaalamu wa elimu ambaye hushiriki mahojiano na mijadala ya kitaaluma kwenye redio na runinga za humu nchini huku akiandika makala ya elimu na siasa katika gazeti la ‘Daily Nation’ linalomilikiwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG).

Kwa kutumia kipaji chake cha uandishi, Mjomba amepiga hatua kubwa katika ufundishaji kutokana na upekee wa kuoanisha talanta, ujuzi wa kiteknolojia na taaluma alizozisomea.

Yeye kwa sasa hupeperusha kipindi ‘Fumbuo la Kiswahili’ kupitia ‘Paukwa Radio Podcast’.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuwa miongoni mwa walimu watakaobadilisha sura ya ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kiteknolojia katika enzi hizi za utandawazi.