Wazee kutakasa eneo la shambulio dhidi ya Raila
NA FRED KIBOR
WAZEE wa jamii ya Kalenjin watafanya tambiko la kutakasa eneo ambako mwaniaji urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, alishambuliwa katika shamba la marehemu Mzee Jackson Kibor, Kaunti ya Uasin Gishu.
Helikopta iliyokuwa ikimbeba Bw Odinga, ilishambuliwa kwa mawe Ijumaa wiki jana baada ya mwanasiasa huyo kuondoka katika boma la mwendazake katika eneo la Kabenes, eneobunge la Soy.
Baraza la Wazee wa Kalenjin (Myoot) tawi la Uasin Gishu, lililaani kitendo hicho na kutangaza kuwa baada ya kukamilika kwa siku 40 za maombelezi, wanachama wake watakongamana katika shamba la Mzee Kibor kufanya maombi ya utakaso.
Wazee hao, walisema hiyo ni kulingana na mila na desturi za jamii ya Kalenjin.Walionya kuwa kitendo hicho ni kama laana kwa jamii na kinaweza kusababisha maafa, haswa mashambulio kama hayo yanapotekelezwa wakati wa hafla ya mazishi.
Wakiongea Jumanne walipotembelea eneo la tukio, ambako Bw Odinga alishambuliwa, wazee hao walisema kitendo kama hicho hakijawahi kutokea katika jamii ya Wakalenjin.
Walisema kuwa kutakasa eneo hilo kutahakikisha kuwa tukio kama hilo halitarudiwa wakati mwingine.
“Baada ya kukamilika kwa siku 40 za maombolezi, tutafanya maombi ya kijamii na sherehe ya utakaso kwa sababu kile ambacho kilitendeka ni mwiko na hakikubaliki katika mila na desturi zetu. Kitendo kama hicho hakijafanyika siku nyingine na tunahimiza kwamba kisitendeke wakati mwingine, “akasema Bw David Singoei, mmoja wa wazee hao.
Mzee Singoei alielezea kusikitishwa na tukio hilo na kuomba msamaha kutoka kwa Bw Odinga na ujumbe wake kwa niaba ya jamii ya Wakalenjin. Alisisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kutembelea eneo lolote nchini.
“Bw Odinga anaalikwa tena kuzuru eneo hili. Kama jamii tunasikitikia kile kilichomtendekea. Anakaribishwa kuendesha kampeni zake hapa jinsi alivyofanya kampeni kwa amani mjini Eldoret mapema mwaka huu 2022,” Mzee huyo akaeleza.
“Izingatiwe kuwa kama jamii tunawakaribisha wageni na hatuungi mkono aina yoyote ya fujo,” Mzee Singoei akaongeza.
Mzee mwingine kwa jina Edwin Chepsiror alitoa wito kwa polisi kuendesha uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo na kuhakikisha kuwa wote waliohusika wamechukuliwa hatua za kisheria.
“Mzee Kibor na Bw Odinga walikuwa marafiki na kiongozi wa ODM alikuwa akihudhuria mazishi kama rafiki wa mwendazake. Hakuja kwa ajili ya kuhutubia mkutano wa kisiasa. Hii ndio maana tunalaani shambulio hili na kumwomba msamaha,” akaongeza.
Next article
Kinyang’anyiro cha ugavana Kakamega kuzua kivumbi kikali