[ad_1]
CHARLES WASONGA: Uhuru aende kuvumisha Raila vijijini Mlima Kenya ikiwa anaamini ndiye!
NA CHARLES WASONGA
NI kinaya kwamba, kampeni za kumpigia debe mgombeaji wa urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga zinafifia katika eneo la Mlima Kenya wakati ambapo uchaguzi mkuu unakaribia.
Nasema ni kinaya kwa sababu, eneo hilo ni ngome ya kisiasa ya mwandani wake wa karibu, Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ameshikilia kwamba anamuunga mkono hadi debeni Agosti, 9.
Akihutubu baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika mtaa wa Pipeline, Nairobi kiongozi wa taifa alipuuzilia mbali miito ya wanasiasa wa mrengo wa Kenya Kwanza kwamba, akome kujichukulia kuwa meneja wa kampeni za Bw Odinga.
Lakini habari za kuvunja moyo kwa kambi ya Azimio la Umoja One Kenya kutoka kaunti kadhaa za Mlima Kenya ni kwamba, wawaniaji viti mbali mbali kwa tikiti ya Jubilee wamechelea kumfanyia kampeni katika maeneo yao.
Duru zasema baadhi yao hata wameondoa picha za Bw Odinga katika mabango, ishara kwamba, wanahofia kujihusisha na mgombeaji huyo wa urais.
Hii ni licha ya kwamba, chama hicho kinachoongozwa na Rais Kenyatta mwenyewe ni miongoni mwa vyama vikuu katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.
Isitoshe, kiongozi wa taifa pia ndiye mlezi wa muungano huo ambao unashirikisha zaidi ya vyama 20 vya kisiasa. Kando na kuitisha mikutano ya viongozi wa kisiasa na wazee kutoka Mlima Kenya katika Ikulu za Nairobi na Sagana, Rais Kenyatta hajawahi kuendesha msururu wa kampeni katika eneo hilo lenye zaidi ya kura 5,000,000.
Nadhani wakati umetimu ambapo Rais Kenyatta anafaa kuanzisha msururu wa mikutano ya kisiasa katika ngome yake ya Mlima Kenya ili kutoa mwelekeo kamili kwa wakazi wa huko.
[ad_2]
Source link