Viongozi wa dini wataka Uhuru, Ruto waridhiane
GEORGE MUNENE NA OSCAR KAKAI
VIONGOZI wa kidini Kaunti ya Embu jana Alhamisi walitoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais wake kuridhiana ili kupunguza taharuki iliyopo nchini.
Walionya kuwa vita vya maneno kati ya Kiongozi wa Taifa na Dkt Ruto huenda vikasambaratisha nchi.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa linalosimamia Makanisa Nchini (NCCK) Askofu Njeru Nyaga, viongozi hao walielezea wasiwasi wao kuwa tofauti kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto ambazo hivi majuzi zimezidi kujitokeza hadharani, huenda zikagawanya taifa ikiwa hazitatatuliwa kwa dharura.
“Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu ufa uliopo kati ya rais na naibu wake huku migogoro ikiibuka katika kaunti mbalimbali na taifa kwa jumla kufuatia uhusiano wao uliosambaratika,” alisema Askofu Nyaga.
Wakihutubia vyombo vya habari mjini Embu, viongozi hao wa kidini waliwasihi viongozi hao kupatana kwa ajili ya amani na umoja.
“Tunawarai viongozi hao wawili wa taifa kusuluhisha tofauti zao kwa njia ya amani na ikiwa hawawezi kufanya hivyo kivyao, wanapaswa kutafuta usaidizi kutoka kwa wazee wanaoheshimiwa ili kuendesha mazungumzo hayo ya amani,” alisema Askofu Nyaga.
Viongozi hao wa kidini walisema wawili hao wanapaswa kuweka mfano bora wa kuigwa na Wakenya kwa kuongoza na kuendeleza uongozi mwema unaozingatia maridhiano na kudumisha amani.
Kwingineko katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, viongozi wa kidini wamepiga marufuku wanasiasa dhidi ya kufanya kampeni katika makanisa na misikiti yao.
Viongozi hao wametaja hali ya kuongezeka kwa joto la kisiasa nchini kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti kama sababu ya hatua yao.
Viongozi hao chini ya Kundi la Madhehebu Mbalimbali Kaunti ya Pokot Magharibi, wamesema sasa hawatawaruhusu wanasiasa kupiga siasa makanisani na misikitini huku wakiahidi kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa njia ya amani.
Aidha, walisema kuwa taharuki ya kisiasa inayotokana na kampeni zinazoendelea zimesababisha hofu miongoni mwa umma huku wakihimiza kuwepo kwa mazungumzo na maridhiano ili kuimarisha amani miongoni mwa Wakenya.
“Uchaguzi Mkuu unapojongea, joto la kisiasa linazidi kupanda kwa njia ya kuhofisha. Migawanyiko baina ya makundi mbalimbali ya kijamii na kambi za kisiasa imezidi kuongezeka hivyo kuchochea uhasama na michafuko,” alisema Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa linalosimamia Makanisa kaunti ya Pokot Magharibi Askofu Moses Long’iro.
Akizungumza Kapenguria, Askofu Long’iro alisema wanasiasa wana haki ya kwenda kanisani kusikiza neno lakini si kupiga siasa.
“Wako huru kuja na kusikiza neno. Tunapinga kuwapa jukwaa la kuzungumzia siasa kwa sababu wanaweza kuwakera baadhi ya watu,” alisema.
Viongozi hao walisema haya siku chache tu baada ya msafara wa ndege wa mpeperushaji bendera wa Muungano wa Azimio la Umoja- One Kenya Raila Odinga kurushiwa mawe katika eneo la Kabenes, Kaunti ya Uasin Gishu Ijumaa iliyopita.