Kilio uhaba wa mafuta ukiendelea
NA MARY WANGARI
WASAFIRISHAJI bidhaa nchini wanakadiria hasara kutokana na kero la uhaba wa mafuta ambalo limegubika Kenya kwa muda wa wiki moja iliyopita huku wakiitaka serikali kutatua suala hilo kwa dharura.
Kupitia taarifa iliyofikia Taifa Leo jana, Muungano wa Wasafirishaji Bidhaa Nchini, umesema kuwa wasafirishaji bidhaa wanapoteza muda mwingi kwenye foleni wakisubiri mafuta hali inayowasababishia hasara kuu ikizingatiwa bado wanahitajika kulipia ada zao.
“Wasafirishaji wamestaajabishwa na ukosefu wa mafuta uliopo kwa sasa. Kunawezaje kuwa na mafuta ya kutosha na wakati huo vilevile uhaba wa mafuta mahali yanapohitajika. Je, kuna mipango ya kuongeza bei ya mafuta? Mafuta yanahodhiwa ili kuongeza bei katika kipindi kipya? Mbona serikali haijaweza kutatua suala hili?” alihoji Mwenyekiti wa Wasafirishaji Bidhaa Nchini, Bw Newton Wang’oo.
Alilalamika kuwa suala la uhaba wa mafuta linaongeza gharama ya uundaji bidhaa hivyo kuwasababishia hasara wahusika katika sekta nyinginezo ikiwemo mawakala na wamiliki viwanda.
“Haitoshi tu kuwahakikishia Wakenya kwamba kuna mafuta ya kutosha. Maisha ya watu yamo hatarini. Ni muhimu pia kujua nyongeza yoyote ya bei ya mafuta itasababisha kuongezeka kwa bei ya usafirishaji na msururu huu utaishia kuwa bei ghali kwa bidhaa. Tunahimiza serikali ya Kenya kwa mara nyingine kubaini kiini cha tatizo hili na kulisuluhisha kikamilifu,” alisema Bw Wang’oo.
Isitoshe, baadhi ya madereva wa masafa marefu wameelezea hofu kuhusu kuongezeka kwa ukosefu wa usalama ikiwemo uwezekano wa mkurupuko wa maradhi katika maeneo yenye misongamano ya magari hasa mipakani kutokana na uhaba wa mafuta unaokumba Kenya.
Akizungumza na Taifa Leo jana, Katibu Mkuu wa Muungano wa Madereva wa Matrela Nchini, Ahmed Omar, alifichua kuwa madereva wa matrela wasiopungua wanane, wameshambuliwa na kuuawa kwenye barabara kati ya Mai Mahiu na Mombasa tangu mwaka huu ulipoanza.
Katibu Mkuu huyo alisema kuwa, eneo lililoathirika zaidi ni kati ya Kanduyina mpaka wa Malaba ambapo madereva wanaosafirisha bidhaa wamekwama kutokana na uhaba wa mafuta unaoendelea nchini.
“Makundi ya vijana wahuni wamekuwa wakishambulia madereva na kuwaibia simu, vipuri na vifaa muhimu. Uhalifu huo huenda unatekelezwa na watu waliowahi kufanya kazi kama madereva na makondakta kwa sababu ni wao tu wanaofahamu umuhimu wa vifaa na vipuri vinavyoibwa,”alisema.
“Idadi kubwa ya madereva wa masafa marefu walipoteza kazi wakati wa janga la virusi vya corona. Tunahofia kuwa suala hili la mafuta huenda likagharimu wengine zaidi riziki yao. Tunaomba serikali na wadau husika kuingilia kati,” alisema.
Aidha, alisema kuwa madereva wa matrela wamekuwa wakihangaika kupata huduma na mahitaji ya kimsingi huku wakilazimika kupanga foleni na kusubiri kwa muda mrefu kupata mafuta ya usafiri.
“Tulikuwa tunanunua mafuta Uganda lakini bei ikapandishwa kutokana na uhaba uliopo nchini. Eneo tulilokwama tukisubiri mafuta halina makao, sehemu za kuendea haja wala chakula. Wachuuzi wanaotuuzia chakula kama vile mayai ya kuchemsha wanatuuzia kwa bei maradufu ambayo madereva wengi hawawezi kuimudu. Waajiri wao hawatumi pesa kwa sababu pia wanazidi kukadiria hasara kutokana na ucheleweshaji wa bidhaa,”alisema.
Kulingana na Naibu Katibu wa Muungano wa Madereva, Kaunti ya Mombasa, Roman Gishingi, mamia ya madereva wa matrela waliokwama katika eneo la Bonje wanalazimika kwenda haja msituni au vichaka vilivyo karibu huku wakihofia kuibiwa vipuri na vifaa muhimu.
Isitoshe, alisema kuwa madereva wengi wamegeukia mihadarati kama vile pombe na miraa baada ya kulazimika kukesha usiku na mchana wakisubiri mafuta na wakati huohuo wakihofia usalama wao.
Next article
Wanasiasa sasa watumia mzozo wa mipaka kusaka kura