Connect with us

General News

Wazee wa Kaya watakasa eneo la ujenzi wa bwawa la Mwache – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wazee wa Kaya watakasa eneo la ujenzi wa bwawa la Mwache – Taifa Leo

MAKALA MAALUM: Wazee wa Kaya watakasa eneo la ujenzi wa bwawa la Mwache

NA CECE SIAGO

HUKU ujenzi wa bwawa la Mwache, utakaogharimu Sh20 bilioni, katika eneobunge la Kinango, Kaunti ya Kwale ukianza, Wazee wa Kaya wamefanya matambiko ya kutakasa eneo hilo ambalo limekuwa takatifu kwa Waduruma na makabila mengine yanayounga jamii pana ya Mijikenda.

Mbali na kuhamishwa kwa watu, makaburi na misitu ya Kaya, maeneo hayo matakatifu kitamaduni pia yatalazimika kuhamishwa ili kutoa nafasi kwa mradi huo.

Katika kijiji cha Fulugani, mojawapo ya mabonde yenye kina kirefu zaidi ambapo Mto Mwache hupita karibu na Kaya Mtswakara, wanachama wa Kaya wanakusanyika.

Bonde hilo linahifadhi angalau vihekalu vitatu ambavyo vitahamishwa.

Hapa, kundi la wanaume na wanawake 14 kutoka kaya za Kilifi na Kwale linakaribia kutoa dhabihu ya kuridhisha miungu yao na kuwaaga.

Mwenyekiti wa Kaya Mtswakara, Shaban Ndegwa, anaongoza wengine katika wimbo na ngoma za kiasili za Kimijikenda.

Mwenyekiti wa Kaya Mtswakara, Shaban Ndegwa (kushoto), aongoza wanachama wengine kufanya maombi wakati wa matambiko ya kutakasa eneo ambalo bwawa la Mwache litajengwa. PICHA | SIAGO CECE

Anaeleza kuwa zoezi hilo ni muhimu sana kwa jamii ya Waduruma.

Shughuli hii ilifanyika katika eneo la Mwananyamala, mojawapo ya sehemu zenye umuhimu wa kimila ambapo wazazi wa watoto waliozaliwa wakiwa na mahitaji maalumu wangewarudisha kwa ‘miungu’ na kujisafisha.

Anaeleza kuwa mtu yeyote ambaye angefika eneo hilo peke yake angesikia sauti za mtoto akilia kila mara, na anapaswa kutoroka kabla “miungu pia haijamchukua.”

“Hapa ni mahali patakatifu sana. Lakini tutaiheshimu serikali kwa sababu tunajua mradi huu utakuwa wa manufaa kwetu sote, kwani utasambaza maji na pia kuruhusu wakazi kufanya kilimo cha kunyunyiza maji,” alieleza Bw Ndegwa.

Mzee huyo alifichua kuwa awali alipinga mradi huo ili kulinda imani zao za jadi, lakini mawazo yao na jamii yalibadilika walipofahamishwa kuhusu manufaa ya bwawa la Mwache.

Siku hii ya tambiko, aliongoza wenzake kuchinja ng’ombe wawili weusi, mbuzi wawili weusi, kuku mmoja mweusi na kondoo wa rangi au jinsia yoyote.

Shughuli hiyo ya kutoa dhabihu ilijumuisha uchomaji wa kondoo aliye na ngozi, kumchinja kuku katika moja ya mapango na kumwaga damu ya ng’ombe waliochinjwa kama sadaka kwenye madhabahu iliyo ndani ya miamba.

Kulingana na Bw Ndegwa, zoezi hilo ni muhimu kwani linafahamisha miungu kwamba ingehitaji kuhama maeneo hayo matakatifu.

Eneo la Mwanayamala ndipo ukuta mkubwa kukinga maji ya Mto Mwache utajengwa, hivyo miti itakatwa na miamba kuporomoshwa.

Isitoshe, alisema ibada hiyo pia ni muhimu kwa sababu mle kwenye mapango mnaishi nyoka wakubwa, na iwapo hawatahama basi wanaweza kuuawa na hiyo itakuwa laana kubwa kwa wazee.

“Pia kunaweza kutokea maafa zaidi wakati wa ujenzi, ambayo yatafanya mradi mzima kusimamishwa. Sitaki kuwajibika kwa kifo cha mtu yeyote,” Mzee Ndegwa alieleza.

Katibu wa Kaya Mtswakara, Bi Jemima Chula, alisema dhabihu hizo zitatuliza miungu.

“Lazima tuwaache wajiandae na kujua kwamba kuna mradi unakuja hapo wanapoishi,” akasema.

Zainab Kanindo pia ni mmoja wa wanachama wa Kaya ambaye pia ni mganga.

Alisema kuwa walilazimika kutumia angalau siku tatu katika msitu wa Kaya ili kujiandaa kwa msururu wa matambiko.Alifichua kwamba, siku ya kwanza alikutana na joka kubwa, lakini baadaye akazungumza nalo na ‘kushughulikia jambo hilo’.

Baada ya kondoo wa kwanza kuchinjwa na sehemu za chakula ndani ya matumbo yake kuchukuliwa, huwekwa ndani ya chungu.

Mbuzi wawili weusi na ng’ombe pia huchinjwa na damu yao kutolewa kupitia shingoni na kutiwa kwa kikombe.

Bi Kanindo aliwaongoza wazee wengine wawili wa Kaya kwenye moja ya vihekalu ambako waliingia na kumchinja kuku mweusi. Kisha walisema kwa lugha ya Kiduruma kabla kutoka nje na kuelekea kwa kaburi lingine.

Naibu Kamishna wa Kaunti, Bw Silonga Ole Masaa, alihoji kuwa serikali inatambua tamaduni tofauti na ilikuwa tayari kuwaunga mkono wazee wa Kaya kufanya matambiko yao katika eneo la Fulugani karibu na mto Mwache.

Alifichua kuwa kuna angalau maeneo 49 ya kaya ya kuhamishwa kutoa nafasi kwa mradi huo; kila moja litagharibu Sh79,000.

Madhabahu zaidi yanatarajiwa kuhamishwa katika siku zijazo ili ujenzi wa uanze bila bughudha.

Mradi wa Mwache ulizinduliwa kwanza mnamo 2016 serikali ilipopata ufadhili. Bwawa hilo linatarajiwa kusambaza maelfu ya lita za maji kwa wakazi wa Kilifi, Kwale na Mombasa litakapokamilika.

Ujenzi umecheleweshwa kuanza kutokana na suala la ulipaji fidia kwa waathiriwa.Wakazi na viongozi wa eneo hilo walikuwa wametoa hofu kwamba pesa za fidia zilikuwa kidogo sana, lakini hili limetatuliwa.

Mwenyekiti wa waathiriwa Bw Simon Kangai alisema fidia hiyo imekamilika katika awamu ya kwanza, na sehemu ndogo ya wakazi imebaki ambao hawajafidiwa.

“Takriban vijiji 40 vinanufaika na mradi huo. Licha ya kupoteza ardhi yetu, tumelipwa fidia. Fedha hizo zimesaidia wakazi wengi ambao awali hawakuwa na nyumba ila sasa wamejenga maboma yao,” akaeleza Bw Kangai.

Ujenzi wa bwawa la Mwache unatarajiwa kuchukua takriban miaka mitano na kukamilika mnamo 2027.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending