ZARAA: Wakuzaji chai wagundua siri ya kujivunia mapato
NA SAMMY WAWERU
KABLA Sheria ya Majanichai 2008 kupitishwa kuruhusu kampuni na mashirika ya kibinafsi kutafutia mazao soko, wakulima walikuwa wakihangaika.
Mamlaka ya Kilimo cha Majanichai (KTDA), ndiyo ilikuwa na idhini kusaka mianya ya soko ndani na nje ya nchi.
Reuben Tanui, mkulima katika eneo la Belgut, Kericho amekuwa akizalisha majanichai tangu 1998 na anasema haikuwa rahisi kupata soko lenye ushindani mkuu kabla sheria hiyo kupitishwa.
“Nusra nisalimu amri kwa sababu mazao yalikuwa yakiharibika yanapokawia kupelekwa kiwandani eneo la kuyakusanya,” akumbuka Mzee Tanui, anayekuza majanichai kwenye ekari mbili.
Changamoto hiyo ilitokana na sekta ya majanichai kutwaliwa na ‘mkusanyaji mmoja pekee’.
Isitoshe, bei ilikuwa duni akifichua kilo haikupita Sh10.
“Mazao yangu nyakati zingine yangesalia katika kituo cha kuyakusanya siku tatu mfululizo,” aelezea Caroline Chepkwony, anayeendeleza kilimo Kericho.
Caroline aliingilia ukuzaji wa majanichai mwaka 2000, na ana jumla ya ekari saba.Chini ya miungano tano inayosimamiwa na Fintea Growers Cooperative Union Ltd, mahangaiko ya soko miongoni mwa wakulima Kaunti ya Bomet na Kericho yamepungua.
Makundi hayo; Kokchaik Cooperative Society Ltd, Kapkap Outgrowers, Chepcheb, Chesetekaa, na Ainamoi Multipurpose, ina jumla ya wanachama 14, 966.Chama hicho cha Ushirika, Fintea Growers, kilichoasisiwa 2012, kupitia James Finlay Kenya Ltd, hutafutia wakulima soko ng’ambo.“Mbali na kuwatafutia wanunuzi ng’ambo, hunadi bei bora,” asema Afisa Mkuu Mtendaji, Nelson Ng’eno.Ni mkulima wa majanichai, na anasema walichukua hatua hiyo kufuatia kilio cha wakuzaji kukadiria hasara.
“Miungano ilitangulia kuanzishwa, kisha chama cha ushirika kikafuata kuwa daraja lao kwa Finlays,” aelezea.
Anasisitiza kwamba mradi huo unalenga kupiga jeki wakulima wa mashamba madogo na ya kadri.
Finlays ina viwanda viwili vya kusaga majanichai ya wakulima; Chomogonday kilichoko Kericho na Kymulot – Bomet.
“Hatuchanganyi chai ya wakulima na ile ya kampuni,” adokeza Nixon Mutai, Naibu Meneja kitengo cha Outgrowers, Finlays.
Kampuni hiyo ina mashamba yake.
Geoffrey Chepkwony (kushoto), Meneja Outgrowers – Finlays na Nixon Mutai, Naibu Meneja, wakivuna majanichai katika shamba la James Finlay Kenya Ltd Bomet. PICHA | SAMMY WAWERU
Chai ya wakulima huuzwa kwa nembo mbili; Masingi na Bondet, baada ya kusagwa.
Ng’eno anasema Fintea Growers imepata cheti cha Rainforest Alliance na Fairtrade, baada ya kuafikia matakwa ya kitaifa na kimataifa kuzalisha majanichai.
Finlays ina soko tayari Uingereza, nchi za Uarabuni na Pakistani.Kenya huuza zaidi ya asilimia 95 ya chai ng’ambo.
Kulingana na takwimu za Fintea Growers 2021, chama hicho kilifanya mauzo ya kilo milioni 21, majanichai mabichi.
Geoffrey Chepkwony, Meneja Outgrowers, hata hivyo anasema haijakuwa rahisi kupata mianya ya masoko.Anataja ushindani mkali miongoni mwa kampuni za kibinafsi na mashirika, kama baadhi ya changamoto.
“Sote tunang’ang’ania wakulima wale wamoja, na baadhi hutekwa na wenye bei bora zaidi,” aelezea.
Kudumisha wanachama wake, Chepkwony anasema Finlays imeibuka na mpango kutuza wale waaminifu kila mwaka.
Kando na malipo ya mwezi, huwapa bonasi kila baada ya miezi mitatu.
“Vilevile, huwasaidia kununua mbolea kwa bei nafuu,” Chepkwony asema.
Miaka 10 baadaye, miungano na chama hicho cha ushirika kinaendelea kuwapa tabasamu.
Wamekwepa kero ya mabroka.Kutoka bei duni ya Sh10 kwa kilo, sasa hulipwa Sh23.
Kwa ushirikiano na Finlays, Fintea Growers imezindua miradi ya mimea mbadala yenye thamani kwa wakulima kama vile kukuza parachichi aina ya Hass, mboga za kienyeji na pia kuwahimiza kuongeza mazao thamani.
Miradi mingine ni ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, nyuki na kuku.