Uhuru kuamua atakayegombea ugavana wa Jubilee Nyandarua
NA DAVID MWERE
RAIS Uhuru Kenyatta ndiye ataamua yule ambaye atapewa tiketi ya Jubilee kuwania ugavana wa Nyandarua.
Wakati huu, angali anajaribu kupatanisha wawaniaji wakuu wa tikiti hiyo ili kuzuia hali ambapo uamuzi wa mwisho utasababisha mgawanyiko miongoni mwa wafuasi wa Jubilee kaunti ya Nyandarua.
Lakini huku Rais Kenyatta akiendelea kufuata mkondo wa mazungumzo ili kutatua kizungumkuti hicho, aliyekuwa Waziri wa Maji Sicily Kariuki ni mwingi wa matumaini kwamba ndiye atapewa cheti kuwania wadhifa huo wa ugavana.
Naye Bw Kimemia anapania kutetea kiti hicho kwa tiketi ya chama hicho cha Jubilee.
Hata hivyo, Bi Kariuki alisema kuwa ingawa chama hicho kimechukua muda mrefu kabla ya kuamua yule atakayepeperusha bendera yake katika kinyang’anyiro cha ugavana Agosti 9, “umoja wa chama hicho ni muhimu.”
“Wafuasi wangu wanasubiri kwa hamu kubwa kule mashinani. Hii ndio maana juzi walifanya maandamano ya amani katika kaunti ya Nyandarua wakitaka chama kikamilishe suala hilo haraka,” akasema.
“Lakini nimewashauri wafuasi wangu kukoma kufuatia mkondo huo kwa sababu nani watakuwa wakiandamana dhidi yake?” akauliza.
Bw Kimemia hakujibu simu za Taifa Leo tulipomfikia.
Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema tayari uamuzi kuhusu suala hilo umefanywa na utatangazwa “wakati ufaao”.
Tayari chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu Rais William Ruto kimemteua Dkt Moses Kiarie ambaye atakabiliana na yule ambaye atateuliwa na Jubilee.
Kwa upande mwingine, chama cha The Service Party (TSP) kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, kimemteua aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo Waithaka Mwangi.
Bi Kariuki pia alisema kuwa Jubilee ilifanya uamuzi bora kwa kukumbatia maelewano kama njia bora ya kuteua mpeperushaji wa bendera yake katika kinyang’anyiro cha ugavana.
Alisema kuwa shughuli hiyo ingekumbwa na udanganyifu mwingi ikiwa ungeendeshwa kwa upigaji wa kura ya moja kwa moja na wanachama wa Jubilee.
“Kimsingi, kura ya mchujo huo ni ghali na husababisha migawanyiko. Kwa hivyo, mbinu ya maelewano iliyofuatwa na Jubilee kuteua wagombeaji wake ilifaa zaidi,” Bi Kariuki akasema.
Mnamo Jumatatu wiki jana, azma ya Bi Kariuki ilipigwa jeki baada ya wanachama 150 wa baraza la wazee la Kiama kutangaza kumuunga mkono.
Tangazo hilo lilitolewa katika mkutano wa wanachama wa baraza hilo katika eneo la Murungaru, Kinangop.
Baada ya hapa Bi Kariuki alipata uungwaji mkono kutoka kwa makanisa kadhaa katika kaunti ya Nyandarua mnamo Jumamosi Aprili 16.
“Bila shaka unafahamu maana ya usemi wa wazee na makanisa,” akasema Waziri huyo wa zamani wa maji.
Bi Kariuki alikana madai kuwa alizua kasheshe katika makao makuu ya Jubilee Ijumaa iliyopita kuvuruga shughuli ya kumpokeza Gavana Kimemia cheti cha uteuzi.
Wakati huo, Katibu Mkuu Bw Kioni alikuwa akitoa vyeti kwa wawaniaji mbalimbali walioteuliwa kupitia maelewano.