MAELFU YA WAKAZI wa Othaya, Kaunti ya Nyeri, Jumamosi walijitokeza kwa wingi kumuaga mbunge wao wa zamani, na rais wa tatu wa Kenya, Mwai Kibaki aliyezikwa nyumbani kwake kijijini Kanyange kwa heshima za kijeshi.
Safari yake ya mwisho ilianza katika hifadhi ya maiti ya Lee, Nairobi, ambako maiti yake ilipakiwa katika gari maalum kwa ajili ya kusafirishwa hadi Othaya, Nyeri, kuanzia saa moja asubuhi.
Gari hilo ambalo lilisindikizwa na wanajeshi lilipita katika kaunti za Kiambu, Murang’a, Kirinyaga na hatimaye Nyeri.
Wananchi walisimama kando ya barabara katika vituo na miji mbalimbali katika kaunti hizo kumpa mkono wa buriani rais huyo anayesifiwa kwa kutekeleza sera bora za maendeleo nchini.
Mwili wa Kibaki ulipokuwa ukisafirishwa, waombolezaji kutoka pembe zote za nchi waliwasili kwa wingi katika uwanja wa shule ya Othaya Approved ambako ibada ya mazishi iliendeshwa.
Waombolezaji kutoka Othaya na maeneo mengine ya karibu walianza kumiminika katika uwanja huo kuanzia saa 10 alfajiri.
Lakini kabla ya kuingia katika uwanja wa taasisi hiyo, waomboleza walikaguliwa na maafisa wa GSU ambao walitumia vifaa maalum vya kutambua vyuma.
Vijana wa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) pia walitumika kudhibiti wageni kwenye foleni na kuwaelekeza pa kuketi kwenye mahema yaliyosimikwa katika uwanja huo wa Shule ya Othaya Approved.
Wageni mashuhuri wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta walianza kuwasili Othaya kwa ndege za helikopta mwendo wa nne asubuhi.
Rais Mstaafu Emilio Mwai Kibaki alizikwa nyumbani kwake Munyange, viungani mwa mji wa Othaya, Kaunti ya Nyeri, Jumamosi, Aprili 30, 2022. PICHA | PSCU
Uwanja wa Shule ya Upili ya Wavula ya Othaya katika kijiji cha Gatuayaini uligeuzwa kuwa uwanja mdogo wa ndege uliojaa helikopa.
Wengine ambao helikopta zao zilitua katika uwanja wa shule hiyo ni Naibu Rais William Ruto na waziri mkuu wa zamani Raila Odinga.
Miongoni mwa wale ambao walikuwa wamewasili kufikia saa nne za asubuhi ni Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, Spika wa Seneti Kenneth Lusaka, magavana Mutahi Kahiga (Nyeri), Anne Waiguru (Kirinyaga), Peter Anyang Nyong’o (Kisumu), James Nyoro (Kiambu), Lee Kinyanjui (Nakuru), Mwangi wa Iria (Murang’a) miongoni mwa wengine.
Pia walikuwepo mawaziri na viongozi wengine mashuhuri kama vile kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Martha Karua (Narc Kenya), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya).
Mwili wa Hayati Kibaki uliwasilishwa karibu na shule ya Othaya Approved saa tano na dakika 11 na kupokelewa kwa heshima na taadhima kuu na wanajeshi wa vyeo vya juu.
Uliwekwa katika gari maalum la kubeba mizinga na kusindikizwa kwa gwaride la wanajeshi hao wakioongozwa na viongozi wa kidini kuelekea katika uwanja wa taasisi hiyo kwa ajili ya ibada maalum ya mazishi.
Ibada hiyo iliongozwa na Askofu wa Kanisa Katoliki, jimbo la Nyeri, Anthony Muheria akisaidiana na viongozi wengine wa kidini wapatao 50.
Askofu Muheria alirejelea ombi alilotoa wakati wa Ibada ya wafu iliyofanyika uwanja wa Nyayo, Nairobi, kwa wanasiasa kwamba wakome kutoa kauli za siasa.
“Familia ya Rais wetu Mwai Kibaki imeomba kwamba wale watakaopewa nafasi kuhutubu wakome kutoa matamshi ya kisiasa. Ombi hilo linaambatana na mapenzi ya kiongozi huyo ambaye tunamsindikiza,” akasema.
Ibada hiyo iliyochukua karibu saa moja na nusu ilifuatwa na kipindi cha watu kutoa kumbukumbu za maisha ya Hayati Kibaki.
Nafasi ya kwanza iliendea familia ya Hayati Kibaki ikiongozwa na watoto wake.
Wa kwanza kuzungumza alikuwa bintiye mkubwa Judy Wanjiku na kufuatwa na kakaye Jimmy Kibaki.
Wengine waliotoa kumbukumbu zao ni mpwa wake Hayati Kibaki, Gavana wa Laikipia, Ndiritu Muriithi, Balozi wa zamani Solomon Karanja na aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Muthaura.
Ibada ya mazishi ilikamilika saa kumi na dakika 13 na kupisha usafirishaji wa mwili kwa mazishi katika boma lake kijijini Kanyage, umbali wa kilomita tatu kutoka shule hiyo.
Ni viongozi wachache walioruhusiwa kufika mahala hapo kwa mazishi ambayo yaliongozwa na wanajeshi.
Wanajeshi hao walifyatua mizinga 19 angani kama ishara ya heshima kwa Hayati Kibaki ambaye alikuwa Amiri Jeshi Mkuu kati ya 2002 hadi 2013.