Jamii yataka kuweka mikataba na wanasiasa kuhusu ahadi
NA KALUME KAZUNGU
BAADA YA MIAKA mingi ya kuhadaiwa na wanasiasa kila wakati wa uchaguzi, jamii moja katika Kaunti ya Lamu sasa imeamua kulazimisha wawaniaji kuweka mikataba rasmi kuhusu ahadi wanazotoa.
Jamii ya Waboni Lamu imezinduka na mbinu mpya ya kuwataka wawaniaji wa viti malimbali vya kisiasa eneo hilo kutia sahihi mkataba wa maelewano (MoU) kama njia mojawapo ya kuhakikisha hawaendi kinyume na ahadi zao.
Hatua hiyo inajiri kufuatia malalamishi kuwa wanasiasa eneo hilo mara nyingi wamekuwa wakiwaendea kuomba kura na punde wanapopata viti wanatoroka wasionekane tena.
Jamii hiyo ndogo huishi kwenye vijiji vinavyopakana na msitu mkuu wa Boni, ikiwemo Bar’goni, Milimani, Basuba, Mangai, Mararani, Kiangwe, Madina, Bodhei-Junction na Pandanguo.
Katika mahojiano na Taifa Leo, wawakilishi wao walisema lazima wawaniaji wanaotafuta nyadhifa kama ile ya ugavana, useneta, ubunge, Mwakilishi wa Kike, kukubali matakwa ya kutia saini MoU kati yao la sivyo wasizingatiwe kupigiwa kura.
Kulingana na jamii hiyo, madiwani mara nyingi ndio wamejaribu kuhudumia vyema Waboni kila wanapochaguliwa ilhali viongozi wa nyadfha za juu wakijitia hamnazo.
“Tumeafikia maamuzi ya MoU na wanasiasa. Ukitaka kura yetu kama jamii, lazima ukubali matakwa ya sahihi. Tumechoka kuchukuliwa kama daraja la kuvukisha watu kisha tunakosa kuthaminiwa baadaye na watu hao hao tunaovukisha,” akasema Khamis Guyo ambaye ni mzee wa jamii hiyo.
Kwa upande wake, Bw Sharuti Ali alieleza kutoridhishwa na hulka ya viongozi ambao huonekana vijijini mwao wakati uchaguzi mkuu unapowadia pekee.
Bw Ali alisema haipendezi kwamba katika karne hii, jamii ya Waboni bado inaishi kifukara bila maendeleo yoyote.
“Waboni hawana shule, hospitali, barabara, maji na miundomsingi mingine bora licha ya kwamba tuko na viongozi bungeni. Hili ni dhihirisho tosha kwamba viongozi wetu hawatujali. MoU pekee ndiyo kiokozi cha Waboni kutambuliwa na kuzingatiwa,” akasema Bw Sharuti.
Bi Asha Ali, mkazi wa Mararani alisema kipindi chote cha miaka mitano ya uongozi, wanasiasa kama vile gavana, seneta, mwakilishi wa kike na mbunge wao bado hawajatia guu kijijini kwao licha ya jamii hiyo kujitolea kuwapigia kura na kuhakikisha wameshinda uchaguzi mkuu wa 2017.
“Kigezo kimekuwa utovu wa usalama. Kwani sisi tunaoishi huku ni wanyama? Cha kustaajabisha ni kuwa huu ni msimu wa siasa, najua tutawaona hao viongozi huku. Tunasubiri kujua uongo mwingine watakaotuambia,” akasema Bi Ali.