Connect with us

General News

Huwezi ukang’olewa huku ukawania kule, DPP Haji amwambia Sonko – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Huwezi ukang’olewa huku ukawania kule, DPP Haji amwambia Sonko – Taifa Leo

Huwezi ukang’olewa huku ukawania kule, DPP Haji amwambia Sonko

NA CHARLES WASONGA

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) amesisitiza kwamba atamzuia aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko kuwania kiti cha ugavana Mombasa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Akiongea katika redio ya Spice FM Alhamisi asubuhi Bw Haji alisema kuwa gavana ambaye ameondolewa mamlakani hafai kushikilia afisi ya umma na hivyo hawezi kupigania kiti cha ugavana, hata katika kaunti tofauti.

“Kwa maoni yangu ikiwa umeondolewa mamlaka kama gavana wa Nairobi, huwezi kuwania kiti hicho katika kaunti nyingine ambayo iko ndani ya Jamhuri ya Kenya. Kwa hivyo, huwezi kuruka kutoka kaunti moja hadi nyingine eti unataka kuwania kiti cha ugavana. Afisi yangu itapinga hilo,” Bw Haji akasema.

Mnamo Aprili 21, 2022 Bw Sonko aliteuliwa rasmi na chama cha Wiper na kupewa cheti cha kuwania ugavana wa Mombasa katika uchaguzi mkuu ujao.

Alipokezwa cheti na Kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka ambaye pia alitangaza kuwa mgombea mwenza wa Sonko atakuwa Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo.

Sonko aliondolewa mamlakani mnamo Desemba 2020 na madiwani wa Bunge la Kaunti ya Nairobi kwa makosa ya kuvunja Katiba, kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake, mienendo mibaya na uhalifu kinyume cha sheria za kitaifa.

Majaribio mawili ya Bw Sonko kutaka hatua hiyo ibatilishwe na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa yaligonga mwamba baada ya majaji wa mahakama hizo kuamua kuwa aliondolewa mamlakani kwa njia halali.

Amejaribu kukata rufaa katika Mahakama ya Juu lakini kufikia sasa stakabadhi zake hazijakubalika.

Hii ina maana kuwa Mahakama hiyo yenye majaji saba chini ya uongozi wa Jaji Mkuu Martha Koome, haijaweka kando uamuzi wa Mahakama ya Rufaa iliyohalalisha kufurushwa afisini kwa Bw Sonko.

Akiongea katika mahojiano na runinga ya Citizen Jumanne asubuhi, Kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Abdi Guliye alisema kuwa tume hiyo haitamzuia mgombeaji yeyote ambaye ana kesi mahakamani.

“Ikiwa mtu amakata rufaa katika kesi yoyote dhidi yake, basi IEBC itamwidhinisha mwanasiasa kama huyo kuwania kiti chochote anachotaka. Miongoni mwao ni magavana ambao waliondolewa mamlakani,” Bw Guliye akasema.

“Lakini iwapo hakuna rufaa yoyote ambayo mwaniaji aliwasilisha katika mahakama ya juu, basi gavana aliyeondolewa mamlakani hataruhusiwa kuwania kiti chochote cha umma,” kamishna huyo akasema.

Hata hivyo, Bw Sonko ameshikilia kuwa hafai kuzuiliwa kuwania ugavana wa Mombasa kwa sababu hajapatikana na hatia kuhusiana na tuhuma za ufisadi alizoelekezewa.

“Hizo kesi za ufisadi zingali mahakamani na sijapatikana na hatia yoyote. Na hatia haitapatikana kwa sababu naamini kuwa kesi dhidi yangu ilichochewa kisiasa,” akasema mwezi Aprili.

Mnamo Februari 2022 Amerika ilimpiga marufuku Sonko na watu wa familia yake kutia guu nchini humo kutokana na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka pia amemtetea Sonko akisema kuwa mwanasiasa huyo hajapatikana na hatia yoyote ya ufisadi na hivyo hafai kuzuiwa kuwania ugavana wa Mombasa.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Trending