[ad_1]
AFC Leopards kusajili wanne mwezi huu
NA JOHN ASHIHUNDU
AFC Leopards wamepanga kutumia muhula huu wa usajili kupata wachezaji wanne kuongezea kikosi hicho nguvu.
Akizungmza na waandishi wa habari za michezo baada ya timu hiyo kucheza na Nzoia Sugar mnamo Jumapili iliyopita, kocha Patrick Aussems alisema tayari ameifahamisha afisi kuu ya klabu hiyo aina ya wachezaji anaotaka.
Aussems alisema anahitaji washambuliaji wawili, kiungo mmoja na mlinzi mmoja anayeweza kucheza sehemu tofauti kwenye safu ya ulinzi.
Leopards ambao watakuwa ugani Kasarani kucheza na Kariobangi Sharks wamecheza mechi sita mfululizo bila kushindwa lakini wamebakia nje ya kumi bora kufikia sasa.
“Iwapo wana uwezo wa kifedha, ni bora wasajili hata zaidi ya wanne ili kuongezea kikosi kizima nguvu,” aliongeza kocha huyo.
“Tumekuwa tukicheza vizuri kuanza nyuma, lakini tunalegea kila tunapokaribi safu ya ushambuliaji. Kwa sasa hatuna ruhusa ya kusajili wachezaji wa kigeni hadi afisi mpya itakapochaguliwa kutwaa uongozi wa FKF,” aliongeza raia huyo wa Ubelgiji.
Kutokana na hali hii, huenda Ingwe ikalazimika kusajili kutoka kituo chake cha akademia, ilikotoa watatu wakati wa dirisha la uhamiaji lililopita.
[ad_2]
Source link