Connect with us

General News

Alianza kukuza nyasi kupiga jeki ufugaji wake, sasa zimegeuka biashara – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Alianza kukuza nyasi kupiga jeki ufugaji wake, sasa zimegeuka biashara – Taifa Leo

Alianza kukuza nyasi kupiga jeki ufugaji wake, sasa zimegeuka biashara

Na PETER CHANGTOEK

WAKULIMA wengi ambao hufuga mifugo, wamekuwa wakipitia changamoto ya ukosefu wa lishe, hususan katika nyakati za kiangazi.

Nicholas Kibet ni mmoja kati ya wakulima wanaofuga ng’ombe wa maziwa, na changamoto ya ukosefu wa lishe na bei ghali ya lishe za mifugo, ndiyo iliyomsukuma kuanza kuzikuza nyasi za kulisha ng’ombe wake.

“Mimi huendeleza ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, na niligundua kuwa, kununua nyasi aina ya hay hugharimu pesa nyingi. Hivyo basi, nikaamua kutumia fursa hiyo kukuza zangu, kwa sababu zilikuwa ghali sana kuzinunua kutoka kwa maduka ya kuuza bidhaa za kilimo,” aeleza Kibet, mwenye umri wa miaka 30.

Hata hivyo, baada ya kugundua kuwa nyasi hizo zina faida, akaamua kuigeuza shughuli hiyo kuwa njia ya kujipatia riziki. Alianza kufanya shughuli hiyo ya ukuzaji na uuzaji wa nyasi mnamo mwaka 2019, na imekuwa biashara ya kufana kwake.

Kibet, ambaye ana stashahada katika kozi ya Usimamizi wa Miradi, huendeleza shughuli hiyo katika Kaunti ya Nandi, ambapo kwa sasa, hulitumia shamba ekari mbili kuzikuza nyasi aina ya Boma Rhodes.

“Mimi hutumia shamba ekari mbili, lakini nina mipango ya kukodi shamba jingine ili kuwa na nyasi nyingi,” asema mkulima huyo, ambaye ni baba wa watoto watatu.

Anadokeza kwamba, huzinunua mbegu za nyasi hizo kutoka kwa kampuni ya mbegu ya Kenya Seed, kwa bei ya Sh1,200.

Anaongeza kuwa, nyasi hizo huchukua muda wa miezi mitatu ili kukomaa, baada ya kupandwa huku akitumia Sh20,000 kulikodi shamba analolitumia. Aidha, baada ya kulikodi shamba, hutumia Sh4,000 kulitayarisha, na Sh24,000 kuzinunua mbegu.

Baada ya kuzipanda mbegu hizo, huzinunua mbolea ambazo hutumika kunawirisha nyasi hizo zinapoendelea kukua. Mbolea hizo humgharimu Sh6,000. Isitoshe, yeye hutumia Sh2,000 kufanya shughuli ya kuondoa magugu yanayoota shambani.

Mkulima huyo hukodi mashine wakati wa kuvuna nyasi hizo. Wakati wa kuvuna, trekta linaloivuta mashine ya kuzifunga nyasi, huhitajika.

Kibet hulipa Sh60 kwa kila robota la nyasi, ambapo hulipa jumla ya Sh30,000 kwa shamba ekari mbili, kwa sababu yeye huvuna morobota 500 ya nyasi kwa wakati mmoja.

Yeye huuza robota moja la nyasi kwa Sh250, ambapo hutia kibindoni Sh125,000 kwa jumla, kwa shamba ekari mbili.

Yeye huvuna nyasi hizo mara tatu kwa mwaka, na huwapata wateja kutoka kwa mitandao ya kijamii na wengine wasiotumia mitandao ya kijamii.

Miongoni mwa changamoto anazopitia ni kupata mashine za kuvuna nyasi.

Aidha, ni vigumu kuvuna nyasi kunapokuwa na mvua kubwa.

Mkulima huyo anasema kuwa, biashara hiyo ya ukuzaji na uuzaji wa nyasi ina faida, kwa sababu haihitaji nguvukazi nyingi au utunzaji mwingi wa nyasi, ikilinganishwa na mimea mingineyo.

Kwa mujibu wa Kibet, ni kuwa, ukuzaji wa nyasi ni muhimu, hususan kwa wale wanaowafuga ng’ombe wa maziwa, kwa kuwa, huwasaidia wakulima hao kupunguza gharama ya uzalishaji.

Mbali na ukuzaji na uuzaji wa nyasi, mkulima huyo pia, hujishughulisha na shughuli ya ufugaji wa kuku wa kienyeji, ng’ombe wa maziwa na ukuzaji wa mboga za kienyeji.

“Ninapanga kupanua shamba na kununua mashine yangu ya kuvuna na kufunga nyasi,” asema mkulima huyo, akiongeza kwamba, anapania pia kuanza kuzikuza aina tofauti tofauti za nyasi.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending