Connect with us

General News

Aliyesingiziwa akafungwa maisha asherehekea ushindi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Aliyesingiziwa akafungwa maisha asherehekea ushindi – Taifa Leo

MAKALA MAALUM: Aliyesingiziwa akafungwa maisha asherehekea ushindi

NA KENYA NEWS AGENCY

ASUBUHI MOJA YENYE kijibaridi mnamo Ijumaa, Machi 2021, Juma Nyasi alisimama huku akitetemeka na misuli yake kufa ganzi ndani ya kizimba kidogo kilichojengwa kwa mawe katika mahakama ya Voi.

Mita chache kutoka kwake, hakimu mwenye sura isiyo na mzaha alisoma hukumu ya ‘jinamizi’ la kesi iliyokuwa imemhangaisha kwa zaidi ya miaka miwili.

Kesi hiyo ilikuwa imevutia umma kwa wingi. Mahakama ilikuwa imefurika huku hewa ikivuma kwa matumaini na kimya kikuu.

Kwake Nyasi, kila neno la hakimu lilimzizima kama vidonge vya barafu moyoni mwake na kupenyeza hadi ubongoni mwake kama mishale yenye makali.

Hatimaye, Nyasi aliyekumbwa na mshtuko hangeweza hata kusimama kwa miguu yake.

“Kwa wakati huo, nilikuwa shahidi wa kuona maisha yangu yote yakisimama,” anakumbuka.

Sauti yake ya chini inaashiria mshangao na hali ya kustaajabu. Kwenye mshangao kuna hisia ya kutoamini kwa mwanamme aliyerejea kutoka kwenye ukingo wa kuangamia kabisa.

Kisa cha mwanamme huyu mwenye umri wa miaka 28 ni kielelezo tosha kwa jamii kuhusu jinsi mifumo ya haki inayodhibitiwa kibinafsi nchini Kenya inavyoweza kuwa katili kwa wanaovunja sheria na wakati huohuo kuwa yenye manufaa kwa wasio na hatia.

Baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha katika Gereza Kuu la kutisha la Manyani na mahakama ya chini, Nyasi ambaye ilikuwa mara yake ya kwanza kushtakiwa kwa kosa la uhalifu na ambaye hana kisomo wala maarifa yoyote kisheria, alikata rufaa katika Mahakama Kuu iliyomwachilia huru.

“Mara tu rufaa yangu ilipokubaliwa, ilirejesha imani yangu kwa mfumo wa haki,” alisema.

Ziara yake hadi ‘jehanamu’ ilianza mnamo Juni 2019.

Ilijitokeza kama mgogoro mdogo wa kinyumbani majuma mawili baada ya Nyasi kurejea nyumbani kwao katika kijiji cha Kale, Marungu, Voi akitoka katika biasha ra yake mjini Malindi.

Ugomvi kuhusu mbuzi aliyerandaranda asipohitajika uligeuka matusi na kuzabana makofi.

“Nilipandwa na mori wakati shemeji yangu alipomtukana mama yangu. Hapo ndipo masaibu yangu yalipoanzia,” anakiri.

Wiki moja baadaye, alihitajika kufika mbele ya chifu kabla ya suala hilo kuzidi na kutua katika Kituo cha Polisi cha Voi.

Muda wote huo, Nyasi alijua mashaka yaliyokuwa yakimwandama yalihusu kisa cha kupigana.

Alipofiikishwa kortini asubuhi iliyofuatia ndipo uhalisia ulipomshtua.

Kosa lake lilikuwa moja kati ya hatia mbaya zaidi katika sheria: kunajisi.

Alishtakiwa kwa kumnajisi mpwa wake mwenye umri wa miaka mitatu; hatia anayosisitiza hakuwahi kutekeleza.

Huku akiwa amepigwa na butwaa, alikanusha mashtaka.

Alitupwa kwenye rumande baada ya kushindwa kulipa dhamana ya Sh300,000.

“Niliwekwa rumande kwa karibu miaka miwili. Hukumu ilipotolewa, korti ilisema nilipatikana na hatia ya mashtaka niliyoshtakiwa dhidi yake,” anasimulia.

Akishikilia ukweli wake, Nyasi analaumu masaibu yake anayosema yalitokana na ugomvi wa kila mara na mke wa kaka yake.

Anasema alisingiziwa kutokana na mgogoro wa kifamilia.

Baada ya uamuzi wa korti, alihamishwa kutoka Gereza Kuu la Voi GK hadi katika jela ya kutisha ya Manyani ambayo ni makao kwa wahalifu sugu wanaotumikia vifungo vya maisha.

Roho ya kupigania maisha yake ilishika kasi.

Huku akifahamu vyema huenda ikawa kazi bure, Nyasi alikata rufaa katika Mahakama Kuu mnamo Aprili 2021.

Wafungwa wenzake walimsaidia kuandika rufaa ya kupinga hukumu dhidi yake.

Rufaa hiyo ilikubaliwa mnamo Juni 2021 na kumpa mfungwa huyo aliyesononeka fursa ya kuonja haki na uhuru.

“Ombi langu lilikuwa tu kwa korti kutazama misingi niliyokuwa nimeshtakiwa,” anasema.

Hukumu yake ilitokana na misingi miwili: madai ya ute uliokauka kwenye sehemu inayozingira njia ya kupitishia choo ya mhasiriwa yaliyotiliwa mkazo na ripoti ya matibabu kutoka kwa daktari wa Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MCRH) ambapo mhasiriwa alikaguliwa.

Nyasi anadai kuwa ushahidi huo uliundwa ili kumnasa.

Anautaja kama njama mbovu zilizoshindwa na mfumo wa haki.

“Sikuwahi kamwe kutekeleza maovu niliyoshtakiwa kuhusu. Uongo ulinirusha jela,”anaeleza.

Wakati mchakato wa rufaa uliposhika kasi, alijisajili kwa Mtihani wa Kitaifa wa Shule ya Msingi (KCPE).

Alikatiza masomo katika Shule ya Sekondari ya Marungu akiwa Kidato cha Pili kutokana na ukosefu wa karo mnamo 2012 ambapo alihisi kujiunga na elimu ya ngumbaro ingempa kitu cha kufanya ikiwemo fursa ya kupata elimu ya msingi.

“Ikiwa nilipaswa kuishi maisha yangu yote gerezani, bado nilihitaji kujiendeleza kielimu. Nilitaka kuwa mtu bora kadri ya uwezo wangu,” anasema.

Matokeo yalipotangazwa, Nyasi aliibuka mtahiniwa bora wa KCPE katika magereza eneo hilo akijitwalia alama 401.

Alipokuwa akisherehekea ushindi wake, hakuwa na habari kuwa ushindi mkuu zaidi ulikuwa ukijongea.

Mnamo Aprili 2022, Jaji John Mativo katika Mahakama Kuu ya Voi alitupilia mbali hukumu iliyotolewa dhidi yake pamoja na mashtaka.

Jaji huyo alieleza kuwa upande wa mashtaka ulitegemea nakala ya mashtaka yenye walakini akisema hakukuwa na ushahidi thabiti uliomhusisha mshtakiwa na hatia iliyotekelezwa.

Siku iliyofuata, Nyasi, ambaye sasa ana umri wa miaka 28, alitoka kwenye malango ya Manyani, akiwa mwanamume huru.

“Kila kitu kilionekana kipya kabisa. Nilikuwa nimetia fora katika mtihani wangu wa KCPE na nilikuwa mwanamume huru. Maisha yalikuwa yananipa nafasi nyingine mpya,” anaeleza kwa tabasamu.

Nyasi anaapa kwamba aliacha kuwa na machungu kuhusu yaliyompata. Shauku yake tu ni kusafisha jina lake lililotiwa doa.

“Nimeanza safari ya kutoshea kikamilifu katika jamii na kuvutia tena imani waliyokuwa nayo kwangu. Ninataka sifa yangu itakaswe. Ninapanga kufanya mambo mazuri zaidi nikiwa hapa nje,” anasema.

Anakiri kwamba alijawa na ghadhabu na ari ya kulipiza kisasi katika miezi michache ya kwanza baada ya kufungwa jela.

Hata hivyo, alijifunza kusamehe baada ya kukutana na mshauri wake wa nasaha ya kiroho Pasta Shadrack Mwakazi, ambaye pia ni pasta mshiriki katika Kanisa la City of Grace.

Mchungaji huyo alimshauri kuacha hasira na kumwelekeza katika mpango maalum kwa jina “Life Sentence Discipleship”.

“Biblia ilinisaidia nisishikwe na kichaa. Ilinifunza kwmaba kila kitu hutendeka kwa sababu na nimemsamehe kila mtu. Sihisi hasira tena,” anasema.

Mipango ya kwanza ya Nyasi ni kuunda uhusiano wa karibu na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu aliyekuwa na miezi mitatu pekee babake aliporushwa rumande.

Aidha, ametoa wito kwa wahisani kufadhili elimu yake ya sekondari.

“Nitakuwa na muda na mwanagu aliyekuwa mtoto nilipofungwa jela. Ninaomba vilevile kupata mfadhili atakayenipeleka shule ya sekondari,” anasema.

Anatazama masaibu yake kama mwanzo wa safari mpya na fursa ya kuandika tena historia yake.

“Kilichotendeka hakiwezi kubadilishwa. Siwezi kurejesha muda niliopoteza lakini ninaweza kusonga mbele nikiwa na furaha kwamba nimeondolewa mashtaka. Ukakamavu wangu, subira na zaidi kuwa bila na hatia ulinyakua ushindi,” anasema.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Trending