Aliyetoweka kwake 1973 apatikana Lamu
NA KALUME KAZUNGU
MZEE aliyetoweka nyumbani kwake kijiji cha Kagio-Kiamaciri, Kaunti ya Kirinyaga miaka 49 iliyopita, amepatikana Lamu akiwa hai.
Bw Wilson Numbi Miato, 83, aliripotiwa kuondoka nyumbani bila kuaga mtu yeyote mwaka 1973, akiwa na umri wa miaka 34. Tangu hapo, alikuwa hajaonekana wala kuwasiliana na familia yake.
Mzee huyo ambaye ni mume wa wake wawili, Mary Wamulango Numbi na Milka Numbi, alikuwa tayari amezaa watoto 10 ambao wote walikuwa na umri mdogo wakati alitoweka.
Binti yake, Bi Pauline Wamwirua Mambo, ambaye alikuwa na umri wa miaka mitano pekee wakati huo, ndiye amekuwa akiendeleza harakati za kumsaka alipo baba yao.
Bi Mambo sasa ana umri wa miaka 54, akiwa mama wa watoto wawili na wajukuu wanne.
Safari ya kumtafuta babake ilifua dafu juma hili alipofaulu kumpata akitibiwa kwenye hospitali ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu, takriban kilomita 690 kutoka Kirinyaga.
Ilibainika kuwa, Bw Numbi alikuwa ameenda kutibiwa hapo juma moja lililopita lakini akalazimika kulazwa kwani hali yake ya kiafya haikuwa nzuri.
Bi Mambo jana Jumanne hakuficha furaha yake kwa kufaulu kuonana na babake mzazi baada ya karibu miongo mitano.
Kulingana naye, alipata habari za alipo babake kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.
Alieleza kuwa, harakati za kumtafuta mzazi wake zilianza zaidi ya miaka 10 iliyopita kwani kutoweka kwake kumekuwa kukimtatiza kiakili.
Licha ya baadhi ya jamaa zake kukejeli uamuzi wake wa kumtafuta baba, Bi Mambo anasema hakufa moyo kwani alikuwa na imani kwamba ipo siku angempata babake.
“Mwaka 2011, nilifunga safari kutoka Kirinyaga hadi Bura, Kaunti ya Tana River kumtafuta babangu baada ya uvumi kuenea kuwa alikuwa ameonekana kule. Nilipiga kambi Bura wiki moja nikimtafuta babangu bila mafanikio. Kabla ya kurudi Kirinyaga, niliamua pia kutembelea vituo vya kutunza wazee Mombasa na Nairobi kujaribu iwapo ningempata babangu lakini wapi,” akaeleza Bi Mambo.
Anasema ilifikia mahali ambapo alimuomba Mungu kumsaidia kumpata babake kabla afe au hata iwapo angeaga dunia kabla amuone, basi Mungu amsaidie kugundua lilipo kaburi lake.
“Baada ya kuomba niliweka anwani zangu kwa mtandao ili watakaomuona wanijulishe. Nashukuru kwamba juma lililopita mmoja wa madaktari hapa aliweka kitambulisho na picha za babangu kwa mtandao kutangaza kwamba kuna mzee ambaye anatafuta jamaa zake. Nilishukuru Mola kwa kujibu maombi yangu kwani nilipoangalia picha na kitambulisho nikapata kweli ni babangu. Nimefika Lamu na nimemuona mzazi wangu akiwa hai, japo bado yuko hospitalini,” akasema Bi Mambo.
Kilichosalia kwa sasa ni Bi Mambo kumsafirisha babake kutoka Lamu hadi Kirinyaga ili kumkutanisha na familia yake kwa mara nyingine.
Bw Paul Murimi, 52, ambaye ni kitindamimba wa Mzee Numbi naye hakuficha furaha yake kwa kufika Lamu na kumuona babake akiwa hai.
Bw Murimi ni kiongozi wa kanisa la PEFA la Gitathi-ini lililoko Kaunti ya Nyeri na aliachwa na mzee Numbi akiwa na umri wa miaka mitatu pekee.
Anasema punde alipopokea taarifa za kupatikana kwa babake, aliacha vyote na kufunga safari ya karibu saa 12 kuja Lamu kumuona mzazi huyo kwa mara ya kwanza.
Alikiri kwamba alikuwa na kinyongo cha miaka mingi dhidi ya hatua ya babake kuhama nyumbani na kuwaacha kuhangaika, lakini akamsamehe punde alipomuona hospitalini Mpeketoni.
“Kwa sasa mimi ni mwanamume mwenye furaha. Angalau nahisi joto la babangu kwa mara ya kwanza. Nimemsamehe yote na tayari nimeanza kujenga uhusiano mwema naye. Niko Mpeketoni kuhudumia babangu hadi apone kabla ya kushirikiana na dadangu Pauline kumrudisha nyumbani Kirinyaga,” akasema Bw Murimi.
Bi Pauline na Bw Murimi aidha wanajukumu kubwa la kuwarai wanafamilia wengine kumkubali tena baba yao arudi nyumbani.
Wawili hao hata hivyo wako na ombi kwa wahisani kuwasaidia kumjengea baba yao mahali pa kuishi atakaporudishwa Kirinyaga, wakisema kuwa tayari ardhi ipo ya kumjengea mzee huyo.
Mwanasaikolojia wa hospitali ya Mpeketoni, Andrew Masama, alisema mbali na afya ya mzee kudhoofika kutokana na ukosefu wa lishe ya kutosha, pia ana tatizo la kusahausahau kutokana na umri wake uliosonga.
Aliwaomba viongozi wa kijamii na wale wa kidini kaunti ya Kirinyaga, utawala wa eneo hilo na wanasaikolojia kuisaidia familia kumkubali mzee Numbi arudi nyumani.
“Nafurahi kwamba tayari wamemsamehe baba yao na wako tayari kumrudisha nyumbani. Ningeomba jamaa zao wengine kuondoa hasira, kinyongo na chuki zote na badala yake wamruhusu mzee kujumuika nao tena,” akasema Bw Masama.