ZARAA: Amegundua siri ya kukuza matunda yanayosakwa mno
Na SAMMY WAWERU
JITIHADA za Josphat Kiarie kupata ajira baada ya kufuzu kwa Stashada ya Uhandisi Masuala ya Maji 2017 zilipogonga mwamba, alijituma kufanya vibarua vya hapa na pale.
Alijitosa katika nyanja ya ujenzi kama fundi wa mabomba jijini Nairobi.
Maisha jijini hata hivyo hayakumuendea alivyotaka, akaamua kurejea mashambani Gacharage, Kandara, Kaunti ya Murang’a anakotoka.
“Nilingilia biashara ya uuzaji kuni kwa viwanda vya majani na shule,” asema.
Ni kupitia jukwaa hilo kusaka riziki alikutana na mmoja wa marafiki zake wa kitambo akamuuliza ikiwa anaweza kumtafutia miche ya matundadamu (tree tomato).
Anasema, ilimgharimu mtaji wa Sh700 pekee.
“Kila mche aliununua Sh100,” afichua.
Hivyo ndivyo Kiarie alijipata katika biashara ya ukuzaji na uuzaji wa miche mbalimbali, ambayo kilele chake kimekuwa kuwa mkulima hodari wa matunda damu. Safari hiyo iling’oa nanga 2020.
Katika kijiji cha Gituya, Kiarie, 28, amepamba nusu ekari kwa mitunda damu isiyopungua 450.
Inayozalisha matunda ni kati ya 200 – 250, mkulima huyu akisisitiza kwamba oda anazopata ni tele kiasi cha kulemewa kutosheleza kiu ya wateja.
“Wanunuzi wanatoka humu Murang’a, Kiambu na Kaunti ya Nairobi wengi wao wakiwa wale wa kijumla,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano shambani mwake.
Tofauti na matunda damu mengine yenye uchachu, ya Kiarie yana utamu wa kipekee anaosisitiza umechochea kuwaniwa sokoni.
Aidha, anasema siri ni kuhakikisha yanakuzwa kupitia mbinu bora na faafu kitaalamu.
Josphat Kiarie katika shamba lake. Matunda yake hutafutwa na wanunuzi wengi akisema ni kutokana na ukulima wake wa ‘kilimohai’ unaofanya matunda yasiwe na uchachu bali utamu wa kipekee. PICHA | SAMMY WAWERU
Mwanzo, anajaribu kila awezavyo kupunguza matumizi ya fatalaiza na dawa zenye kemikali kukabili magonjwa na wadudu.
Hii ina maana kuwa amekumbatia mifumo ya kilimohai, inayojumuisha; mbolea ya mifugo, na endapo lazima apulizie dawa anatumia zile hai.
Pili, akiwa na uzoefu katika uzalishaji wa miche anasisitiza inapaswa kuwa salama dhidi ya magonjwa ya mimea na wadudu.
“Iwe bora; yenye afya, huru kutokana na magonjwa na wadudu kwa sababu miche huyasambaza inapohamishiwa shambani kwa minajili ya upanzi,” afafanua. Akionya kuhusu mdudu hatari aina ya Nematode, Kiarie anasema miche iliyoathirika huwa chocheo la udongo kupata magonjwa na wadudu.
David Kariuki, mtaalamu anasema mazoea kupulizia mimea dawa zenye kemikali ndiyo yamechangia rutuba kudhoofika.
“Udongo unapokua duni, kiwango cha mazao kinashuka. Suluhu si kupulizia mimea dawa zenye kemikali kunawirisha mazao, ila ni kufanyia udongo vipimo kujua virutubisho na madini yanayokosekana yaongezwe,” Muriuki ashauri, akihimiza wakulima kurejelea mifumo asilia.
Kwa sasa, Kiarie anavuna kilo 50 – 60 kila wiki, akisema mazao yake hayajafika kilele. Kilo moja haipungui Sh80.
Hutumia mitandao ya kijamii, hasa Facebook kupitia ukurasa wake wa Green Nurseries kutafutia mazao soko.
Anaendelea kuzalisha miche ya matunda damu, maparachichi, macadamia, strawberry guava, kiwi, karakara, machungwa, pomegranate, maembe, zabibu, kati ya mingineyo.