Connect with us

General News

Amerika, Ulaya zijue shida za kiusalama ziko kila mahali – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Amerika, Ulaya zijue shida za kiusalama ziko kila mahali – Taifa Leo

WANDERI KAMAU: Amerika, Ulaya zijue shida za kiusalama ziko kila mahali

Na WANDERI KAMAU

MNAMO Desemba 30, 2021 serikali ya Uingereza ilitoa tahadhari kwa raia wake dhidi ya kusafiri katika baadhi ya maeneo nchini kutokana na tishio za kiusalama.

Kwenye tahadhari hiyo, Uingereza ilisema kuna uwezekano mkubwa maeneo hayo kukumbwa na mashambulio ya kigaidi wakati wowote baada ya siku hiyo.

Siku chache baadaye, serikali ya Canada ilitoa tahadhari kama iyo hiyo kwa raia wake dhidi ya kusafiri nchini Nigeria.

Kama Uingereza, Canada iliyataja maeneo kadhaa ambayo huenda yangekumbwa na mashambulio ya kigaidi, ghasia za kikabila au visa vya utekajinyara.

Mwanzoni mwa Desemba 2021, Amerika, Canada na Uingereza kwa pamoja zilitoa masharti makali kwa watu wanaosafiri kutoka Nigeria kuingia katika nchi hizo ili “kuwalinda” raia wake dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona aina ya Omicron.

Hizi ni baadhi tu ya “tahadhari” ambazo Amerika na mataifa ya Ulaya zimekuwa zikitoa kwa raia wake dhidi ya kusafiri Afrika pindi tu zinapohisi kutoridhishwa na hali za kiusalama katika mataifa hayo.

Ni hali ambayo imekuwa kama mazoea. Hii si mara ya kwanza, wala huenda isiwe ya mwisho.

Ingawa tahadhari hizo wakati mwingine hulingana na habari za kijasusi kuhusu hali ya usalama katika nchi hizo, maswali yanayoibuka ni: Ni Afrika pekee inayokumbwa na changamoto za kiusalama duniani?

Je, tahadhari hizo zinamaanisha mataifa hayo (Amerika na washirika wake) hazina matatizo yoyote ya kiusalama? Mbona ni Afrika pekee inayochukuliwa kuwa kitovu cha ukosefu wa usalama duniani?

Kimsingi, huu ni mwendelezo wa ukoloni-mamboleo. Ni ubaguzi wa wazi unaoashiria “ghadhabu” fiche ya Amerika na washirika wake dhidi ya Afrika. Amerika na Ulaya si mbinguni. Ni maeneo yanayokumbwa na changamoto sawa au hatari zaidi hata kuliko Afrika.

Mwaka 2020, dunia nzima ilielekeza macho yake nchini Amerika, baada ya polisi Weupe kumuua Mwamerika Mweusi George Floyd kwa tuhuma za kukataa kukamatwa.

Licha ya polisi hao kuhukumiwa na mahakama, ilimlazimu Rais Joe Biden kuiomba msamaha dunia yote kutokana na kisa hicho, ikizingatiwa polisi walionekana wakitenda ukatili huo kwenye video iliyorekodiwa na msichana mdogo aliyeshuhudia tukio hilo.

Kinyume na Amerika, ni vigumu sana kusikia visa vya mtu anayewageukia wenzake kwa ghadhabu na kuwaua kwa kuwafyatulia risasi bila kujali hata kidogo barani Afrika.

Visa kama hivyo pia vimekuwa vikiripotiwa katika baadhi ya nchi za Ulaya.

Ijapokuwa makala haya hayalengi kamwe kuipaka tope Amerika na washirika wake, ni makosa makubwa kwa nchi hizo kutumia ushawishi wao kisiasa na kiuchumi kueneza dhana ya Afrika kuwa kitovu cha kila aina ya maovu.

Hii ni taswira ya nyani kutoona kundule bali kuona la mwenzake. Amerika na Ulaya pia zinazongwa na changamoto si haba za kiusalama.

Kwa kuwa hizi ni changamoto zinazoiathiri dunia yote, tiba yake kuu ni mataifa yote kubuni ushirikiano wa pamoja ili kuzitatua kikamilifu.

Ni nafasi pia ya Amerika na Ulaya kukomesha maonevu yake dhidi ya Afrika.

[email protected]

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending