[ad_1]
Amri meli yenye vifaa hatari itengwe
Na ELVIS ONDIEKI
SERIKALI imeamuru meli moja ya mizigo iliyowasili katika bandari Mombasa kutengwa ikisema inabeba vifaa hatari.
Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe alitoa agizo hilo Jumamosi akisema meli hiyo inabeba vifaa vyenye mionzi hatari.
Alisema meli hiyo, Seago Piraeus na yenye nambari za usajili 174S b/l 214735 ni hatari kwa usalama wa Wakenya kutokana na vifaa ilivyobeba.
Kwenye taarifa, Bw Kagwe aliagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Nishati ya Nuklia (KNRA) nchini na afisa msimamizi masuala ya afya bandarini kukagua meli hiyo pamoja na mizigo iliyobeba.
“Mkurugenzi Mkuu wa KNRA akague kwa kina kilichoko kwenye shehena hiyo kubaini kiwango kilichoko na hali yake,” waziri akaeleza.
Waliokuwa kwenye meli hiyo pia watafanyiwa ukaguzi wa kimatibabu, Kagwe akisisitiza kuwa “sharti wajibu maswali yatakayoibuka kwa mujibu wa Vifungu 60 na 62 vya Sheria ya Afya ya Umma”.
Alisema Kenya ina haki kukagua na kuzuia kuingia nchini vifaa vya kimagendo vyenye mionzi na nguvu hatari za nuklia, pamoja na silaha sugu.
Uchunguzi kupitia tovuti ya vesselfinder.com, unaonyesha meli hiyo ina nembo ya bendera ya Denmark.
Chini ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita, imekuwa Kenya, Oman, India na Pakistani.
Maelezo ya tovuti hiyo yanasema mnamo Desemba 2, meli hiyo ilikuwa Mundra, India.
[ad_2]
Source link